Vitu vilivyoharibiwa katika Kanisa la KKKT Mbagala baada ya Kuchomwa Moto |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewaachia huru,
Hamed Sekondo na wenzie wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya
unyang'anyi wa kutumia silaha, kisha kulichoma moto Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Usharika wa Mbagala, baada ya kuwaona hawana kesi ya
kujibu.
Uvamizi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, ambaye
alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo ya jinai namba 294/2012
ilikuwa imekuja kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi wa ama kuwaona
washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.
Akisoma uamuzi wake, Lema alisema upande wa Jamhuri katika
kuthibitisha kesi yao, ulileta mashahidi 14 na kwamba awali kesi hiyo
wakati inafunguliwa mahakamani hapo mwaka jana, ilikuwa na jumla ya
washtakiwa 10.
Alisema kuwa hivi karibuni mshtakawa mmoja, Ramadhan Mbulu, alifariki
dunia na hivyo kufanya kesi hiyo kubakiwa na washtakiwa tisa ambao kwa
kipindi chote walikuwa wakiishi gerezani kwa sababu kosa la unyang’anyi
wa kutumia silaha lililokuwa likiwakabili halina dhamana.
Namna vitu vilivyokuwa vimeharibika |
Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na wakili wa kujitegemea, Yahya Njama.
“Baada ya kusikiliza na kuchambua ushahidi na vielelezo vilivyotolewa
na upande wa Jamhuri, mahakama hii imefikia uamuzi wa kuwaona washtakiwa
wote hawana kesi ya kujibu, hivyo inawaachilia huru kwa sababu upande
wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yake,” alisema.
Lema aliongeza kuwa ushahidi wote walioutoa ni dhaifu na umeshindwa
kuishawishi mahakama iwaone washtakiwa wana kesi ya kujibu.
Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Mwandamizi, Tumain Kweka na Inspekta wa Polisi, Hamis Saidi.
Mwaka jana eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam lilikumbwa na vurugu
kubwa zilizodaiwa kufanywa na baadhi ya waumini wa Kiislamu, ambao
walikuwa wakipinga dini yao kudhalilishwa kwa kukojolewa kitabu cha
Kurani, hatua iliyosababisha kuchoma moto makanisa.
- Tanzania Daima -