Kanisa la Baptist Vingunguti |
KANISA la Baptist, lililoko Vingunguti jijini Dar es Salaam
limechomwa moto usiku wa kuamkia Jana ambapo vitambaa na madhabahu
vimeteketea kwa moto.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Marietha Minangi amesema kuwa, tukio hilo limetokea usiku wa saa nane, na hadi
anazungumza na mwandishi, hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa kuhusiana na tukio
hilo.
Kamanda Minangi alisema, ilikuwa mapema mno kuhusisha tukio
hilo na tofauti za imani za kidini. Alisema, polisi wanaendelea na uchunguzi.
Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Hezron Mwaisemba
alimwambia mwandishi wa habari hizi kanisani hapo, kuwa wakiwa wamelala usiku
kama saa nane na robo hivi, binti mwenye umri wa zaidi ya miaka ishirini
aliwaamsha na kuwaambia kuwa, ameambiwa kanisa linawaka moto.
“Tuliamka na kuelekea kanisani, tukakuta kweli kanisa
linaungua. Yule binti alituambia aligongewa dirisha na motto wa jirani
akamwambia kuwa kanisa linawaka moto. Basi, tulipofika hapa tukakuta meza moja
pamoja na ile ya madhabahuni vimeteketea kabisa.
"Tulikuta kisu na kiberiti na pembeni pale kulikuwa na moto
walikusanya maboksi wakayachoma, naona lengo lilikuwa kuteketeza kabisa jengo
hili. Kwa bahati nzuri tulifanikiwa kuzima moto kwa kutumia mchanga,” alisema
Mchungaji Mwaisemba.
Mchungaji huyo alisema kuwa, tangu kanisa hilo lijengwe
mahali pale mwaka 1992 limekuwa na uhusiano mzuri na majirani, hivyo
wameshangazwa na kitendo hicho.
“Sijui huyo mtu au watu waliofanya kitendo hiki walikuwa na
sababu gani. Sisi hapa tuna uhusiano mzuri sana na jamii yote hapa Vingunguti,”
alisema.
Mchungaji huyo alisema kuwa, thamani ya vitu vilivyoungua
moto inaweza kufika shilingi 200,000/=.
Hata hivyo, Mchungaji Mwaisemba alilalamika kuwa, ukiacha
tukio hilo la kuchomwa moto kanisa lake lenye waumini wapatao 150
linakabiliwa na matukio mengi ya wizi, ambapo watu wasiojulikana wamekuwa
wakifika kanisani hapo usiku na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo viti
vinavyotumiwa na watoto wa shule ya awali inayomilikiwa na kanisa.
- Funguka Sasa -