Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Moses Kulola |
SAKATA la kupotea kwa Askofu wa Evangelism Assemblies of God Tanzania
(EAGT), Lomanus Lukosi (60), anayeishi mjini Makambako Wilaya ya
Wanging’ombe mkoa wa Njombe, limezua mkanganyiko kutokana na kauli
zinazotolewa na kanisa hilo na Jeshi la Polisi.
Mkanganyiko huo unatokana na viongozi wa Jeshi la Polisi na kanisa
hilo kwa nyakati tofauti kusema askofu huyo alipatikana jana na
anawasiliana na familia yake kutoka sehemu alikojificha kwa ajili ya
kufanya maombi ingawa hajaonekana hadharani.
Katibu Mkuu wa EAGT, Askofu Brown Mwakipesile, alisema baadhi ya
viongozi wa kanisa hilo akiwamo katibu wa askofu huyo wamepewa jukumu la
kushughulikia suala la kupotea Askofu Lukosi.
Alisema hadi jana Askofu Lukosi amekuwa akiwasiliana na familia yake kutoka mahali alikojificha kwa ajili ya maombi.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Moses Kulola, alipotafutwa
jana kuelezea tukio hilo, simu yake ilipokelewa na mtu
ambaye alijibu kuwa askofu hajajulishwa na wasaidizi wake kuhusiana na
tukio hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani, alisema
askofu huyo hajapatikana ingawa anaendelea kuwasiliana na familia yake
akiwa katika eneo ambalo halijulikani.
Naye Mchungaji Asimbagwe Mwaisabila wa kanisa hilo, akizungumza na
NIPASHE kutoka Sumbawanga alisema amewasiliana na viongozi wenzake
waliopo Makambako ambao walimweleza kuwa amepatikana.
“Mimi ni mmoja wa watu tuliokuwa tunafuatilia suala hili,
nimewasiliana na wenzangu wanasema askofu amepatikana ingawa sijafahamu
kama ni kweli au la maana wanasema anawasiliana na familia yake,”
alisema.
- Nipashe -