James Kalekwa |
Somo linaendelea....
Kusoma Sehemu ya Tatu, Bofya Hapa
Hesabu
14:1-5
“Mkutano
wote wakapaza sauti zao wakilia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha Wana wa
Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakamwambia,
Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchiya Misri, au, ingekuwa heri kama
tungalikufa katika jangwa hili. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili
tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali
turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri”
Kama unaweza kupata nafasi ya kuwa karibu na Biblia
yako tafadhali rejea sura ya 13 ya kitabu cha Hesabu ambayo kwa ujumla inaeleza
juu ya habari ya wapelelezi 12 ambao Musa aliwatuma kuipeleleza nchi ya
Kanaani.
Kati ya wapelelezi 12, ni wapelelezi 10 ambao walikuja na habari mbaya
kwa wana wa Israeli: taarifa ya watu 10 wa kwanza juu ya upelelezi ilijaa
vitisho, kushindwa na kila hali ya kukata tamaa. Ndipo sasa kwenye sura ya 14
mistari niliweka hapo juu utaona mrejesho (feedback) wa wateule wa Mungu juu ya
taarifa maliyopokea.
Kitu ninachotaka uone ni kwamba hawa ndugu si tu kwamba
walisikia taarifa bali walisikiliza taarifa (kuna tofauti kubwa kati ya kusikia
na kusikiliza). Taifa zima lilikuwa makini kusikiliza, waliyaelekeza macho
na masikio yao kwenye taarifa hii muhimu ya kiintelijensia. Kwahiyo
maandiko niliyokuwekea hapo juu ni ufupisho (summary) wa mawazo yao juu ya
ahadi ya Mungu kuingia Misri.
Wamekuwa ni watu wa kulaumu, kunung’unika,
kujiona ni mateka, kutamani kifo, kutaka kurudi Misri n.k kwasababu tu
wameelekeza macho na masikio yao kwenye taarifa zisizosahihi. Ni
Muhimu ukakumbuka sana hapa ya kwamba Israeli walikuwa ni taifa teule la Mungu
na walikuwa na ahadi zote za Mungu… Mbona hawakuziamini ahadi, mbona
hawakumwamini Mungu?... Macho na masikio yalielekzwa kwingine!
Warumi 10:14
“Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije
yeye wasiyemsikia? Tena wamsikiaje pasipo muhubiri?”
Ili mtu aweze Kuokoka lazima ifikie mahali asikie…
Ndiyo Paulo anafundisha hivyo kwenye kanisa la Rumi.
“Tena wamwiteje yeye
wasiyemsikia?” hili ni swali muhimu sana kulichambua. Nadhani unaelewa wazi
kwamba kusikia ni kazi ya masikio, amabayo ni moja ya milango ya fahamu. Kwa
maana hiyo basi, ili mtu amwite Yesu ni lazima apewe taarifa hizo au kwa maneno
mengine ni kwamba mtu huyo anapaswa kuyaelekeza masikio yake kusikia taarifa.
Ukiona mtu ameokoka tambua kuna kazi ya milango ya fahamu kuleta taarifa kwenye
nafsi ya mtu husika!
Kumbuka:
Haijalishi una miaka mingapi katika wokovu,
haijalishi umewekewa mikono na watumishi wangapi, haijalishi unanena kwa lugha
kwa viwango gani, haijalishi umetolewa unabii mara ngapi… kama milango yako ya
fahamu imeelekezwa kwenye vyanzo vibovu vya taarifa, basi dhoruba itakapokuja,
siku zako zinahesabika!!! Lakini habari njema ni kwamba: Umeanza kujifunza,
umeelekeza milango yako yako kwenye fundisho hili. Mungu akusaidie sana.
Baada ya kukuonyesha walau kwa ufupi sana kwamba
mwanzo wa mawazo yote ni milango ya ufahamu, ninaomba tuambatane sasa kuyaelewa
mawazo kwa mapana kiasi.
Mithali 23:7a
“Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo…”
Ili uweze kuulewa kwa upana wake huu mstari ni vyema
turejee Biblia za tafsiri kadhaa ili tuweze kunasa upana wa maana
iliyokusudiwa.
“For as he thinks in his heart, so is he.” (NKJV)
“For as he thinketh in his soul, so is he.” (DARBY)
“For as the thoughts of his heart are, so is he.”
(BBE)
“For as he hath thought in his soul, so [is] he.”
(YLT)
Ukisoma tafsiri hizo kwa ujumla wake zinazungumzia
“mawazo”… Kwahiyo Biblia inaposema “aonavyo” imekusudia hasa kumaanisha
“awazavyo”. Kwahiyo twaweza kuusema mstari huo namana hii: “Maana awazavyo mtu
nafsini mwake, ndivyo alivyo.”. Yaani kwa ukubwa wa maana yake ni kwamba MTU NI
MAWAZO!
Ni wazi kwamba huwezi kuwa kinyume, juu, zaidi ama tofauti na mfumo
wako wa mawazo. Kumbuka mawazo ni hali
ya ndani unayoishikilia kuhusu jambo fulani. Wakati fulani nilikuwa
ninazungumza na ndugu kadhaa na ili kutambua mawazo yao kuhusu maisha ya ndoa
niliwauliza, “Kwa uelewa wenu, Mwisho wa ndoa ni nini?”…
Jibu halikuwa gumu
sana kutoka kwa ndugu hawa, “Mwisho wa ndoa ni talaka ndugu James.” Nikatikisa
kichwa kwa maana ya kuwaelewa mawazo yao kisha nikawaambia, “Muasisi wa ndoa
amekusudia kuwa mwisho wa ndoa ni kifo... Unawezaje kuutenganisha mwili mmoja”…
Sasa ndugu msomaji unaona tofauti hapo?
Tafsiri yake ni kwamba mawazo ya hao
ndugu ndiyo yatakayoongoza maisha yao ya ndoa… Ipo siku watatumia wazo la
talaka, ipo siku watashauri kuhusu talaka, ipo siku wazo la talaka
litajifunua…. Ipo siku! Kwahiyo huo ndiyo uelekeo wa maisha yao. Ule ukiri na
kiapo “mpaka kifo kitakapotutenganisha…” kwao si halisi kabisa.
Mfano mwingine ni juu ya mwanzo wa maisha… Je, maisha
huanza lini? Kipindi mimba inapotungwa au kipindi mtoto anapozaliwa? Majibu juu
ya maswali hayo ndiyo yamezaa harakati za kuhalalisha utoaji mimba… wafanyao
hivyo husema maisha huanza mtoto anapozaliwa!
Sasa Hebu fikiri kama umeoa mke
mwenye mawazo hayo juu ya maisha ya mtoto… saa yoyote anaweza kufanya uamuzi wa
kutoa mimba na vado akalindwa na “wanaharakati” wa “haki” za binadamu! Sijui
unaelewa ninachomaanisha? Maana awazavyo mtu nafsini mwake, ndivyo alivyo!
Hakuna namna yoyote ambapo mtu anaweza kuwa tofauti na mawazo yake.
Wafilipi 4:8
“Hatimaye ndugu zangu, mambo
yoyote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo
yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza,
yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakirini
hayo.”
Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu