James Kalekwa |
Kwahiyo, somo hili litaanza kwenye mzunguko wa malengo na ni
wajibu wako kujua kusudi lako, maono na dhamira yako.
Ninaanza kwa kuamini
kwamba (based on the assumption that), wewe, ndugu msomaji wangu,
umekwishawekeza muda wako kulitafuta kusudi la Mungu juu ya maisha yako,
unayajua maono yako na umeyafikisha kwenye hatua ya dhamira (utume).
Malengo ni nini?
Binafsi nimekuwa na changamoto kubwa sana kutafuta maana
rahisi na ya kueleweka juu ya neno “malengo.” Huwa ninawaambia watu wengi ya
kwamba inawezekana kwamba usiwe na maana (definition) ya malengo, lakini
ukiyaona ni lazima utayafahamu.
Lakini, huwa ninaamini ya kwamba huwezi kuanza
kutenda/kushughulika na kitu, jambo au hali usiyoijua. Na kwa misingi hiyo
basi, ninawiwa kujenga ufahamu ndani yako juu ya malengo. Katika mzunguko
niliouonyesha hapa awali kwenye taswira, malengo huzaliwa kutoka kwenye dhamira
(utume).
Lazima dhamira ikusukume kuumba malengo! Sasa, malengo ni nini basi? Malengo
ni ajenda au mahitaji husika/mahususi ambayo
mtu fulani hujiwekea kwa kipindi cha muda fulani ili kumzalishia matokeo
yanayoonekana, matunda na/au mabadiliko yaliyokusudiwa… hupimika, huweza
kufanyiwa tathmini!
Weka malengo kwa vigezo hivi:
Malengo mazuri huwa na sifa ya “SMART”, neno la
kiingereza linalomaanisha nadhifu, -enye uelewa mzuri. Kwahiyo malengo yako
yanapaswa kuwa nadhifu, sasa neno smart linabeba maana kubwa sana kwa kila
herufi yake:
S -(Specific), kwanza lazima lengo liwe ni maalum
au hususani juu ya jambo, mtu au hali fulani. Kwa mfano mtu anaposema,
“Mimi ninataka kupambana na umaskini.”. Ni sawa hilo ni lengo lakini si
hususani, yaani halina mwelekeo… Je, mtu huyo anataka kupambana na umaskini wa
aina gani (umaskini wa kifikra, kifedha…), Je, anapambana nao katika ngazi ipi?
(mtu binafsi, kijiji, familia, nchi…) lazima uainishe.
Na ndivyo ilivyo katika
huduma, unaweza kusema nina wito wa kuhubiri injili, ni sawa lakini ni katika
ngazi gani? Ni wazi kwamba kuizungukia dunia yote ni jambo ambalo si rahisi
(nchi zote, mikoa yote, majimbo yote, wilaya zote, vijiji vyote na kaya zote za
dunia.) Si jambo rahisi, ukijaribu utaumia tu na matunda hayatakaa.
Mfano: Lengo langu ni kuihubiri injili nchini
Tanzania.
Kumbuka kuwa Tanzania ni nchi kubwa, ina mikoa zaidi
ya ishirini na wilaya zake na tarafa, kata, mitaa/vijiji na kaya (familia)
kwahiyo unatakiwa kuwa specific zaidi. Kwahiyo waweza kusema, kuhubiri
injili nchini Tanzania katika ngazi ya wilaya.
M -(Measurable), Pili lengo lolote linatakiwa kupimika,
Je unaweza kuuona ufanisi, matokeo au matunda ya lengo hilo? Kwa mfano
lengo la kuihubiri injili nchini Tanzania katika ngazi ya wilaya…Baada ya muda
je unaweza kupima matokeo ya lengo hilo.
Sasa kuna njia mbalimbali za kuyapima
malengo yetu, baadhi ya njia ni kuangalia mabadiliko katika maisha ya watu, je,
kuna mabadiliko yoyote,njia nyingine ni kuangalia je, idadi iliyokusudiwa
imefikiwa? Tukiendelea kuutumia mfano wetu wa kuihubiri injili nchini Tanzania
katika ngazi ya wilaya ili tuufanye kuwa SMART; Ili kuweza kupima lengo hilo
waweza kusema:
Kuihubiri injili kwa watu 1000 nchini Tanzania katika
wilaya 4 (unapaswa kuzitaja wilaya ulizokusudia kuzifikia) kuanzia Januari
mpaka Juni.
Je, unaweza kuyapima matokeo ya lengo hilo? Kwasababu
unaijua idadi ya watu unaotaka kuwafikia ni watu 1000 na tayari unajua wapi pa
kuwapata (wilaya 4, Tanzania) kwa maana hiyo basi ni watu 250 kwa kila wilaya.
Kwahiyo hatimaye unaweza kuangalia Je, hizo wilaya 4 zilifikiwa na injili na
Je, watu 1000 walifikiwa pia? Hivyo ndiyo kupima malengo!
A (Attainable), Jambo jingine la tatu na la msingi
kufahamu ni kwamba lengo lolote linapaswa kufikika. Hapa unapaswa
kuangalia kwamba Je ,ninao uwezo wa kukamilisha lengo hilo kwa kiwango hicho, Je,ninao
watu wa kushirikiana nao kufika huko,Je ninahitaji maandalizi ya kimaombi, kifedha,
kifursa n.k kiasi gani?
Kuna malengo mengine ukiyatazama unatambua tu kwamba
mtu huyu anaota ndoto za mchana, kwa kutumia mfano wetu wa injili nchini
Tanzania, unakuta mtu anasema: Lengo langu ni kuihubiri injili nchi yote ya
Tanzania kwa mwaka. Hilo ni lengo zuri na lina nia njema lakini Je, unaweza
kuifikia nchi yote ya Tazania kwa mwaka? maana yake mikoa zaidi ya 20, yaani
wastani wa wilaya 5 kila mkoa, sawasawa na wilaya 100. Mwaka una siku 365,
ambapo ni sawasawa na wastani wa siku 3 kila wilaya.
Unaweza? Vipi kuhusu muda wa kujiandaa? gharama? familia? mapumziko?
Usafiri,si unajua wakati mwingine inachukua siku nzima kusafiri toka mkoa mmoja
kwenda mwingine? Mikutano hiyo au huduma hiyo utaiandaaje? Je, lengo hilo
linafikia?, basi hata kama likifikika halitakuwa na ufanisi.
Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764