Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi Mkoani Kilimanjaro Isack Amani |
ASKOFU Mkuu Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi mkoani Kilimanjaro, Isack
Amani amesema watanzania 175 wanaoshikiliwa nchini China, kwa tuhuma za
kufanya biashara ya dawa za kulevya, serikali haiwezi kuwaombea msamaha,
kutokana na kutokuwa na mamlaka na serikali ya China.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki, wakati akizungumza kwenye sherehe za
mahafali ya kwanza ya kidato cha nne ya shule ya Sekondari St. Amedeus,
inayomilikiwa na Kanisa Katoliki jimbo la Moshi, pamoja na kuzindua
jengo la maabara ya sayansi.
Alisema serikali hawezi kuwaombea msamaha wa kutonyongwa watanzania
wanaoshikiliwa kwenye magereza ya nchini China, kwani hawezi kuingilia
sheria za nchi nyingine.
Alisema hakuna wa kulaumiwa, endapo watanzania hao watanyongwa, kwani
wao ndio waliojitakia. Alieleza kuwa watuhumiwa hao wanatambua sheria
za nchi hiyo vizuri, kwamba endapo mtu akikamatwa na dawa za kulevya,
lazima anyongwe.
“Serikali haiwezi kuwaombea msamaha watanzania 175 wanaoshikiliwa
nchini China kwa dawa za kulevya, sheria za nchi hiyo walizijua hivyo
walijitakia wenyewe, pia serikali yetu haina mamlaka kwenye sheria za
China,” alisema Askofu Amani.
“Hakuna umuhimu wa serikali kuwaombea wasinyongwe, wamejitakia
wenyewe kifo kwani wanajua vyema kule kuna sheria kali, na sisi hatuna
mamlaka na huko hivyo serikali yetu haina cha kufanya,”alisema.
Alisema serikali wakati ikishererekea miaka 50 ya uhuru inapaswa
kutatua tatizo la ajira kwa kuweka mazingira mazuri kwa vijana ili
wasiweze kujiingiza kwenye matukio ambayo yanawagharimu uhai wao.
Akofu Amani alifafanua kwamba wakati serikali ikipigana na adui
maradhi, ujinga na umaskini, pia itambua upougonjwa wa dunia wa uaminifu
na kutojali amri za Mungu, maadili katika jamii, hali inayosababisha
taifa kuyumba kutokana na kukosekana kwa haki.
- Habari Leo -