Askofu Mkuu wa kanisa la Africa Independent Pentecostal Church of Kenya, AIPCK, John Baptista Mugecha Karume (katikati) |
WAKENYA wengi wanaendelea kumhimiza Rais
Uhuru Kenyatta asihudhurie kesi inayomwandama katika mahakama ya
kimataifa ya Uhalifu (ICC), huku Novemba ikikaribia ambapo Rais Kenyatta
anahitajika kusafiri Uholanzi kwa kesi hiyo.
Baadhi ya viongozi na waumini wa Kanisa la African Independent Pentecostal Church of Kenya (AIPCK), katika ibada yao waliomba Rais Kenyatta asihudhurie kesi hiyo na wakamhakikishia kumuunga mkono kama kiongozi wao.
Walisema kuwa
kiongozi wa mashtaka Fatou Bensouda alikuwa anapoteza muda wa viongozi
wawili wa nchi ya Kenya, Rais Uhuru na Naibu wake William Ruto, kwa kesi
ambayo haina uzito wowote.
Wakiongozwa
na Askofu Mkuu Mugecha Karume, Mwenyekiti Nchini Simon Kimani na
Mwekahazina George Njuruba walisema kuwa kesi hiyo ilikuwa na mambo
mengi yasiyoeleweka na hakukuwa na haki yoyote kwa kesi hiyo kuendelea.
Askofu Mkuu
Mugecha aliomba Mkuu wa Sheria Githu Muigai na wakili wengine kuangalia
katiba ya Kenya kwa undani ili kutoa viongozi walio humo ICC kutoka kesi
hiyo.
“Wakenya
walichagua Rais Uhuru kwa sababu wana imani naye, na hivyo basi kesi ya
ICC inaendelea dhidi ya viongozi wa nchi kinyume na katiba ya Kenya,”
walisema.
Bw Njuruba aliongeza, “Tunataka vongozi hawa wawili kuwa nchini ili wafanye kazi ambayo Wakenya waliwapatia kwa kuwachagua.”
Zaidi ya haya, walifanya dua kwa walioaga katika mkasa wa Westgate na kesi hiyo ya ICC katika ibada iliyokuwa katika Kanisa la AIPCK la Githunguri, Kiambu.
Wengine
waliokuwa katika ibada hiyo ni: Naibu wa Gavana wa Kiambu Gerald
Githinji, Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu Nyokabi Gatheca na
Mbunge wa Kiambu Mjini Jude Njomo.
Bi Nyokabi na Bw Githinji waliomba Wakenya waendelee na maombi ili nchi iwe na amani wakati wote, hata kesi za ICC zinapoendelea.
Mwishoni mwa
wiki, kundi la Mururumo Mashaninani kupitia kiongozi Caleb Warari pia
lilimtaka Rais Kenyatta apuuze kesi hiyo dhidi yake.