Advertise Here

Monday, March 25, 2013

Usikose Kusikiliza kipindi cha "Alive Xpress Show Time".

Usikose kusikiliza kipindi cha Alive Xpress Show Time kupitia Radio ya Kikristo ya Hhc Alive Fm(91.9Mhz) kwa Wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa, Kila Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia Saa 8 kamili Mchana hadi Saa 10 Kamili Jioni.

Sikiliza Hhc Alive Fm Online Kupitia;
www.hhcalivefm.org

Saturday, March 23, 2013

Historia ya Mwimbaji Sipho Makhabane.

Sipho Makhabane
Sipho Makhabane, Mwimbaji mwenye jina kubwa barani Afrika, ambapo umaarufu wake umepatikana kutokana na uwezo wake wa kutunga nyimbo zenye ujumbe wa hali ya juu wa kumsifu na kumuabudu Mungu.

Kutokana na uwezo wake huo mashabiki wengi wa muziki wa Injili wamekuwa wakimfananisha na wanamuziki mahiri kama Joyous Celebration ama Sfiso Ncwane.
  Makhabane mwenye umri wa miaka 45 ni mmoja wa magwiji wa uimbaji nchini Afrika Kusini, na ameshiriki katika shughuli mbalimbali za kiroho na kijamii. 

Kutokana na kutingwa na shughuli zake mwaka 2010 alitangaza kuachana na kazi ya kuimba, hata hivyo mwaka 2012 aliushangaza ulimwengu kwa kuachia albamu yake mpya iliyokubalika na watu wengi.

Historia ya maisha yake inaonesha kuwa ni mtu aliyekulia katika muziki huo, na kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa ukiikabili familia yake, Makhabane alilazimika kuacha shule akiwa darasa la tano na akiamua kufanya kazi katika shamba la miwa la Kaaruls huko Mpumalanga kama ilivyokuwa kwa mwimbaji mwingine nguli Rebecca Malope.
  Makhabane alifanya hivyo walau aweze kupata fedha ya kuwasaidia wazazi wake pamoja na ndugu zake ambao walikuwa wakimtegemea yeye.

 Alipotimiza  miaka 17, alihamia kwenye kazi za ujenzi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Afrika Kusini ya Kruger.

Akiwa huko alifanya kazi ya kuwasaidia mafundi waliokuwa wakijenga nyumba kambini hapo na alipotimiza miaka 21 alikuwa tayari na ujuzi wa kutosha katika kazi ya ujenzi na akapata kazi katika eneo la Pienaar.

Mwaka 1986, Makhabane alipata ofa nzuri katika kampuni ya Telkom kama fundi, lakini katika kuhangaika kwake alijikuta akiishia kwenye muziki wa Injili.

Hata hivyo hakuwa akijua kuwa nyota ya mafanikio yake ilikuwa kwenye huduma hiyo ya uimbaji na badala yake alikuwa akifanya muziki wa kujifurahisha zaidi na si wa biashara.

Mwaka 1990, wakati huo akiwa na umri wa miaka 25, Makhabane alifunga ndoa na binti aliyekuwa na umri wa miaka 18.

Baada ya hapo ndipo alianza kazi ya kununua na kuuza kazi za muziki ndani na nje ya nchi ya Afrika Kusini.

Kutokana na kuona muziki umeanza kuingia kwa kasi kwenye akili yake, Makhabane aliamua kuachana na kazi ya ufundi mitambo ya simu na kujikita kwenye muziki.

Katika kuhakikisha anapunguza wizi wa kazi zake, mwanamuziki huyo aliamua kusambaza kazi zake mwenyewe, lakini kikwazo kwake kikawa ni namna ya kuwavutia wasambazaji waliokuwa tayari kununua kazi kutoka kwake.

Kazi yake iliyomfanya kukubalika ilianza kusikika kwenye redio ya Swazi ambayo inajulikana zaidi kwa jina la Ligwalagwala FM, ambapo kibao kilichomtambulisha ni kile cha Ngitinikela Kuwe.
Hatimaye mwaka 1996, Makhabane aliamua rasmi kuifanya kazi hiyo ya muziki wa Injili na kuacha kazi aliyokuwa akiifanya kwenye kampuni ya simu.

 Mwaka huo huo aliachia album yake iitwayo “Yek’intokozo” wimbo ambao mpaka leo unakumbukwa na mashabiki wake kwani ndio ulimtambulisha vema, ingawa tayari alishatoa album nyingine mbili miaka ya 1993 hadi 1999 za ‘Thum'umlolo” na “Jesu Uliqhawe”. 

Mwaka 1998, kupitia kampuni ya CCP Records aliachia album yake ya nne iitwayo “Uyigugu” iliyofanya vema kabla ya mwaka uliofuata kuachia nyingine iitwayo “Makadunyiswe,”. 

Mwaka 2001, alifyatua album ya Calvary ambayo iliuza kufikia kiwango cha juu na mwaka uliofuata (2002), aliachia albamu  nyingine ya ‘Akukhalwa’ ambayo ilitikisa kama album ya “Yek’intokozo,” akiuza zaidi ya nakala 70,000.

Mwaka 2003, Makhabane aliachia album ya ‘Moya wami’ ambayo pia iliuza zaidi ya nakala 70,000. 

Kutokana na umahiri wake, Makhabane ameweza kushirikishwa katika album na waimbaji wakongwe wa nchini kwake kama Jabu Hlongwane, Marehemu Vuyo Mokoena, Lundi, Hlengiwe Mhlaba na wengine wengi. 

Pia akiwa nyuma ya mafanikio ya waimbaji lukuki kama Hlengiwe Mhlaba, Ncandweni Christ Ambassadors, Shongwe na Khuphuka Saved Group. 

Nje ya uimbaji, Makhabane ni mtayarishaji wa kazi za muziki wa injili akiwa daraja la waimbaji wengine kutokana na kuwika vilivyo kupitia kazi zao zilizoandaliwa na gwiji huyo.
 
Sipho Makhabane ni mmoja kati ya Waimbaji watakaohudumu siku ya Tamasha la Pasaka la Mwaka huu litakalofanyika Uwanja wa Taifa.

Tuesday, March 19, 2013

Mtawa wa Kanisa Katoliki apigwa Risasi na Kuporwa Mil. 20.

Mtawa Shobana Synd akiwa amelazwa baada ya kujeruhiwa kwa Risasi
WATU wanaoaminika kuwa ni majambazi, wamemjeruhi kwa kumpiga risasi Mtawa wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Shobana Synd na kumpora kiasi kikubwa cha fedha.

Habari kutoka kwa wenzake zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas zinasema kuwa mtawa huyo raia wa India kutoka Shirika la Notre Dame, alishambuliwa kabla ya kuporwa fedha hizo.

Kwa mujibu habari hizo, mtawa huyo aliyekuwa akitoka benki, alijeruhiwa kwa risasi mbili wakati akisubiri kufunguliwa geti la kuingia katika Shule ya Msingi Notre Dame.

Ingawa Watawa hao hawakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha zilizoporwa, habari zinasema ni zaidi ya Sh20 milioni zilizochukuliwa benki kwa ajili ya malipo na shughuli mbalimbali za shule hiyo.

Shule ya Msingi ya Notre Dame iliyoko eneo la Njiro, jijini Arusha inamilikiwa na shirika hilo la Watawa ambao wengi wao wana asili ya Asia ambako mtawa huyo, Shobana ndiye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo. “Alipigwa risasi mbili, moja kwenye mguu wa kushoto uliovunja mfupa na nyingine ilipenya kwenye nyama za mkono wa kushoto ambako kwa bahati haijagusa mfupa...Tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema mmoja wa watawa kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Akizungumza katika wodi ya Hospitali ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), alikolazwa, mtawa huyo alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa kuninusuru katika kifo...Walinirushia risasi kadhaa wavamizi hao.

“Ninamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, si ujanja wala uwezo wangu kuendelea kuwa hai hadi leo baada ya mashambulizi yale ya risasi. Ninawaombea msamaha na rehema wahusika ili waache uovu na kurejea katika njia ya haki.”

Kamanda Sabas mbali na kukiri kutokea kwa tukio hilo alishindwa kulizungumzia kwa undani kwa maelezo kuwa muda huo alikuwa akiendesha gari na kuahidi kulitolea ufafanuzi leo.

Kumekuwa na matukio kadhaa ya wateja wanaochukua fedha kutoka benki mjini Arusha kuvamiwa na kuporwa fedha, matukio ambayo yanazua hisia ya kuwapo mtandao wa uhalifu unaoshirikisha baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Mwaka jana, wafanyakazi wawili wa Shirika la Here’s Life Africa Mission linalomilikiwa na Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Stanley Hotay waliochukua fedha katika moja ya benki hizo walivamiwa na kuporwa zaidi ya Sh10 milioni.

Tayari uongozi wa benki zilipochukuliwa fedha hizo umeanza uchunguzi kuhusu jambo hilo kwa nia ya kubaini kwa nini taarifa za wateja wanaochukua fedha zinafika kwa majambazi ambao huwapora njiani au baada ya kufika ofisini kwao.

 - Mwananchi -

Monday, March 18, 2013

Pinda akusanya Milioni 31 Harambee ya Kanisa Dar.

Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameongoza harambee ya papo kwa papo na kufanikiwa kukusanya sh milioni 31.5 zikiwa ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda la Magomeni, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo jana kabla ya kuendesha harambee hiyo, Waziri Mkuu aliusifu uongozi wa kanisa kwa kuamua kufanya upanuzi wa kanisa hilo, ili liweze kuhudumia waumini wengi zaidi.

“Nia yao ni nzuri sana na wameona mbali mapema. Magomeni hii ya leo si ya wakati ule, na wala haitakuwa hivi katika miaka mingine 50 ijayo. Zamani usingeweza kuona hata ghorofa moja hapa Magomeni, lakini sasa hivi maghorofa hayahesabiki,” alisema.

Aliwasisitiza waumini hao kujitoa kwa ajili ya kazi ya Bwana kwa sababu hakuna sadaka ambayo ni ndogo.

“Hakuna sadaka iliyo ndogo mbele ya Mungu, kikubwa ni dhamira tu. Kanisa ni letu na litajengwa na sisi waumini ili mradi kila mmoja wetu aseme kanisa hili nitalijenga,” alisisitiza.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini hao, Baba Paroko wa kanisa hilo, Padri Sixfrious Rwechungura, alisema wameanza kazi ya ukarabati tangu Agosti 15 mwaka 2011 na kwamba hadi sasa wamekwishakusanya sh milioni 350 kutokana na nguvu za waumini wenyewe.

Alisema wanahitaji sh milioni 300 ili kukamilisha kazi hiyo ambayo inapaswa kukamilika katika miaka miwili ijayo ili iendane na maadhimisho ya miaka 50 ya kanisa hilo.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mkewe Tunu Pinda waliahidi kuchangia sh milioni 10 na wakatoa sh milioni mbili za kianzio.

- Tanzania Daima -

Sunday, March 17, 2013

Maganga James Gwensaga: Kutoka kuwa Mpiga Debe mpaka kuwa Meneja wa vituo viwili vya Radio za Kikristo.

Maganga James Gwensaga
Jina lake kamili ni Maganga James Gwensaga Almaarufu kama President. Ni mtoto wa pekee kwa Baba yake Mzee Julius Mashenene Gwensaga na Mama yake, ingawa kwa upande wa Baba ana dada zake wanne na kwa upande wa Mama ana wadogo zake wanne pia.

Alizaliwa mkoani Morogoro kijiji cha Kichangani, wakati Mama yake akiwa ni mluguru wa Mikese, na Baba yake akiwa ni Msumbwa wa Geita.

Baada ya kuzaliwa Mkoani Morogoro, Baba yake mzazi Mzee Julius Mashenene Gwensaga ambaye ni marehemu kwa sasa, alipata uhamisho wa kikazi kutoka Morogoro kwenda Mkoani Iringa.
Maganga akiwa katika Shughuli za uchoraji enzi hizo
Toka walipofika Iringa baba yake alikaa kwa muda wa miaka mine tu na kufariki na kumuacha Maganga akiwa mikononi mwa mama yake wa kufikia ambaye alimlea toka wakati huo, baada ya mama yake mzazi kukataa kuondoka na baba yake Maganga kutoka Morogoro kwenda Iringa.

Baada ya baba yake kufariki ambaye alikuwa ni mwajiliwa wa Wizara ya ujenzi kitengo cha Ufundi katika Kiwanda cha Karatasi cha Mgororo kilichopo Mkoani Iringa, ililazimika kurudi Dar es salaam kwani uongozi wa kiwanda cha karatasi cha mgororo hakikuwa na mkataba na wao isipokuwa baba yake ambaye alishafariki.

Kutoka Iringa walienda Dar es salaam, na mwaka 1989 Maganga akaanza darasa la kwanza katika shule ya msingi Mianzini iliyopo Mburahati Mianzini.

Akiwa hapo shule ya msingi, Maganga alishiriki michezo mbalimbali na jambo analokumbuka akiwa darasa la nne alichaguliwa kujiunga na bendi ya shule jambo ambalo halikuwezekana kwa mwanafunzi yeyote wa darasa la nne kwani ilikuwa ni mpaka ufike darasa la sita ndipo ujiunge na Bendi ya Shule.

Alipomaliza darasa la Saba Maganga hakuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya serikali na hivyo kulazimika kusoma kwenye shule za kulipia(Private School), ambapo alijiunga na elimu ya sekondari kwa masomo ya jioni.
Enzi hizo Maganga akiwa anafuga rasta
Alimaliza elimu ya sekondari mwaka 1999 na kuanza kufuga nywele rasmi kama Rasta. Mwaka 2000 aliingia katika masuala ya uandishi wa habari na uchoraji wa katuni wakati huo akichorea gazeti la maisha na sanifu ya jijini Dar es salaam.

Mbali na uchoraji wa katuni katika Magazeti, lakini pia alikuwa ni mwandishi wa hadithi mbalimbali za maandishi katika gazeti la Majira.

Maganga anasema, “Namshukuru sana dada yangu Juliana Gwensaga aliyekuwa akinitia moyo katika fani hii ya uandishi wa habari.”

Mwaka 2005 Maganga alikata Rasta zake zote na kubaki na nywela za kawaida tu baada ya kufuga Rasta hizo kwa miaka 6. Ilipofika Mwaka 2007 Maganga alikutana na mwanadada Peresia Shilla na kukubaliana kuishi pamoja kama Mke na Mume, na kweli mwaka huo huo walifunga ndoa na kwa sasa wana watoto wawili wote wa kiume ambao ni Brian(mkubwa) na Brighton(mdogo).
Maganga akiwa na Mkewe Peresia Shila siku ya Harusi yao
Kwa mara ya kwanza alikutana na Askofu Magike wa Jijini Mwanza mwaka 2005 jijijni Dar es salaa, wakati huo Maganga akiwa ni msanii wa uchoraji na alikuwa na kibanda chake cha uchoraji maeneo ya mbezi mwisho jijini Dar es salaam.

Wakati akifanya shughuli hiyo ya uchoraji, pia Maganga alikuwa akihubiri Injili katika kituo cha mabasi cha mbezi baada ya kuokoka, huku akiwa ni mwajiriwa katika shule ya msingi St. Ann’s kama mwalimu wa somo la uchoraji.

Baada ya kukutana na Askofu Magike katika moja wapo ya mikutano ya Injili hapo Dar es salaam, Askofu Magike alimuomba Maganga ampigie picha za video katika mkutano wake wa Injili wa Jijini Dar na baada ya mkutano huo, alimuomba tena ampigie picha za video kwenye harambee ya kuchangia uanzishwaji wa radio ya Kikristo ya Living Water katika Jiji la Mwanza.

Baada ya harambee hiyo haukupita muda mrefu, Akofu Magike akamuita Maganga Jijini Mwanza akimwambia kuwa ile radio waliyokuwa wanaifanyia harambee imeanza kuruka hewani hivyo kama anaweza aende Mwanza.

Kweli Maganga alienda Mwanza na kuiacha familia yake Jijini Dar lakini baadaye ilikuja kujiunga naye ambapo mpaka sasa yuko nayo huko jijini Mwanza.
Watoto wa Maganga. Brighton(Kushoto), na Brian(Kulia)
Maganga anaongeza kwa kusema kuwa ” Baada ya muda flani nilichaguliwa kuwa Meneja wa kwanza hapo Living Water na baadaye nikaacha kazi na kwenda katika Radio nyingine ya Kikristo ya  Hhc Alive Fm ya Jijini Mwanza pia nikawa Meneja katika kituo hicho. Badae nikatoka na kwenda Afya Radio kama Mtangazaji wa kawaida na ndipo nikarudi tena Living water na kuwa Meneja kwa mara nyingine tena katika kituo hicho cha Radio. Hapo sikukaa sana tena ndipo Mwanzoni mwa Mwaka huu 2013 nikarudi Hhc Alive Fm na kuwa Meneja tena”

“Nimejifunza kutokukata tamaa katika maisha hasa nikikumbuka toka wakati ule nikiwa mchoraji, kwa kweli kuna wakati ilipita wiki nzima bila kupata kazi, na kuna kipindi nilifanya mpaka kazi ya kupiga debe ili walau Mkono uende kinywani. Lakini kwa sasa namshukuru Mungu hata kama sina gari, lakini la ofisi lipo natembelea ingawa naamini la kwangu linakuja.” – Aliongeza Maganga.
Maganga akiwa katika Studio za Afya Radio
Kwa sasa Maganga ni Station Manager wa radio ya kikristo ya Jijini Mwanza ya Hhc Alive Fm (91.9Mhz) “Sauti ya Tumaini” na pia anajiandaa kuchukua masomo ya Diploma ya uandishi wa habari katika chuo cha uandishi wa habari na utangazaji cha Arusha baada ya kusoma Certificate ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal kilichopo Jijini Dar es salaam.

- To God Be The Glory -