JUKWAA la Wakristo Tanzania (TCF), limeitaka Serikali ya Rais Jakaya
Kikwete kutoa ufafanuzi juu ya baadhi ya madai mbalimbali yanayotolewa
na Waislamu dhidi ya Wakristo, vinginevyo Serikali ikiri kwamba inaunga
mkono madai hayo ya Waislamu.
TCF ni jukwaa linalojumuisha Taasisi kuu za Umoja wa Makanisa nchini,
ambazo ni pamoja na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste
Tanzania (PCT) na Kanisa la Waadventiste Wasabato (SDA).
Tamko hilo limetokana
na maazimio ya kikao cha wawakilishi wa taasisi hizo kilichofanyika Dar
es Salaam, Desemba 6 mwaka huu, chini ya Mwenyekiti wake Askofu Bruno
Ngonyani na Katibu wake, Mchungaji Dk. Leonard Mtaita. Lilianza
kutangazwa katika ibada ya Krismasi juzi usiku na kurudiwa jana katika
Ibada ya Kataifa mjini Moshi na Askofu Dk. Martin Shao.
Katika tamko hilo ambalo limechapishwa kwa ukamilifu ndani
ya gazeti hili , TCF inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi juu ya madai
kadhaa yanayotolewa na Waislamu mara kwa mara dhidi ya Wakristo,
yakiwamo madai ya kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa ikiongozwa na
Mfumo Kristo.
Mengine ni madai ya kuwapo kwa ‘Memorandum of Understanding (M.o.U)’
ya mwaka 1992 baina ya Makanisa na Serikali kwa ajili ya huduma za
Makanisa kuhusu sekta za afya na elimu, uchochezi unaofanywa na baadhi
ya viongozi wa Kislamu dhidi ya Wakristo, tishio la kuuawa kwa maaskofu
na wachungaji wa makanisa pamoja na tukio la uchomaji wa makanisa
Mbagala na Zanzibar.
Kwa mujibu wa maaskofu na wachungaji hao, kuendelea kukaa kimya kwa
Serikali kuhusu madai hayo ya Waislamu, kwanza kunachangia kuongezeka
kwa uhusiano mbaya baina ya dini mbili hizo, na hivyo kuhatarisha umoja
na mshikamano wa taifa lakini pia kunatoa taswira kwa viongozi hao wa
Kanisa kujua kwamba Serikali inaunga mkono chokochoko zote hizo za
Waislamu dhidi ya Wakristo.
Kikao hicho cha TCF kimewaagiza viongozi wote wa makanisa nchini kusoma
tamko hilo mbele ya waumini wao kabla ya mwisho wa mwaka huu, wakianzia
na ibada za Sikukuu ya Krismsi na Mwaka Mpya kutokana na kile ambacho
makanisa hayo yanasema juhudi zao za kutaka kukutana na Rais Kikwete ili
wamweleze msimamo wao huo wa Kanisa nchini, kukwama.
Kuhusu madai ya kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa ikiongozwa na Mfumo
Kristo, tamko hilo la TCF linasema: “Maneno ya kashfa ya hoja kuwa nchi
inaendeshwa kwa mfumo kristo, hayana msingi wowote. Jukwaa la Wakristo
nchini linakanusha wazi kuwa nchi hii haiongozwi kwa mfumo kristo.
“Labda kwa kuwakumbusha tu, viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu
Tanzania asilimia 90 ni Waislamu, itakuwaje nchi iendeshwe na mfumo
kristo? Rais wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa
Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (wote hawa ni
Waislamu).
“Upande wa Zanzibar (viongozi Waislamu) ni asilimia 100. Na si kweli
kwamba Zanzibar hawapo Wakristo wenye sifa za kuongoza. Hata uwakilishi
wa Tume ya Kuandikwa Katiba Mpya, theluthi mbili ya wajumbe wake ni
Waislamu, na mifano mingine mingi tu hii ni baadhi tu.
“Nchi hii (inaendeshwa kwa) misingi ya kidemokrasia, na Serikali yake
haina dini bali wananchi wake ndio wana dini. Jukwaa la Wakristo
linaitaka Serikali ithibitishe ukweli huu badala ya kukaa kimya wakati
maneno ya uchochezi kama haya yanaenezwa wazi na hadharani.”
Kuhusu M.o.U, tamko linasema: “Memorandum of Understanding (M.o.U)
ya mwaka 1992, kwa ajili ya huduma za Makanisa (Afya na Elimu) kwa
jamii ya Watanzania katika huduma za hospitali, vituo vya afya na
zahanati pamoja na shule mbalimbali zinazoendeshwa na Makanisa. Kanisa
limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru
na baada ya uhuru pasipo ubaguzi.
“Ili kuondoa hali ya Kanisa kuendelea kutukanwa, chuki na kukashifiwa
juu ya M.o.U, ambayo ni jambo zuri la kuwahudumia Watanzania afya zao,
Jukwaa la Wakristo linaitaka Serikali ama izirudishe hospitali na shule
za Makanisa kwa wamiliki wake wa awali, yaani Makanisa, na zile za
Waislamu warudishiwe. Kama hili haliwezekani, basi Serikali itoe tamko
la ufafanuzi juu ya M.o.U hiyo, maana na makusudi yake na manufaa yake
kwa Watanzania.”
Kuhusu uchochezi, matusi dhidi ya Kanisa na kuzorota kwa uhusiano baina
ya Uislamu na Ukristo, Jukwaa hilo linasema: “Ni wakati wa kukubali
kwamba misingi ya Haki, Amani na Upendo katika Taifa letu vimetikiswa
kwa kiwango kikubwa. Uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa maksudi
unaofanywa na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu ukiendeshwa na
kuenezwa kupitia vyombo vya habari vya kidini, mihadhara, kanda za
video, CD, DVD, vipeperushi, makongamano, machapisho mbalimbali na kauli
za wazi za viongozi wa siasa na dini husika, pasipo Serikali kuchukua
hatua yoyote ikibakia kimya tu, inatoa taswira kwa viongozi wa Kanisa
kujua kuwa Serikali inaunga mkono chokochoko hizi. Jambo hili
linavyoendelea kuachwa hivi hivi, linaashilia hatari kubwa ya
kimahusiano siku zijazo.
Aidha, Jukwaa hilo la makanisa nchini limeitaka Serikali kuhakikisha
kwamba hadhi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere inahifadhiwa.
“Huyu ni kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu
akitetea Watanzania wote bila kuwabagua, akiimarisha umoja, amani na
upendo kwa watu wote. Kashfa, kejeli na habari za uongo dhidi yake ni
kuondoa moja ya alama muhimu ambazo kiongozi huyo alisimamia kwa ajili
ya umoja wa kitaifa, mambo yote hayo yanayoenezwa yanalenga kukipotosha
kizazi hiki na vizazi vijavyo juu ya juhudi binafsi za kiongozi huyo kwa
Watanzania aliowapenda sana.