MCHAKATO rasmi wa kumpata kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani
atakayemrithi Papa Benedict XVI aliyejiuzulu Februari 28, unaanza
kesho. Katika mchakato huo, makardinali 115 wataingia kwenye Kanisa la
Sistine kwa kazi hiyo ngumu ya kupiga kura.
Kura hiyo ya siri inatarajiwa kurudiwa mara kadhaa hadi apatikane mtu anayekubalika. Tayari kanuni za uchaguzi huo zimeshaandaliwa zikiwamo za namna ya kupiga kura kwa usiri na wasimamizi wa kura.
Makardinali hao kutoka mataifa mbalimbali duniani, wamekuwapo Vatican ambako kila walipowasili walikula kiapo cha kutunza siri wakati wote wa kikao hicho muhimu. Viongozi hao wa kidini, wataongozwa zaidi na sala na maombi kwa roho mtakatifu.
Kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, kampeni haziruhusiwi katika mchakato huu mzima. Kukosekana kwa kampeni, hata hivyo, hakuzuii watu kutoa mawazo yao kuhusu nani angefaa kuchaguliwa.
Wengine wanaipa nafasi kubwa Italia, yaliko makao makuu ya kanisa hilo, Vatican, ingawa pia kuna wale wanaofikiri kuwa sasa ni zamu ya Afrika na Amerika Kusini kutoa kiongozi wa juu wa kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.2.
Pia, wengine wanadhani kuwa Ulaya, ambayo ina
makardinali wengi zaidi, bado inastahili kutoa kiongozi huyo kama
ilivyokuwa kwa Poland na Ujerumani katika miaka ya hivi karibuni.
Kwanini Afrika?
Sababu ya msingi inayotajwa kuipendelea Afrika kwa sasa ni, ongezeko la waumini wapya ambako takwimu zinaonyesha kuwa nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tanzania, Uganda zimo katika orodha ya 20 bora duniani kwa waumini wengi wa Kikatoliki.
Afrika na Amerika Kusini, zikilinganishwa na mabara ya Ulaya na Marekani, zinaelezwa kuwa zina idadi kubwa ya waumini wapya , makanisa yake yanajaa, idadi ya mapadri inaongezeka, tofauti na Ulaya na Marekani inakopungua.
Makardinali wawili, Francis Arinze mwenye umri wa miaka 80, raia wa Nigeria na mwenzake, Peter Turkson (64) kutoka Ghana, wamekuwa wakitajwa kuwa miongoni mwa wale wanaofaa kwa kazi hiyo. Wakati wote wa mchakato huo, makardinali hao 115 hawatakuwa na mawasiliano yoyote na ulimwengu wa nje hadi apatikane papa mpya ndani ya wiki mbili.
Kwa pamoja, wataishi katika hosteli ya kisasa iliyomo ndani ya eneo hilo, umbali mdogo kutoka katika Kanisa la Sistine, ambalo milango na madirisha yake yamezibwa kuzuia watu kuchungulia ndani yake.
Hosteli hiyo ya kisasa inayojitegemea, imeandaliwa mahsusi kwa kazi hiyo, ikiwa na huduma zote za msingi. Ina madaktari, mapadri ambao watawahudumia makardinali hao wakihitajika.
Kila kardinali ataishi katika chumba chake kidogo chenye kitanda, meza ndogo na kabati la nguo, akisali zaidi na wakati huo akifanya tafakuri ya kina kati yake na Mungu ni nani hasa kati yao aliyeteuliwa kuliongoza kanisa hilo.
Inaelezwa kuwa wakati wote wa mchakato, makardinali hao hawazungumzi, bali kusali na kufanya tafakuri na kukutana wakati wa chakula.
Ni nchi gani zinawakilishwa?
Zipo nchi kadhaa ambazo zina uwakilishi katika uchaguzi huo. Hizi ni pamoja na: Italia (28), Marekani (11), Ujerumani (6), Hispania, India, Brazil (5) kila moja, Ufaransa, Poland (4) kila moja Mexico, Canada (3) kila moja Ureno, Nigeria, Argentina ( 2) kila moja.
Australia, Austria, Ubelgiji, Bolivia, Bosnia Herzegovina, Chile, China, DR Congo, Colombia, Croatia, Cuba,Czech , Dominica, Ecuador, Misri, Ghana, Guinea,Honduras, Hungary, Ireland, Kenya,Lebanon, Lithuania, Uholanzi, Peru, Ufilipino, Senegal, Slovenia, Afrika Kusini, Sri Lanka, Sudan, Uswisi, Tanzania, Venezuela, Vietnam (1) kila moja.
- Mwananchi -