Advertise Here

Tuesday, May 14, 2013

Maiti mbili zaokotwa kanisani Tabora.

Picha hii, haihusiani na Habari hii
MIILI ya watu wawili akiwemo mtoto wa mchungaji wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililo kwenye kitongoji cha Rehani, kata ya Tutuo, wilayani Sikonge, Tabora imeopolewa kwenye dimbwi la maji katika mazingira ya kutatanisha.

Mtoto wa mchungaji huyo aliyetambuliwa ni Pascal Yasin (27) na Utukufu Stefano Bugore (16) ambao ni wanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari ya Tutuo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vifo hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Edward Bukombe alikiri kupokea taarifa hiyo kutoka kwa watu waliotembelea eneo hilo.

Alisema marehemu hao hawakuwa na jeraha lolote katika miili yao ila mmoja alikuwa akitoka damu puani huku akibainisha kwamba uchunguzi wa awali umeonyesha kwamba marehemu walikuwa wakiogelea kwenye dimbwi hilo.

“Marehemu mmoja alikuwa na nguo ya ndani tu huku mwenzake akiwa na suruali bila shati, hivyo inawezekana walishindwa kuogelea wakazama… kwa sababu hawana alama yoyote ile katika miili yao,” alisema kaimu kamanda huyo.

Kwa mujibu wa Bukombe Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Sikonge amebainisha kuwa marehemu walizama baada ya kushindwa kuogelea hivyo wakanywa maji mengi. Aidha uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Awali mchungaji wa kanisa hilo wilayani Sikonge, Michael Namba, alisema upo uwezekano watu hao wameuawa kwa vile mchungaji wa kanisa la Tutuo hutumiwa ujumbe wa vitisho.

“Meseji zote za vitisho tunazo na tumetoa taarifa kwa polisi wa hapa Sikonge ili ziwasaidie katika uchunguzi wao, kwani hili lilipangwa na vitisho hivyo vinaendelea,” Alisema mchungaji Michael Namba.

Chanzo: Tanzania Daima

Tuesday, May 7, 2013

Hongera Boniphace Magupa na Jessica Honore kwa kufunga ndoa.

Juzi ilikuwa ni Siku ya Furaha kwa Wanandoa hawa wapya Boniphace Magupa ambaye ni Mtangazaji wa kituo cha luninga cha Chanel 10 na Jessica Honore ambaye ni Mwimbaji wa Nyimbo za Injili.

Harusi hii ilifungwa katika Kanisa la Anglikani mkoani Shinyanga, na kufuatiwa na tafrija fupi nyumbani kwa akina Boniphace Magupa maeneo ya Ndala, Shinyanga kabla ya kuelekea Ukumbi wa NSSF kwa ajili ya kuwapongeza Maharusi hawa.

Shughuli hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali kutoka mikoa mbalimbali Tanzania.
 Mtandao huu, unawatakia Maharusi hawa Maisha mema na yenye Furaha tele.

Monday, May 6, 2013

Bomu larushwa kanisani Arusha, mmoja afariki.

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 59 kujeruhiwa akiwamo Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla jana asubuhi baada ya mtu asiyejulikana kurusha bomu wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Jengo la Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha.

Miongoni mwa majeruhi, imeelezwa kuwa wanne ni mahututi. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amelielezea kuwa tukio hilo kuwa ni la kigaidi hasa kutokana na kumlenga Balozi wa Papa nchini na kwamba mtu mmoja anashikiliwa akihusishwa nalo.

Wataalamu wa mabomu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanachunguza aina ya bomu lililotupwa lakini uchunguzi wa awali unaonyesha lilikuwa limetengenezwa kienyeji.

Watu walioshuhudia tukio hilo wanasimulia kuwa bomu hilo lilirushwa yapata saa nne asubuhi wakati mgeni rasmi akijiandaa kufungua jengo la kanisa baada ya ujenzi wake kukamilika.

Shambulio hilo lilitokea wakati balozi huyo akiwa amesimama na mwenyeji wake, Askofu Mkuu, Josephat Lebulu, mapadri na watawa kutoka mashirika mbalimbali ya Jimbo Kuu la Arusha kwa ajili ya kukata utepe wa uzinduzi.

Kamanda Sabas alisema mtu aliyerusha bomu hilo alitokea nyuma ya kanisa hilo la ghorofa na kurusha bomu hilo kwa mkono wa kulia... “Alifanya jitihada za kupenya ili awafikie viongozi lakini alishindwa kutokana na wingi wa waumini waliokuwapo kwenye eneo hilo.”

Padri Moses Mwaniki aliyemshikia Balozi Padilla maji ya baraka yaliyotumika kubariki kanisa hilo, alisema kilichosaidia bomu hilo kutomfikia mwakilishi huyo wa Papa ni kutua mgongoni mwa mmoja wa waumini na kuanguka chini kabla ya kulipuka na kujeruhi watu.

“Ingawa hatuwezi kusema kwa uhakika, tunaamini mlengwa mkuu alikuwa mgeni wetu, Balozi Askofu Mkuu Padilla. Tunatakiwa kuliombea sana Taifa liondokane na matukio mabaya kama haya,” alisema Padri Mwaniki.

Baada ya tukio hilo, Balozi Padilla, Askofu Lebulu na viongozi wa kanisa hilo waliondolewa na kuhifadhiwa katika moja ya vyumba vya kanisa hilo kabla ya kutolewa kwenye eneo hilo yapata saa 5.30 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Msemaji wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Padri Festus Mangwangi alisema aliyerusha bomu hilo alishuhudiwa na mtoto mdogo aliyekuwapo kanisani hapo.

“Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto huyo, mtu huyo alikuwa amevaa kanzu nyeupe pamoja na koti la mvua lenye rangi ya kahawia na alikimbia mara baada ya kulirusha katikati ya watu. Ametusimulia kuwa mtu huyo baada ya kurusha bomu lile alikimbia na kuwahadaa watu kwa kuita ‘mwizi mwizi mwizi…’ akionyesha mbele kama kuna mtu anayemfukuza jambo lililowazubaisha watu lakini mtoto aliyemwona akirusha bomu aliwaeleza kuwa ndiye mhusika.”

“Waliomshuhudia mhusika akikimbia wanasema walishindwa kumwona mwizi aliyekuwa akimfukuza na hivyo kubaki wakimkodolea macho, hali iliyomfanya atokomee katikati ya nyumba za watu,” alisema Padri Mangwangi, ambaye aliongeza kuwa katika kipindi hicho kulikuwa kuna mkanganyiko mkubwa kutokana na bomu kulipuka na mtu huyo kudai kuna mwizi.

Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Julius Mbaga ambaye mkewe, Concesa (42), ni mmoja wa majeruhi, alisema ni kudra za Mwenyezi Mungu pekee ndizo zimeepusha madhara na maafa makubwa

Aliyefariki ametambuliwa kuwa ni Regina Losioki (46), ambaye alikuwa anaimba kwaya katika kanisa hilo. Alifariki baada ya kufikishwa katika Hospitali ya St. Elizabeth, Arusha.
Mamia ya watu jana walifurika katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kushuhudia watu waliokuwa wakifikishwa hapo kutoka katika eneo la tukio.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa, Dk Frida Mokiti alisema majeruhi 41 walikuwa wamelazwa Mount Meru, 16 walikuwa Hospitali ya St Elizabeth huku mmoja akiwa katika Hospitali ya Selian na mwingine Hospitali ya Kaloleni... “Kuna mgonjwa mmoja, ambaye amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC (Moshi) kwa matibabu zaidi.”

Waliojeruhiwa ambao majina yao yalibandikwa katika ukuta wa Hospitali ya Mount Meru ni Christopher Raymond (10), Consensia Mbaga (53), Deborah Joachim (24), Elizabeth Isdori (24), Bertha Cosinery (49), Anna Didas (52), Edda Ndowo(77), Derick Cyprian (8), Faustine Andrea (35), Mary Okech na Neema Daud (13).

Alex Arnold, Agripina Alex (9), James Gabriel (16), Loveness Nelson (17), Amalone Pius (25), Frank Donatus (10), Alphonce Nyaland (26), Athanasia Reginald (14), Phillemon Ceressa (49), Neema Daud (13) Sophia Kanda (72), Theofrida Innocent (21), Regina Darnes (17).

Mesoit Siriri (33), Clenes Pius (22), Joyce Yohana (15), Restuta Alex (50), Mathias Riha (74), Magreth Andrew (45), James Gabriel (16), Regina James (17), Elizabeth Masawe (15), Elizabeth Sauli (18), Njau (35), Yasinta Msafiri (160) na Doreen Pancras (28).

Waliokuwa katika Hospitali ya St. Elizabeth kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Samwel Mlay ni Fatuma Tarimo, Glory Tesha, Rose Pius, Isabela Michael, Jenipher Joachim, Samwel Laswai, John James, Joan Temba, Joram Kisera, Novat John, Neema Kilusu, Regina Shirima, Inocent Charles, Lightness na Anna Edward.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Wednesday, May 1, 2013

Word Explosion Summit yaanza rasmi Mwanza.

Mch. Emmanuel Mchutah
Ile Semina ya WORD EXPLOSION SUMMIT inayoingia siku ya pili leo, Jana ilifanyika katika Kanisa la TAG Nyamalango, Malimbe Mwanza na kuhudhuriwa na Watu wengi sana. Semina hiyo ambayo wanenaji ni Mchungaji Emamuel Mchutah na Janeth Mchutah, itafanyika kwa Siku 5, ambapo siku ya jumamosi itakuwa ndiyo siku ya mwisho ya Semina hiyo.

Siku ya Jana ilikuwa ni Siku ya Utangulizi tu, na Mafundisho rasmi yanaanza leo kuanzia Saa 11:45 Jioni mpaka Saa 2 Usiku. Kwa siku ya Jana, Vijana wengi walijitokeza kukabidhi Maisha yao kwa Yesu(Kuokoka).

Tazama video hii, inayoonyesha baadhi tu ya Watu walioamua kumpokea Yesu huku Mchungaji Emmanuel akiwaongoza sala ya toba