Mch. Josephat Gwajima akihojiwa na Deo Mosha wa Radio Sauti ya Injili - Moshi |
Mchungaji Josephat Gwajima ambaye ni Mchungaji kiongozi wa kanisa la Glory Of Christ Tanzania Church maarufu kama Nyumba ya Ufufuo na Uzima lenye makao yake makuu Kawe, jijini Dar es Salaam; asubuhi ya jana amefanya mahojiano
na Mtangazaji wa Radio Sauti ya Injili iliyopo mjini Moshi huku akiweka bayana maswala kadhaa kuhusu Huduma hiyo.
Akieleza changamoto alizokutana nazo katika mkutano wa Injili wa Arusha,
Mch. Gwajima alisema kuwa changamoto zipo, kwasababu ya ukweli kuwa
mkutano wa injili ni mjumuiko wa mambo mengi sana. Akitolea mfano wa
Mkutano wa kanisa hilo jijini Arusha, Mch. Gwajima alisema,
"tumesafirisha vyombo vya mziki roli mbili na mabasi yaliyobeba
wachungaji wapatao mia mbili kutoka Dar es Salaam waliokuja kwa ajili ya
kuhudumia watu, kwa maana hiyo hizo gharama zote ni changamoto kwetu"
Pia alisema, "kanisa la Ufufuo na Uzima linajitegemea katika mikutano
yake bila kutegemea wafadhili kutoka nje ya nchi kwa maana hiyo
changamoto bado ni kubwa kwetu."
Akiongelea Mkutano wa Moshi unaotarajiwa kuanza tarehe 20 hadi 27
Oktoba, alisema kuwa mkutano huo utakuwa wa maajabu na miujiza ya kupita
kawaida, na akawaasa watu wa Moshi kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia
waliokuwa msukuleni wakirudishwa na waliokufa kurudi kwenye uhai wao
tena.
Alipoulizwa kwa habari za Misukule na kufufua watu waliokufa; Mch
Gwajima alisema kuwa kazi hii si ya mtu mmoja bali ni kazi ya Bwana Yesu
ambayo Mtu yeyote wa Mungu atakayeamua kufufua na kurudisha; Mungu
atamtumia kwa nguvu ile ile. Akitoa andiko kutoka katika kitabu cha Mathayo 10:8;
alisema kuwa Biblia iko wazi sana kwa habari ya kufufua watu waliokufa;
na kusema kuwa tatizo la waafrika wengi ni vile wanashindwa kuthamini
kitu kikubwa ambacho Mungu anakianzisha kwao.
Mwisho, alitoa wito kwa Wachungaji vijana kwa kusema kuwa "Yatupasa
kuifanya kazi ya BWANA kungali bado asubuhi maana saa inakuja ambayo
hatoweza mtu kuifanya". Kwa maneno hayo aliwaasa vijana kuifanya kazi ya
Mungu wangali vijana kwasababu mtu akianza kazi ujanani anapata muda
mzuri wa kusahihisha makosa yake lakini akianza kazi uzeeni atakosa muda
wa kusahihisha makosa na hivyo kushindwa kufanya vizuri.
- Ufufuo na Uzima Blog -