Advertise Here

Monday, January 13, 2014

Safu ya James Kalekwa: Ongeza Maana/Thamani kwenye maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea. - Part 2

James Kalekwa
Kisa mkasa (Scenario) #2
Mchezo wa mpira wa miguu bila magoli

Kama wewe ni mpenzi, mshabiki au mfuatiliaji wa mchezo wa mpira wa miguu basi uanelewa fika juu ya muundo wa viwanja vya mchezo huo… Moja ya vitu muhimu sana kwenye ujenzi wa kiwanja ni milingoti minne mikubwa isimamayo pande mbili tofauti (zinazokabiliana) za uwanja. Bila shaka umekwisha baini ya kwamba ninazungumza kuhusu magoli.


Hebu fikiri, mchezo wa mpira wa miguu pasipo magoli uwanjani… Je, inawezekana kuwa na mchezo huo? Hata ule mpira wa “mchangani” huwa na magoli, hata kama ni ya mawe au vijiti…

Hauwezi kuwa mpira wa miguu bila magoli. Hebu jiulize wachezaji wangekuwa wanakimbiakimbia uwanjani, wanapiga chenga, wanapeana pasi, wanakaba/wanazuia mashambulizi… ili iweje sasa???

Kuna umuhimu gani wa kuwa na mchezo wa mpira wa miguu pasipo magoli? Lengo kuu la mpira wa miguu ni magoli. Ukiyatoa malengo hayo, umeondoa maana, umeondoa thamani iambatanayo na mchezo huo.


Kabla hatujachukua hatua kubwa sana katika kujifunza haya, ninaomba tujenge uelewa wa pamoja juu ya maswala kadhaa ambayo yana uhusiano wa moja kwa moja na maswala mazima ya malengo.


Kusudi – ni sababu kuu ya kuwepo kwako. Hii hujibu swali la “Kwanini ninaishi?” mfano: Ninaishi ili kuudhihirisha utukufu wa Mungu kwenye kizazi changu.


Maono – ni taswira/picha kubwa uionayo juu ya mwisho wa maisha yako. Ni mkusanyiko wa mwisho wa maisha yako. Hii hujibu swali la “ninakwenda wapi?” mfano: … Kumtukuza Mungu kwa kufanya ugunduzi, uvumbuzi na utatuzi chanya wa mahitaji ya kizazi changu.



Dhamira – ni namna gani utafanya ili kuyafikia maono hayo kivitendo. Hii hujibu swali la “Namna gani nitatekeleza?” Mfano: … Kufungua taasisi ya utafiti wa uwezo wa mwanadamu na uelimishaji wa vijana.

N.B Unaweza kuwa na dhamira zaidi ya moja… Hakuna ukomo ilimradi tu dhamira zinafanikisha ufikiaji wa maono yako.



Malengo/Mipango – ni kuweka namna/njia za kivitendo na zinazopimika ili kufanikisha dhamira yako/zako Mfano: … Kufanya usajili wa taasisi yangu ifikapo March 28 ili kuanza utendaji rasmi.



Mkakati – ni mchanganuo wa hatua kwa hatua na uratibu wa rasilimali ili kufanikisha malengo yako. Hii hujibu maswali mengi “Nifanye nini, nifanye wapi, wakati gani?...” Mfano:


Mkakati wa usajili wa taasisi:

#
Jukumu
Yatakayohitajika
Kinachotarajiwa
Muhusika
Lini
Hali ya utendaji

Kuandika katiba ya taasisi.

Katiba ya taasisi
Frida
1-23 January, 2014
Inaendelea

Kualika wajumbe waanzilishi na kuwashirikisha wazo

Kikao/mkutano wa kwanza
James
28 January, 2014
Bado

Kufanya shughuli za usajili wa taasisi

Cheti cha usajili
Charisa & Joshua
19 February, 2014
















Kutoka kwenye mkakati huu unaweza kutengeneza bajeti (maelezo juu ya uratibu wa rasilimali fedha).


Lengo la kuainisha, walau kwa ufupi tu, tofauti ya mambo hayo ni ili uwe na uhakika na kitu gani unakiendea na unapaswa kufanya. Ni muhimu sana ufahamu ya kwamba kusudi ndilo huwa sababu ya maono; maono huzaa dhamira (utume) na dhamira ndiyo huleta malengo ambayo huzaa mikakati tayari kwa utekelezaji. Ili kurahisisha uelewa juu ya mambo haya, tazama na kujifunza kwenye Taswira ifuatayo:


Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764

Thursday, January 9, 2014

Mwimbaji wa Nyimbo za Injili Nchini Nigeria anusurika kifo.

I don’t care, whether you like me or my music -Busola Oke
Queen Eleyele

Mwimbaji maarufu wa Nyimbo za Injili toka Nchini Nigeria Busola Oke maarufu kama Queen Eleyele anusurika kufa kwenye ajali mbaya ya gari iliyotokea January 4, Mwaka huu akitokea Oyo Estate kuelekea Lagos.

Baada ya Ajali hiyo kutokea, watu waliokuwa eneo la tukio waliwahi haraka eneo la tukio na kumchukua Mwimbaji huyo kisha kumpeleka hospitalini.

Hata hivyo gari iliyokuwa ikiendeshwa na Mwimbaji huyo iliharibika vibaya.
http://4.bp.blogspot.com/-oGgP2XlVC4I/Us12M0h_mzI/AAAAAAAABxs/N1YkkEyXpK8/s1600/bubu.jpg
Hii ni Video ya wimbo wa Queen Eleyele ujulikanao kama Afefe Ife

Wednesday, January 8, 2014

Kanisa la Moravian Mkoani Mbeya latoa Msaada kwa watoto yatima.

Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Chunya Mjini, limetumia zaidi ya Sh6 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya shule kwa watoto 100 yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
 
Akikabidhi msaada huo jana mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, Mchungaji wa Kanisa hilo Anyandwile Kajage alisema kuwa fedha hizo zilitumika kwa ajili ya ununuzi wa sare za shule, madaftari, viatu na chakula.

Kajage alisema kuwa lengo la kutoa msaada huo ni sehemu ya hamasa kwa watoto walio katika makundi hayo ili kuwajengea mazingira mazuri ya kuishi kwa amani na faraja.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro alipongeza jitihada za wadau na waumini katika kutoa misaada na kuitaka jamii kujitolea kwani kutoa ni moyo na siyo utajiri.

Alisema amefarijika kwa kiasi kikubwa kwa mwamko wa madhehebu ya dini kwa kutambua uhitaji wao kwa kukabiliana na janga la ongezeko la watoto wa mitaani na kuzitaka asasi nyingine za kiraia kuiga mfano huo.

Naye Mtoto Salome Zumbe alilishukuru kanisa hilo kwa kutoa msaada huo na kwamba utakuwa ni chachu na kichocheo cha wao kufanya vizuri katika mitihani yao na kuzingatia masomo ili kuweza kuendelea katika elimu ya ngazi za juu.

- Mwananchi -

Tuesday, January 7, 2014

Safu ya James Kalekwa: Ongeza Maana/Thamani kwenye maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea. - Part 1

James Kalekwa
Mithali 29:18, “Pasipo maono, watu huacha kujizuia…” 
Habakuki 2-3, “BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili kila aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingoje; Kwakuwa haina budi kuja, haitakawia.”

Salamu za mwanzo wa Mwaka
 Ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mafundisho yetu kwa njia ya mitandao, pokea salamu za heri ya mwaka mpya kwa jina la Yesu Kristo kutoka kwangu na mke wangu kipenzi, Frida. Tumekuwa na shauku sana kukushirikisha mafundisho haya na tumeomba sana kwaajili yako. Kiu iliyojaza mioyo yetu ni kuona unatembea na kuliishi kusudi la Mungu kwenye maisha yako binafsi, familia, jamii na kisha uweze kuepika (influence) taifa letu kwa ujumla.

Pia, tunaomba upatapo muda tafadhali omba kwaajili yetu tunapotekeleza wito tulioitiwa wa kuwakamilisha watakatifu kwa njia ya mafundisho. Mwaka huu tunataraji kuona wigo ukifunguka zaidi na mikoa na wilaya nyingi hapa kwetu
tutawafikia kwa mafundisho ya neno la Mungu. Kumbuka kuomba kiwemo chakula cha kutosha ghalani!

Sasa, nikukaribishe uungane nasi kwenye mfululizo huu mpya juu ya kuongeza thamani ya maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea.

Lengo kuu la somo:
Kumuwezesha mtu binafsi kuwa na ufanisi na mwelekeo katika maisha ya siku kwa siku.

Malengo mahususi ya somo:
        i.            Kuelekeza kwa upana juu ya usuri (essence) wa maisha yenye malengo.
     ii.            Kujifunza kutoka kwenye maisha ya waliotutangulia juu ya malengo na kumahalisha (contextualize) mafunzo hayo.
   iii.            Kujenga stadi na mbinu za kuweka, kutekeleza na kutathmini malengo kwa mtu binafsi na vikundi.
   iv.            Kumuandaa mtu binafsi kwaajili ya kuwa chachu ya mabadiliko kwenye taifa.

Ni Muhimu sana ukatunza kumbukumbu ya malengo hayo ili uyapime na ujipime kulingana nayo wakati wote wa mfululizo huu.
Ndugu, imekuwa ni desturi miongoni mwa watu wengi sasa kila ifikapo mwanzo na/au mwisho wa mwaka au msimu fulani kuwasikia wakisema, wakielekeza na wakikumbushana juu ya kuwa na malengo kwenye maisha. Mijadala ya namna hiyo si maarufu sana katikati ya mwaka na wengi hawajisumbui kuyaelekea wala kutathmini hayo malengo – hilo ni tatizo kubwa. Nasi kwa neema ya Mungu, tumeiona ni vyema tuanze mwaka huu kwa kukukumbusha na kukuelekeza juu ya hilo, si kama desturi, kwa kuwa ni shauku yetu kuona unakuwa na kustawi… Karibu ujifunze, si kama desturi.

Hebu jiulize pamoja na mimi juu ya mambo haya:
Kisa mkasa (Scenario) #1. Msafiri asiyejua aendako:

Nimewahi kuzungumza mahali pengi na kwenye kitabu changu cha “Wokovu ni uhakika wa maisha ya Sasa na ya Baadaye.”  Juu ya mfano huu… Hebu jaribu kufikiri ukiwa katika stendi kubwa ya mabasi yaendayo katika mikoa mbalimbali (mfano stendi ya Ubungo- Dar Es Salaam, Nyegezi/Buzuruga- Mwanza, Msamvu- Morogoro n.k) Anatokea mtu mmoja ambaye kwa mwonekano wake ni msafiri… amebeba mabegi na mizigo kadhaa, mkononi ameshikilia chupa ya maji ya kunywa… akakujia kisha akakuuliza, “Ndugu, naomba unionyeshe basi kwani ninataka kusafiri.”

Je, utamuonyesha basi gani? Au utamuonyesha basi la kwenda wapi?...
Kwa kadiri nijuavyo mimi ni kwamba mtu mwenye akili timamu na nia njema, kama wewe ndugu msomaji wangu, utahitaji kupata maelezo kamilifu… utataka kujua kule anakoelekea yaani mwisho wa safari yake ili umwonyeshe basi linaloelekea mwisho huo.

Sasa iwapo ukimuuliza swali hilo kisha akakujibu kwamba “ndugu, sijui kule ninakokwenda.”  Je, utamuonyesha basi liendalo wapi? Au utamwonyesha basi gani? Huwa ninaamini na kushawishika kabisa ya kwamba wewe hutakuwa na kosa utakapomwonyesha basi lolote ili aende kokote kwasababu hajui kule aendako! Kwahiyo kokote atakapopelekwa ni sawa.

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764