Bw. Alex Msama |
KWAYA ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration ni
miongoni mwa burudani zitakazokuwepo kwenye Tamasha la Pasaka Machi 31,
mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama jana ilieleza kuwa makundi hayo
ya jijini Dar es Salaam tayari yamethibitisha ushiriki wao pamoja na
mwimbaji mahiri Upendo Kilahiro ambaye pia atashiriki.
“Niseme mambo yanaenda vizuri na leo (jana) kuna msanii tunamalizana
naye kutoka Afrika Kusini, nina imani wakati wowote kuanzia Jumanne
(leo) tutamtangaza kwa mashabiki wetu, nia ni kulifanya tamasha liwe
zuri zaidi,” ilisema taarifa hiyo.
Wasanii wengine wa Tanzania watakaoshiriki tamasha hilo ni Rose
Muhando, John Lissu na Upendo Nkone, wakati wa nje ya Tanzania ni
Ephraim Sekeleti wa Zambia anayetamba na albamu zake za Acha Kulia na
Mungu Mwenyewe.
Wasanii wengine wa nje watakaokuja ni Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya, ambapo pia mwaka huu
kuna ingizo jipya ambalo ni kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali
Rwanda inayotamba na albamu ya Mtegemee Yesu.
Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31 na litaendelea
Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa
Samora mkoani Iringa na Aprili 6 itakuwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na
siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Tamasha la mwaka jana liliwashirikisha waimbaji mahiri kama Rose
Muhando, Rebecca Malope, Christina Shusho, Nkone, Kilahiro, Mukubwa,
Atosha Kissava, Sekeleti, kundi la Glorious Celebration, kwaya ya
Kinondoni Revival na Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka DRC.
- Habari Leo -