James Kalekwa |
Somo linaendelea....
Kusoma sehemu ya Pili, Bofya Hapa
Mathayo 12:35
"Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu
mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya."
Wakati fulani nilikuwa ninafundisha vijana kwenye mkoa
fulani na hapo nilipata kuwatambulisha kwenye kanuni moja muhimu sana ambayo
huwa ninaiita kanuni ya mavuno… Moja ya msingi wa kanuni hiyo ni kwamba: Huwezi
kuvuna mazao yaliyo tofauti na mbegu uliyopanda! Kama una nafasi naomba uirejee
sentensi hiyo, “HUWEZI KUVUNA MAZAO YALIYO TOFAUTI NA MBEGU ULIYOPANDA.” .
Iwapo umepanda
njegere, hupaswi kutarajia kuvuna pamba… Haiwezi kutokea!!!
Kitu ninachotamani utunze kwenye maisha yako ni kwamba
ni kweli moyo wako huamua mtiririko/mwenendo wa maisha yako lakini hii siyo “automatic”… Haitokei hewani hewani tu.
Nafsi hulishwa na milango ya fahamu…
Kwahiyo kama unataka kulinda nafsi yako,
chunga sana mahali unakoielekeza milango yako ya fahamu kwasababu ni kwa njia
hiyo ndiyo utapanda mbegu ndani ya nafsi; ndiyo utaongeza pesa kwenye akiba
yako ya nafsi.
Mwanadamu ana milango mitano ya fahamu: macho, pua, ngozi,
ulimi na masikio ambayo kwa pamoja hupeleka taarifa ndani ya nafsi tayari kwaajili
ya kutendewa kazi. Kwa maneno mengine ni kwamba mwanadamu huweka akiba ama
huongeza salio ndani ya akaunti ya maisha yake, au hupanda mbegu ndani ya
shamba la nafsi yake kwa njia ya milango ya fahamu. Kile unachokiona na kusikia
katika vyombo mbalimbali vya habari, unachokisoma na kile ambacho unakihisi kwa
njia ya ngozi yako huwasilishwa nafsini mwako na hicho ndicho baadaye huamua
mtiririko wa maisha yako.
Wakati fulani nikiwa Arusha kama moja ya wawezeshaji
kwenye kongamano la vijana, nilizungumza juu ya dhana ya utandawazi kwa mtazamo
wa kitaaluma na neno la Mungu.
Niliwaambia vijana kuwa kwenye maduka ya vitabu
(bookshops) kuna aina mbalimbali za vitabu, je , wao husoma vitabu gani?
Unasoma magazeti, majarida, vijitabu gani…
Unasoma machapisho gani? Kwenye
mtandao wa internet kuna tovuti, blogs, na mitandao mingi ya kijamii, je, wao
hutembelea au hushiriki kwenye mitandao gani? Kwenye ulimwengu wa habari kuna
vyombo mbalimbali vya habari, je, wao husikiliza vyombo gani na husikiliza
habari gani? Je, huchagua kusikiliza mazungumzo gani au huwa na marafiki wenye
mazungumzo gani? Unasikiliza nyimbo, hotuba, mafundisho gani? Unatazama sinema,
tamthiliya, michezo gani?... Swali langu kubwa kwako ni UMEELEKEZA WAPI MILANGO
YAKO YA FAHAMU?
Kama umetoa jibu, juu ya maswali mengi yaliyotangulia hapo juu,
basi hongera kwasababu umetambua kule ulikoelekeza milango yako ya fahamu!
Lakini hiyo haitoshi ndugu yangu….
Ni kwa njia ya milango ya fahamu kwamba taarifa
huletwa nafsini na kisha hutunzwa kama hazina na taratibu huanza kutumiwa kama
wazo.
Kabla mtu hajadhihirisha chochote, tambua huwa anawaza… Anawaza kwa
kutumia akiba iliyoongezwa au kwa kutumia mbegu iliyopandwa kwa njia ya milango
ya fahamu.
Mfumo wa
maisha ya binadamu hujizungusha katika mtirirko niliouwasilisha hapo juu.
Kwanza huanza mawazo ambayo baada ya kukomaa hufanyika maneno… baada ya maneno
kukua hayo hufanyika matendo ambayo baada ya muda hujengeka na kuwa tabia
ambayo hiyo huamua mfumo wa maisha. Nitaeleza hatua moja baada ya nyingine kwa
utaratibu na kwa mifano kadhaa ili kukusaidia kuelewa vyema.
Mawazo
Je, ndugu
msomaji unaelewa nini kuhusu biashara ya kimataifa? Je, nini mtazamo wako
kuhusu mgogoro wa Mashariki ya kati (Israeli na Palestina)? Je, msimamo wako
kuhusu hali ya siasa za Tanzania ni upi? Vipi uelewa wako kuhusu maisha ya
ndoa? Unasemaje kuhusu nafasi ya kanisa kwenye jamii? Pindi usikiapo neno
uwekezaji huwa unaelewa nini?
Kama
umeweza kujibu maswali hayo, basi umeweza kuyatambua mawazo yako juu ya
mazingira niliyokutambulisha kwayo. Kwa ujumla wake, mawazo ni hali ya ndani ya
nafsi ya mtu binafsi (state of mind) juu ya hali, mtu, mazingira fulani. Hali
hiyo ya ndani huamua uelekeo wa mtu huyo kuhusiana na nyanja mbalimbali za
kimaisha. Naomba nikujulishe mapema ya kwamba kuna mawazo ya muda mrefu na yale
ya kitambo, muda mfupi tu…
Na mara nyingi mawazo ya muda mfupi yasipotendewa
kazi na kutunzwa hupoteza nguvu ya kuongoza mwelekeo wa maisha ya mtu. Mawazo
ya muda mrefu, amabayo hufanyiwa kazi na kutunzwa, hayo huunda mtazamo wa mtu
juu ya swala fulani… Hayo ndiyo mawazo ninayoyazungumza hapa. Kwahiyo unaweza
kugundua tu ya kwamba tunaposema mawazo kamwe hatumaanishi hali ya kuwa na
msongo (stress) au kuzama kwenye lindi la kifikra bali uelewa wa ujumla wa mtu
binafsi juu ya jambo fulani!
Ili uweze
kudumu na kuendelea kusimama katika wokovu uwe makini na mawazo yako kwa ujumla
si tu juu ya wokovu bali juu ya nyanja zote za kimaisha. Sasa ni kwa namna gani
unaweza kushughulika na mawazo yako mwenyewe… si kazi ngumu sana!
Lazima
utambue ya kwamba mawazo huja kwa njia moja tu nayo ni MILANGO YA FAHAMU!
Kwahiyo ili uweze kuyaongoza mawazo yako, ni lazima uwe makini kuongoza milango
yako ya fahamu dhidi ya vyanzo vya taarifa. Hebu nikuonyeshe mambo kadhaa kisha
tufanye mjadala kwa upana juu ya mawazo.
Somo litaendelea Jumatatu Ijayo....
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu, na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu, na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com