James Kalekwa |
Mithali 29:18,
“Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.”
Bwana Yesu asifiwe! Ndugu msomaji, ni neema kubwa sana ya
Bwana Yesu kwamba tumepata kibali cha kuwa hai lakini zaidi kutumia uhuru wetu
wa habari na utashi wetu kukutana hapa kwaajili ya kuanza mfululizo mpya juu ya
“Usuri wa njozi kwenye maisha binafsi”.
Neno la utangulizi:
Je, unafanya mambo yaleyale kwa namna
ileile huku ukitaraji matokeo tofauti?
Hagai 1: 5-7
“BWANA wa majeshi
asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo;
mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo
lakinihapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara ili kuutia katika mfuko
uliotoboka-toboka. BWANA wa majeshi asema hivi zitafakarini njia zenu.”
Mungu anawasemesha kitu cha tofauti na kigumu sana taifa la
Israeli kupitia kinywa cha mtumishi wake Hagai. Wanaisha maisha yasiyo na tija
– pesa ya mshahara haikai wala kuwazalia matunda yoyote, chakula hakiwashibishi
tena na wala nguo haziwapi joto.
Wao wakijitazama wanaona hakuna tija lakini
wanaendelea na mzunguko uleule wa maisha wakitegemea kupokea mabadiliko.
Binafsi ninaamini kabisa, ni upumbavu kurudia mambo yaleyale huku ukitarajia
matokeo ya kiutofauti kwenye maisha – ni upumbavu wa ngazi ya juu sana!
Ni kama Mungu anawaambia hakuna “njozi” ndani ya nguo,
hakuna “njozi” ndani ya mshahara na hakuna “njozi” ndani ya chakula! Ninapata
wapi ujasiri wa kusema hayo? Ni kwenye habari ya tija na faida ya mfumo wa
maisha!
Soma maandiko hayo kwa jicho la kujifunza, utagundua ya kwamba ndugu
hawa wameamua kuwekeza muda na nafasi zao kutafuta tija ya maisha kwa njia
tatu:
Mshahara (pesa/mali)
Chakula na vinywaji
Mavazi
Lakini ukutazama kwa kina zaidi utagundua ya kwamba ndani ya
hayo mambo mitatu, hawa ndugu hawakupata ridhiko la nafsi wala maisha yao. Ni
kweli walikuwa wanapata mshahara, wanapata chakula na vinywaji na wanapata
mavazi…
Lakini kulikuwa hakuna utoshelevu katika hayo! Kitu cha ajabu na cha
kushangazwa ni kwamba, pamoja na hayo yote hawa ndugu waliendelea kufanya mambo
yale yale wakitegemea vitu vya tofauti mpaka pale Mungu alipowasemesha jambo na
kisha kuwaita kwenye maisha ya kiwango kikubwa “Zitafakarini njia zenu”.
Huu ni mwito wa moyo wangu na kilio cha moyo wangu kwa Mungu
kwa muda mrefu kwaajili ya taifa la Tanzania na vijana wa taifa hili kwenye
maisha yao binafsi na maisha ya kijumuiya. Unapoendelea kujifunza katika
mfululizo huu, zitafakari njia zako!
Hazina ya kukumbuka kutoka kwenye mfululizo uliopita:
“Lengo”
si kuwa na malengo bali kuwa na matokeo
Kabla hujachukua hatua ya kuanza sasa kuweka mafundisho haya
kwenye matendo, ninapenda nisisitize jambo moja kwako ambalo linaweza kuwa
mtego kwako.
Watu wengi baada ya kuwa wamejifunza huelekeza akili na mawazo yao
kwenye shughuli nzima ya kuweka malengo na kujisahau kabisa kuhusu usuri
(essence) ya mchakato wa uwekaji malengo.
Kwahiyo utakutana na watu ambao
wanazungumza na kujivunia kabisa malengo! Kwa mfano, mtu anaweza kusema
“nimeweza kuhubiri kwenye wilaya 4 za Tanzania.” Au utakuta mwingine
anajaivunia kabisa “oooh, mwaka huu nimeandika na kuchapisha kitabu kimoja.”
Ni
sawa, ni mambo mazuri lakini hayo yote si “malengo” ya malengo yako! Sidhani
kama unaoujasiri wa kuweka lengo ili ulifikie tu; sidhani kama ni furaha yako
kukamilisha ratiba na kukamilisha shughuli fulani iliyo ndani ya malengo –
sidhani!
Najua nyuma ya kila lengo kuna matokeo ambayo yamekusudiwa. Ndiyo
kusema lengo la kuweka malengo au usuri wa malengo ni kuzalisha matokeo
yaliyokusidiwa, kwa mantiki hiyo basi malengo ni nyenzo kukupeleka kwenye
matokeo hayo. Kama una lengo lakini halikufikishi kwenye matokeo yako…. Ni heri
kabisa ukachagua kufanya jambo jingine!
Ni heri kutokuwa na malengo kuliko kuwa na malengo
yasiyokufikisha kwenye mwisho wowote yatakapokuwa yamekamilishwa! Mungu akupe
hekima ya kunia kuwa na matokeo, kuzaa matunda, kuona mabadiliko na kisha
malengo yakusaidie kuelekea huko!
Somo hili litaendelea Jumatatu Ijayo
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764