Siku moja mama Allen (hili siyo jina lake halisi) alianza
kunishirikisha mambo ya ndoa yake yanavyomtesa. Akaniambia mwanangu hizi
ndoa tunapenda tu kuingia bila kujua kilichomo ndani yake. Hivi
unavyoniona sina hamu kabisa ya ndoa, maana maisha tunayoishi (ingawa
kwa nje watu wanaona tuko pamoja), lakini ukweli ni maisha ya taabu na
majuto karibu kila siku.
Tabia ya mume wangu imefika mahali haivumiliki. Nikamuuliza tatizo ni nini hasa? Akasema ni fedha, elimu yake na kutoka nje ya ndoa.
Fedha ya mume wangu wanaijua wazazi wake na si wazazi wangu, kwani mara
kwa mara yeye hutuma fedha kwa wazazi wake. Inaniuma maana natamani
hata mie wazazi wangu niwatumie fedha pia.
Mume wangu ni kweli Mungu kamjalia kuwa na
elimu ya kutosha, lakini elimu yake imekuwa dharau kwangu nisiye ana
elimu kama yake. Maana hunisema kwa sababu ya elimu yangu ndogo, kazi
yangu na mshahara wangu mdogo ukilinganisha na wake. Kubwa na baya Baba
Allen sio mwaminifu katika ndoa, sina amani na hasa ukizingatia ugonjwa
huu wa ukimwi, nina mashaka makubwa sana ndani yangu.
Nikamuuliza umefanya jitihada gani ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizi za ndoa yako? Akajibu akasema nimeamua kuishi naye kwa kuzikubali tofauti zetu (agree to differ).
Kwa lugha nyingine nimekubali kuishi na hali hii, kwamba haya ndiyo
maisha yangu ya ndoa chini ya jua. Hivyo imefika mahali sina jingine la
kufanya ila kukubali kwamba mwenzangu yuko vile na mimi niko hivi,
tutendelea kuishi kwa kutofautina hadi kifi kitutenganishe, kwani
jitihada za kujaribu kurekebisha mambo haya zimekwama.
Baada ya kusikia maelezo haya niliumia sana, nikamshauri mambo kadhaa
ya kufanya ili kuiponya ndoa yake. Lengo langu la msingi katika
kuandika habari za mama Allen ni kujaribu kukufukirisha mwanandoa
mwenzangu mambo kadhaa yatakayokusaidia kuiponya ndoa yako pia;
- Jambo la kwanza – Ndoa ni wito wa upungufu na hivyo suala la uvumilivu ni la lazima.
Si watu wengi wanaojua kwamba ndoa ni wito wa mapungufu pia. Maandiko yanasema ‘ Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja’ (Mwanzo 2:24).
Ni dhahiri kwamba watu wanapooana wanakuwa wametoka katika asili na
malezi (background) tofauti hasa kutokana na mazingira waliyokulia. Ile
tu kwamba huyu anatoka katika familia hii na huyu ile, fahamu kwamba
lazima kutakuwa na tofauti kadhaa katika ndoa hiyo. Naam tofauti zenu
ndiyo sehemu ya mapungufu kwenu kama wanandoa. kwa sababu wewe
ungependa mwenzako awe hivi na yeye kuna vitu ambavyo angependa
vibadilike kwako.
Na wala usije ukajiona wewe upo kamili, naam kwa upande wako unaweza
kuwa sawa lakini kwa mwenzako, hauko kamili. Ni vizuri ukafahamu kwamba
unapoingia kwenye ndoa, utakabilana na mapungufu ya mwenzi wako. Kwa
sababu hii suala la uvumilivu, kuchukuliana, kusameheana kwa wanandoa ni
la msingi ili kufikia mahala pa kutengeneza tabia au mfumo mpya wa ndoa
yenu.
- Jambo la pili – Haijalishi mwenzi wako anatabia mbaya kiasi gani, Yesu anaweza kumbadilisha.
Jambo la pili ambalo nimeoana vema kusisitiza ni kwamba wewe mama au
baba ambaye ndoa yako ipo kwenye misukosuko kama ya mama Allen pengine
na kuzidi, usifike mahala pa kukata tamaa na kuamua kuishi kwa
kuzikubali tofauti zenu kama sehemu ya maisha. Kwa kufanya hivyo utakuwa
unamzuia Roho Mtakatifu kukusaidia kuiponya ndoa yako. Ni lazima kwanza
ubadili fikra zako na mtazamo wako kwamba, kwa Mungu hakuna
lisilowezekana na hivyo haya si maisha yangu ya ndoa ninayostahili
kuyaishi.
Kwa Mungu sisi tu watoto wake. Hakuna Baba mwenye kufurahia kuona
maisha ya ndoa ya watoto wake yanakuwa ya majuto. Mungu alipoleta wazo
la ndoa ilikuwa ni kwa ajili ya kusudi la ufalme wake na kuwa furaha kwa
watoto wake na si majuto. Nasikitika kusema leo, ndoa nyingi zimekuwa
ni majuto na si kile Mungu alikiona wakati wa uumbaji hata akasema, kila
kitu nilichokifanya ni chema sana (Mwanzo 1:31).
Kwa kilio kilichopo kwenye ndoa hivi sasa ni dhahiri kwamba kuna
mahali kama wanandoa tumekosea na kumpa Iblisi nafasi (Waefeso 4:27)
hata ameleta majuto kiasi hiki. Ushauri wangu ni kwamba ni vema kila
mwanandoa akasimama kwenye nafasi zake (Mwanaume kama kichwa na Mwanamke
kama Mlinzi na Msaidizi nk) kwa pamoja tumpinge Shetani naye
atatukimbia. Endapo mwenzi wako hayuko tayari kwa hili au hamjui Mungu
wako, basi wewe mwenye kujua siri hii kama anza, maana kwa Mungu mtu
mmoja natosha kuleta uponyaji wa Taifa, je si zaidi ndoa yako? Naam
usikate tamaa, Mungu wetu, ni MUNGU ASIYESHINDWA.
Bwana Mungu na akusaidie katika kuzikabili changamoto za ndoa yako!
Mwl. Patrick Samson Sanga
0755 816800