Advertise Here

Wednesday, December 26, 2012

Wachungaji wafukuzana KKKT Dayosisi ya Kaskazini kati.

Askofu Mkuu wa KKKT, Dr. Alex Malasusa
 HALI imezidi kuwa tete katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati baada ya Mchungaji Philemon Mollel kufukuzwa kazi na kusimamishwa kutoa Huduma katika Kanisa hilo Nchini.

Wiki iliyopita bodi ya Dayosisi hiyo chini ya Uenyekiti wa Israel Ole Karyongi ambaye pia ni katibu mkuu wa KKKT, ilimtimua kazi Meneja wa Hotel ya Corridor Springs Bw. John Njoroge kwa Tuhuma za Ubadhilifu wa fedha.

Vyanzo vya Habari vinasema kuwa, Chanzo cha Mchungaji Philemon Mollel kufukuzwa kazi, ni kushindwa kutekeleza mambo matatu ambayo Tume maalum ilimtaka Mch. Mollel ayafanye, na alipewa Siku 3 za kuomba radhi na hakufanya hivyo.

Habari zaidi zinasema kuwa, mambo matatu ambayo Mch. Mollel alitakiwa kuyafanya ni; 1. Kumuandikia Barua Askofu wa Jimbo la Kaskazini Kati Dr. Thomas Lazer kueleza ni kwanini alimkashfu na kumdharau. 2. Kutoa tamko katika Mtaa wa Azimio Ibadani Desemba 23, kuomba radhi kwa yale aliyotamka.

3. Amwarifu Katibu Mkuu kwa Barua baada ya kuyatekeleza hayo na awe amefanya hivyo kabla ya Desemba 24 Mwaka huu.

Habari zinaeleza kuwa, walioteuliwa Desemba 14 Mwaka huu na kwenda kumuona Mch. Mollel ili kutekeleza hayo ni Pamoja na Msaidizi wa Askofu, Mch. Solomon Massangwa, Katibu Mkuu wa Jimbo la Arusha Magharibi Mch. Godwini Lekashu na Katibu Mkuu Israel Ole Karyongi.

Hata hivyo Mch. Mollel alipopigiwa simu, alikiri kupokea nakala ya barua hiyo ya kufukuzwa kazi na kuvuliwa Uchungaji lakini alisema hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo. Mch. Mollel aliongeza kwa kusema kuwa Uamuzi huo umechukuliwa kwa Chuki na Fitina, na haukuangalia madhara ya Deni la Sh. Billioni 11 endapo Kanisa litashindwa kulipa fedha hiyo.

- Habari Leo -