UONGOZI
wa Kanisa la Katoliki, Parokia ya Kinyerezi Dar es Salaam unalazimika
kugharimia ufukuaji wa makaburi zaidi ya 15 ya Waislamu yaliyopo kwenye
kiwanja namba 1370 kitalu B kilichopo katika Kata ya Kinyerezi , baada
ya kupewa kwa shughuli za kijamii.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hii Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Venance Kweka
alisema wanalazimika kugharimia ufukuaji wa makaburi hayo ili yaweze
kuhamishwa kutoka katika kiwanja kupisha shughuli nyingine za kijamii kama Ujenzi wa hospitali katika eneo hilo.
Alisema
tayari wamejiandaa kugharimia shughuli hiyo kwa kuwa makaburi hayo
ndiyo pekee yanayokwamisha kuanza kwa mikakati ya ujenzi wa hospitali
hiyo, ambayo kanisa linaamini itakuwa ni msaada mkubwa kwa kinamama na
watoto wanaoishi katika eneo hilo la Kinyerezi.
Taarifa
iliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa Halmashauri ya Ilala Gabriel
Fuime, ilifafanua kuwa itasimamia zoezi hilo kwa Sheria ya Serikali za
Mitaa( Mamlaka na Miji) ya mwaka 1982, kanuni ya mwaka 2008 namba 4 c
ambako itatumia wataalam wake.
Fuime
katika taarifa yake hiyo alisisitiza ndugu na jamaa wa waliozikwa
katika eneo hilo kuwasiliana na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kinyerezi
wakiwa na barua ya utambulisho kutoka kwenye ofisi ya Serikali ya mtaa
wanaoishi kabla ya Januari 20 mwaka 2013.
Alibainisha
kuwa makaburi hayo yanatarajiwa kuhamishiwa kwenye makaburi ya
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yaliyopo kata ya Kitunda eneo la
Mwanagati Februari 9 mwaka 2013 baada yataratibu zote kukamilika.
- Juma Mtanda -