JAMBO LA SITA
Uamuzi wa kuoa au kuolewa unaweza wakati mwingine
kukuletea marafiki au maadui.
Uamuzi wa kuoa au kuolewa unaweza wakati mwingine
kukuletea marafiki au maadui.
Sasa nakufikirisha hivi vitu vikusaidie, inawezekana kabisa hujafikia
umri wa kuoa au kuolewa, lakini ninakuambia weka maombi yako ya akiba,
(sijui kwa upande wako, lakini mara nyingine huwa nawaombea watoto wangu
maombi ya akiba, kwa ajili ya ndoa zao kama Yesu atakuwa hajarudi, kwa
sababu najua maana yake ni nini).
Ni vizuri upate maombi ya namna hii mara kwa mara – ujiombee
mwenyewe, ukipata watu wa kukuombea shukuru Mungu, lakini hata kama
hujapata watu wa kukuombea, ninakuambia kazana kujiwekea maombi ya
akiba. Hiyo ni njia panda. Mahali pa kuoa au kuolewa ni njia panda.
Ukichagua njia ambayo haiko sawasawa, maisha yako yatakuwa magumu sana.
Sasa ukiangalia kwenye kitabu cha Hesabu.12:1-2 inatuonesha wazi
kabisa ya kwamba, harusi ya Musa ilileta ugomvi katikati yake na ndugu
zake, hasa dada yake na Haruni. Kilichowasumbua ni kwamba alikwenda kuoa
mwanamke Mkushi; au amekwenda kuoa mahali ambako hawakutarajia, kwa
hiyo wakakasirika. Halafu naamini Musa aliwaambia Mungu amesema naye juu
ya kuoa mke huyu, wale watu wakasema, ‘Mungu anasema na Musa tu peke
yake, haiwezekani’ – ugomvi ukaingia.
Unajua ugomvi uliingia kiasi ambacho Mungu akasikia yale maneno na
hayakumfurahisha, akawaita kwenye hema. Ikabidi ajieleze wazi uhusiano
wake na Musa.
Kitabu cha Hesabu 12:6-8 kinasema; “Kisha akawaambia, Sikilizeni basi
maneno basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA,
nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo
kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;
kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na
umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa kumnenea
mtumishi wangu, huyo Musa?” Alivyomaliza kusema namna hiyo dada yake
Musa akapata ukoma!
Ugomvi umetokea wapi? Musa alipooa! Kwa kuwa ameoa msichana ambaye
dada yake hakumtaka. Mungu alimtaka, lakini dada yake hakumtaka. Dada
mtu akaanza kumsema kaka yake, Mungu akampa adhabu! Dada mtu alipopewa
adhabu ile na kaka mtu akapata shida, Israeli nzima ikapata shida,
hawakusafiri walisimama wote, hawakuendelea na safari. Ugomvi ulitokea
wapi?
Ulitokea mtu mmoja alipooa!
Nimeona ndoa zingine kijana anaoa lakini uhusiano wake na baba yake
na mama yake unakatika wakati huo huo. Vijana wengine wanakuwa hawako
waangalifu hapo, na ndio maana mambo yakiwa magumu, na wazazi
wanawabishia juu ya kuoa au kuolewa kwao hawataki kwenda kuzungumza na
wazazi wao; wanapiga ‘short cut’, wazazi wao wanakuja kuambiwa tu saa na
tarehe ya harusi!
Biblia inasema, “waheshimu baba na mama yako, hii ni amri ya kwanza
yenye ahadi ili upewe siku nyingi katika nchi upewayo na Mungu wako”
(Waefeso 6:1). Na kwa sababu hiyo vijana wengi sana wakiishakorofishana
wazazi wao hawaendelei katika ndoa muda mrefu wakiwa na amani.
Sasa sisemi kwamba wamkubali tu huyo msichana au huyo kijana, ni
zaidi ya hapo unajua. Suala ninalozungumzia hapa ni la wao kukupa
kibali, na wakafurahi. Unaweza ukasema, hawaelewi kitu au hawajaokoka,
kwa hiyo hawahitaji kuelezwa kitu. Hapana!
Ndio maana unahitaji kuomba. Kwa sababu unajua suala la kutaka kuleta
msichana au kijana ndani, sio la kwako peke yako, linawahusu wazazi
wako na ndugu zako kwa sababu unawaingiza kwenye familia nyingine. Hata
kama unataka kuoa au unataka kuolewa, ni mambo ya kifamilia maana ni koo
mbili zinakutanishwa na kuunganishwa.
Wakati mwingine unaunganisha kabila mbili au unaunganisha kabila
tatu, (wengine hawaelewi kitu ninachosema, kwa mfano; “Mimi ni
mnyakyusa, mke wangu ni msukuma, watoto wangu ni kabila gani”?
Wanakabila mbili, ni mchanganyiko wa wanyakyusa na wasukuma, maana
ningetaka kujipendelea ningesema ni wanyakyusa.
Lakini ndani wanaunyakyusa na wanausukuma halafu waolewe na mtu wa
kabila lingine ambalo sio mnyakyusa wala sio msukuma, ni makabila
mangapi yanaungana hapo, matatu! Sasa fikiria na anayeoa kwangu na yeye
awe ametoka kwenye mchanganyiko wa namna hiyo.
Unaunganisha hapo makabila matatu, manne, matano, sasa wewe unataka
wazazi wako wasiifuatilie ndoa hiyo kwa karibu. Kwa nini? Ukipata shida
utarudi kwa wazazi wako, sasa kwa nini wakati wa maamuzi wasikusaidie!
Na mimi ninakuambia iko njia ya kutokea, ikiwa utapata tatizo la
namna hii; wewe kukaa kwenye maombi kwa namna ambavyo, kama ni Mungu
kweli aliyekupa huyo msichana au aliyekupa huyo kijana, basi ataweka
kibali hicho hicho ndani ya wazazi wako, ili na wao wamkubali.
Saa nyingine unaweza ukapata marafiki wengine wazuri, lakini wakati
mwingine marafiki wengine wanakuwa ni wabaya. Maana ukishaolewa marafiki
wa mume wako ni marafiki zako, ukishaoa marafiki wa msichana ni
marafiki zako. Vijana siku hizi wanaotaka kuoa au kuolewa wakitaka kujua
ukoje, hawakuangalii wewe wanaangalia marafiki zako. Marafiki ulionao
ndio wanaoonyesha picha uliyonayo ndani yako.
Rafiki wa kweli hafuati pesa ulizonazo, anafuata tabia uliyo nayo,
wale marafiki wanaokufuata kwa sababu unacho kitu cha kuwapa hao sio
marafiki, wanakufuata kwa sababu unachokitu, siku ukiishiwa huwaoni.
Lakini wale marafiki unakuwa nao wakati wa shida na wakati wa raha, ni
marafiki ambao malengo yenu na tabia zenu, kufikiri kwenu kusema kwenu
zinafanana. Hao ndio marafiki ambao wanakuwa marafiki zako wa kweli;
siku ukiwa na shida ni marafiki zako, unahela ni marafiki zako,
umefilisika ni marafiki zako, hao ndio marafiki zako!
Sasa kama mtu anataka kukuangalia ulivyo, anaangalia marafiki zako.
Sasa, akiangalia marafiki zako, hata kama unasema, ‘Bwana asifiwe’, hata
kama unapiga pambio mpaka jasho la damu linatoka, lakini wanaangalia
marafiki zako ulionao, na wakati mwingine ni wabaya kuliko wale wa kule
duniani, wanajua na huyu msichana au huyu mvulana kuna mahali ‘ana
short’.
Kwa wengine inakuwa vigumu kuliona kwa namna hii, lakini ni lazima
ufahamu ukiwa kama kijana, lazima uwe mwangalifu juu ya marafiki
ulionao. Vijana wengine wanabaki kushangaa kwa nini wasichana
wanahangaika wanasema hatuoni vijana wa kuwaoa, wakati vijana wapo,
lakini nani ataolewa na vijana ambao wameokoka lakini hawana msimamo?
Nani anataka kijana wa namna hiyo ambaye anashinda vijiweni sawasawa na
hao vijana wengine wa duniani?
Mwanaume akitaka kuoa lazima ajifunze kuwajibika. Hawezi akawa na
marafiki ambao hawawajibiki kimaisha – na akataka aone na aendelee na
urafiki nao. Akiwa karibu na hao marafiki, itakuwa ni vigumu kuwa na
ndoa yenye amani. Angalia tu marafiki alionao, unashangaa kwamba
anaendelea kusema bado ameokoka.
Unashangaa wale marafiki alionao,
hawafananii, hawawezi hata kumtia moyo kuomba, hawawezi kumtia moyo
kusoma neno, vitu wanavyozungumza ni vitu vya ajabu.
Unajua, hata wakati mmoja hawana maneno ya kutiana moyo ya kuwa na
maendeleo binafsi, lakini ndio anaoshinda nao toka asubuhi mpaka jioni,
halafu anataka kuoa msichana ambaye ameokoka, anayeshinda kwa Mungu ,
anayekaa kwenye maombi, anayetaka kuona cha Mungu kinasimama katika
maisha yake, ndiye anataka kwenda kwake ili amuoe;- hii siyo sawa! Ndoa
yao itakuwa na matatizo tu kwa muda mrefu.
Maana usije ukapata shida ukiingia kwenye ndoa na kijana wa namna
hiyo. Wewe uliona kabisa marafiki zake walivyo, unaolewa na ndipo
unaposema, ‘mimi sitaki hao marafiki zako’! Imeanza wapi? Atakuambia
vizuri kabisa “ulinikuta nao”, kwa nini hukusema mapema kabla hatujaoana
ya kuwa huwataki?
Msichana anaolewa na ndipo kijana anamwambia hao marafiki zako
nisiwaone hapa, lakini alikuwa anawakuta chumbani kwako wakati alipokuwa
anakuja kukutembelea na hakusema kitu, na wakati mambo yakiwa magumu
katikati yenu alikuwa anawatumia wao kukubembeleza ukubali kuolewa naye,
sasa umekwishaolewa hawataki. Anaanza kuwasema ya kuwa tabia zao sio
nzuri. Hili jambo si zuri; alitakiwa aseme mapema juu ya kutoridhika
kwake na rafiki zake.
Unapotaka kuoa au kuolewa, usifikirie tu picha ya yule mtu wakumuoa
au kuolewa naye, ni vizuri kuangalia na aina ya marafiki zake wa karibu –
je unaweza kuchukuliana nao?.