Mwl. Patrick Samson Sanga |
KATIKA kuumalizia mwaka huu wa 2012, nataka nikutafakarishe kwa
kukuuliza swali hili, Je! malengo yako uliyojiwekea katika mwaka 2012
katika nyanja mbalimbali kama vile kiroho, kihuduma, kifamilia, kikazi,
kibiashara, kiuchumi nk yamefanikiwa kwa kiwango gani? Na kama
hujafanikiwa je umejiuliza kwa nini hujafanikiwa kwa kiwango ambacho
unaamini ulitakiwa kufanikiwa? Je, umegundua nini ni vikwazo vya wewe
kufikia malengo yako?
Kama ukiyatafakari maswali hayo hapo juu utagundua kwamba najaribu
kutaka kujua kama kwanza huwa una tabia ya kuwa na malenngo, na kisha
kuweka mikakati inayotekelezeka ili kufikia hayo malengo, na mwisho
kufanya tathimini mara kwa mara ili kupima malengo yako yanafanikiwa
kwa kiwango gani kadri siku zinavyozidi kwenda.
Naam najua si watu wengi sana wenye tabia ya kujiwekea malengo na
hasa wapendwa. Ukiwauliza kwa nini huna malengo? atakuambia naenda kwa
imani. Ukimuuliza imani maana yake nini? Atakujibu, kuwa na uhakika wa
mambo yatarajiwayo tena bayana ya yale yasiyoonekana (Waebrania 11:1).
Tatizo la wapendwa wengi ni kutokujua uhusiano uliopo kati ya imani
na mtu mwenye malengo. Kulingana na tafsiri ya imani ni dhahiri kwamba,
kuwa na malengo ni namna mojawapo ya kuwa na imani, kwani ili imani
iwepo ni lazima kuwe na matarajio. Hivyo unapoweka malengo maana yake
unaifanya imani yako kuwa na uelekeo, kwa kujua mahali unapotaka kufika.
Kuna tafsiri nyingi za malengo na hasa kwa kutegemeana na kile
unachotaka kukipata au kukifikia, lakini tafsiri rahisi zaidi ni hii.
Malengo ni hatua fulani katika maisha ya mtu ambayo hajaifikia na hivyo
anataka kuifikia. Na jambo la msingi, unapaswa kufafanua vizuri lengo
husika ambalo unataka kulifikia. Ufafanuzi mzuri wa lengo au malengo
yako utakusaidia katika kujiwekea mikakati mizuri yenye kutekelezeka.
Katika ujumbe huu mfupi wa funga mwaka ya 2012 nataka tu kukukumbusha mambo kadhaa ya msingi yatakayokusaidia unapoanza kuweka malengo yako ya mwaka 2013.
1. Weka malengo yako mapema, kwa kuzingatia vipaumbele vyako.
Ni vema ukaweka malengo ya mwaka unaofuata kabla mwaka huo
haujaingia. Mfano, kama mpaka sasa bado hujaweka malengo unayotaka
kuyafikia katika mwaka 2013 basi tumia muda huu uliobaki kufanya kazi
hiyo. Kwa nini nasema jambo hili, hii ni kwa sababu utekelezaji wa
malengo yako unapaswa kuanza tarehe 01.01.2013 kama tukifika kwa neema
yake Kristo.
Kwa hiyo kama tarehe hiyo ikifika hujapanga malengo yako jua kwamba
tayari umeanza vibaya na kuna uwezekeano mkubwa wa kutokufikia malengo
yako. Ikiwa ulishaweka malengo kwa kipindi cha mika mtatu, mtano au
zaidi, bado pia unalazimika, kuyafafanua vizuri hayo malengo yako kwa
kuzingatia mazingira yaliyopo na rasilimali utakazohitaji. Naam
unapoweka malengo kumbuka kuyawekea muda wa hilo lengo kufikiwa.
Mfano;
Moja ya malengo yangu kila mwaka kihuduma, ni kuandaa masomo
yasiyopungua hamsini(50) na kuyaweka kwenye blog. Ukichukua 50
ukagawanya kwa miezi kumi na mbili unapata wastani wa masomo manne kila
mwezi. Na hii ina maana kila wiki ni lazima niandae somo moja. Kwa hiyo
ikipita wiki sijaandaa somo, ni dhahiri kwamba nitakwama katika kufikia
malengo yangu. Nimekupa mfano huu rahisi ili uone umuhimu wa kuweka
malengo mapema tena kwa kuyafunga kwenye muda.
Kwa uzoefu wangu katika kuweka malengo
kikazi,kihuduma,kiuchumi, kifamilia, nk, nimejifunza na kugundua kwamba
malengo ni muda, malengo ni mikakati na kisha malengo ni nidhamu
uliyonayo katika kutekeleza mikakati na hasa ile inayohusu fedha. Muda
ni ufunguo mkubwa wa kukusaidia kufikia malengo yako. Ukicheza na muda,
huwezi kufikia malengo yako. Na kwa sababu hii ni lazima ujifunze
kufikiri kimuda na kim-kakati kwa kila lengo unaloliweka.
Naam kufanikiwa kwa malengo ya Mtu binafsi, Shirika, Serikali nk kutategemea namna mtu/watendaji wa Serikali au Shirika husika wanavyotumia muda walionao, mikakati iliyopo na mwisho nidhamu yao katika utendaji wao. Naam, mambo haya matatu yakizingatiwa yatafanyika funguo za kufikia malengo yako au ya Shirika lako.
2. Weka mikakati ya kutekeleza malengo yako.
Ili malengo yako yaweze kutekelezeka, sharti uwe na mikakati
inayotekelezeka, vinginevyo huwezi kuyafikia malengo yako. Mikakati ni
mbinu, njia utakazotumia katika kutekeleza malengo yako. Naam kwa kuwa
malengo yako yanakuwa ndani ya muda fulani ni lazima na mikakati nayo
iwe kimuda. Katika kuweka mikakati, kuna baadhi ya malengo yatakutaka
ushirikiane na baadhi ya watu, sasa kuwa makini na nani unashirikana
naye katika kuyafikia malengo yako.
3. Fanya tathmini ya utekelezaji wako wa malengo.
Watu wengi sana, huwa wanasahau sana hiki kipengele katika
utekelezaji wa malengo yao, na ndio maana si wengi wanaofikia malengo
yao. Tathmini unaweza ukafanya kwa vipindi viwili au vitatu kwa mwaka.
Maana yangu ni kwamba unaweza uka-ugawa mwaka mara mbili na hivyo kuamua
kwamba utakuwa ukifanya tathmini zako mwezi wa sita na kumi na mbili.
Naam huu ndio mfumo ambao mimi binafsi huutumia. Hata hivyo kuna baadhi
ya malengo huwa nayafanyia tathmini yake kila mwezi, ingawa tathmini
kubwa huwa nafanya Juni na Desemba. Katika kufanya tahmini jambo kubwa
ni kuangalia mikakati yako imekusaidia kwa kiwango gani kufikia malengo
yako.
4. Boresha malengo kadri muda unavyokwenda, kwa kuzingatia tathmini unayoifanya.
Kama katika tathmini unayofanya mara kwa mara umegundua kwamba kuna
lengo au malengo haya tekelezeki, basi kwanza litazame hilo lengo tena
vizuri, kisha mikakati yake. Lazima kama siyo lengo, basi mikakati
unayotumia haijakaa vizuri, na kwa hiyo unaweza kuliboresha lengo lako
vizuri na hvyo mikakati yake pia. Mimi hutumia tathmini ya mwezi wa sita
kurekebisha baadhi ya malengo na kisha kuboresha mikakati yake. Na
kisha baada ya tathmini kubwa ya Desemba ndipo pamoja na mke wangu
tunaweka malengo yetu ya mwaka unaofuta. Jambo la msingi hapa ni
kuhakikisha kwamba malengo tunayoweka kila mwaka yanalenga kutufikisha
kwenye malengo yetu ya miaka mitano mbele, tuliyokwisha kuyaweka tangu
mwanzo.
5. Jenga mazoea ya kuyasoma na kutafakari malengo yako mara kwa mara.
Jambo hili litakuwekea msukumo wa kuhakikisha unatekeleza mikakati
yako ili kuyafikia malengo yako. Mfano unaweza kuweka malengo yako
kwenye Laptop/Computer yako, unaweza ukaweka malengo yako kwenye meza
yako ya kusomea au unaweza ukaweka ‘Remainder” kwenye simu yako iwe
inakukumbusha kila wiki kupitia malengo yako nk. Hata hivyo ni vema
ukaweka, malengo/mikakati yako, mahali ambapo ni salama kwa maana ambayo
haitakuwa rahisi kwa mtu au watu wengine kuona, Shetani asije
akawatumia hao katika kukwamisha malengo yako.
Kutokana somo hili, hebu angalia katika mwaka wa 2012 kama uliweka
malengo, umeyafikia kwa kiwango gani? Naam kama haujafanikiwa vizuri,
basi naamni somo hili litakusaidia katika kujipanga kwa mwaka 2013 ili
kama kwa neema ya Mungu tukifika Desemba 2013 unapofanya tathmini ya
mwisho wa mwaka uwe na sababu ya kumshukuru Mungu kwa namna
alivyokusaidia kuyafikia malengo yako.
Mungu akubariki sana. Mimi na familia yangu, tunakutakia heri ya Mwaka mpya wa 2013 na Neema ya Kristo na iwe nawe daima.
Mwl. Patrick Samson Sanga
+255 755 816 800