Bw. Alex Msama |
TAMASHA la Krismasi 2013 limepangwa kufanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 25.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, ilieleza awali mikoa
sita iliomba kuwa mwenyeji wa tamasha hilo, lakini kamati yake imeteua
Dar es Salaam iwe ya kwanza.
“Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Krismasi imeamua lifanyike Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam, halafu Desemba 26 tutatizama mkoa mwingine.
Tunaomba mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono,” alisema Msama.
Alisema awali walipokea maombi kutoka kwa wadau mbalimbali wa muziki
wa Injili nchini wakiomba lifanyike katika mikoa yao, ambayo ni Mbeya,
Mwanza, Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Shinyanga.
Tamasha la Krismasi linaandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya
jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka.
Kwa mujibu wa Msama, wanataka Tamasha la Krismasi liwe bora zaidi
kuliko la Pasaka kwa kualika wasanii maarufu kutoka nje na ndani ya
Tanzania.
Alisema hilo ni tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu na litakuwa
na tofauti kubwa kulinganisha na mengine yaliyowahi kuandaliwa na
kampuni yake.
- Tanzania Daima -