MAKADINALI wote isipokuwa mmoja
waliokuwa wakisimamia benki ya Vatican wamefutwa kazi na Papa Francis.
Waliokumbwa na ‘fagio hilo la chuma’ ni makadinali wanne ambao ni pamoja
na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Kadinali Tarcisio Bertone SDB,
Kadinali Odilo Scherer kutoka Brazil, Telesphore Toppo kutoka India na
Domenico Calcagno kutoka Vatican.
Kadinali Jean-Louis Tauran ambaye ni
Mkuu wa Baraza la Upapa linalohusika na Mijadala ya Kidini, amenusurika
kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la Kikatoliki la The Tablet.
Gazeti hilo lilieleza jana kuwa
isipokuwa Calcagno, makadinali hao wote ndio kwanza walikuwa wametimiza
miezi 11 tangu wateuliwe katika kipindi cha pili cha miaka mitano,
wakiwa wameteuliwa na Papa Benedict XVI muda mfupi kabla ya kujiuzulu.
Benki hiyo ya Vatican ilikumbwa na
kashfa ya utakatishaji fedha mwaka 2010 baada ya waendesha mashitaka wa
Italia kugundua shughuli zenye shaka zihusuzo fedha chafu ndani ya
benki.
Mwenyekiti wa Benki hiyo, Ettore Gotti
Tedeschi na naibu wake, Paolo Cipriani walichunguzwa baada ya polisi
kukamata euro milioni 23 kutoka kwenye akaunti ya benki hiyo.
Ilidaiwa kuwa ingawa benki hiyo ilikuwa
inadai kupambana na utakatishaji fedha, ilivunja sheria kwa kujaribu
kuhamisha fedha hizo bila kutambulisha mtumaji wala mpokeaji, au
zilikuwa zinatumika kwa shughuli gani.
Tuhuma hizo zilikanushwa kwa nguvu zote
na Vatican. Papa Francis ameteua makadinali wengine kuziba nafasi za
aliowatimua na kuunda alichokiita Tume ya Makadinali ya Kusimamia
Taasisi kwa ajili ya Kazi ya Dini (IOR), ambao ni makadinali Christoph
Schönborn (Vienna), Thomas Collins (Toronto); Santos Abril y Castillo´
(St Mary Major) na Kadinali Pietro Parolin (Waziri wa Mambo ya Nje).
- Habari Leo -