Advertise Here

Monday, September 2, 2013

Gospel Music Concert ndani ya Kigamboni.

 
 
Pastor Abel na Rebecca Orgenes wanakukaribisha katika Tamasha maalumu la Nyimbo za Injili linalowaleta pamoja, kwaya mbalimbali, vikundi wakiwemo Glorious Celebration na waimbaji binafsi akiwemo Mirium Lukindo Mauki, Tumaini na Ona, Amoni Kilahiro na wengine wengi.

Ni Jumapili ya tarehe 8 mwezi wa 9 kuanzia saa 9 mchana na kuendelea. Na mahali ni Kigamboni, Mji mwema, Maweni kwenye ukumbi wa Barakuda. (Barracuda).

KUMBUKA HAKUNA KIINGILIO

Mawasiliano: 0754363096

Simanzi yatawala Mapokezi ya Mwili wa Marehemu Askofu Dr. Mosses Kulola Mwanza.

Ndege iliyobeba mwili wa Marehemu ikiwasili Uwanja wa ndege wa Mwanza
Jana mida ya Saa 7:09 Mchana, mwili wa Marehemu Dr. Mosses Kulola uliwasili uwanja wa ndege wa Mwanza na kupokelewa na watu mbalimbali akiwepo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh. Engeneer Evarist Ndikilo, Maaskofu mbalimbali, Wachungaji, na waumini wa Makanisa mbalimbali Mwanza pasipo kujali Imani za dini zao.

Mwili huo baada ya kupokelewa ulipelekwa moja kwa moja nyumbani kwa Marehemu Askofu Dr. Mosses Kulola ambapo simanzi ilizidi na ni kama msiba ulianza upya kwani kila kona ilikuwa ni vilio tu.

Mwili wa Askofu Dr. Mosses Kulola utaagwa kesho katika Uwanja wa CCM Kirumba kuanzia mida ya Saa 4:00 Asubuhi hadi Saa 12:00 Jioni ili kuwapa nafasi nzuri na ya kutosha wakazi wa Mwanza na Mikoa Jirani kupata fursa ya kuuaga mwili wa Marehemu.

Hizi ni baadhi tu ya Picha za Mapokezi ya Jana, kuanzia Airport kuelekea nyumbani kwa Marehemu
Umati wa watu wakisubiri mwili wa Marehemu
Gari lililobeba Mwili wa Marehemu
Mtoto wa Marehemu Mch. Daniel Kulola (wa kwanza kushoto) akiwa na viongozi mbalimbali
Mch. Daniel Kulola (kushoto) na Mwl. Jacob (kulia)
Mke wa Marehemu akishuka kutoka kwenye ndege
Polisi nao walikuwepo wa kutosha kuhakikisha usalama unakuwepo
Emmanuel Mbasha
Watu wakiwa wamejipanga barabarani
Msafara wa Magari ukielekea nyumbani kwa Marehemu
Kwasasa mwili wa Marehemu umewekwa katika hospitali ya Bugando na kesho utakuwa ukiagwa katika Uwanja wa CCM Kirumba.


- Picha Zote na Baraka Samson -

Safu ya James Kalekwa: Mambo yakupasayo Kujua Juu ya Maamuzi - Part I.

Mwl. James Kalekwa

Utangulizi wa Somo:

Kwasababu ya mazoea ya kufanya maamuzi mara kwa mara, watu wengi wamejikuta wamenaswa kwenye mtego wa kutofahamu upana, kina na ukubwa wa jambo hili muhimu. Kila mwanadamu hufaya maamuzi ya kudumu au ya kitambo (muda mfupi); maamuzi ya mara moja (sudden) au yale yachukuayo muda mrefu kuyafikia. Kwa ujumla wake, maisha ya mwanadamu hutawaliwa na maamuzi. Mfano kutembelea blog hii ni uamuzi, kusoma fundisho hili kwenye blog ni uamuzi, kuamka toka kitandani ni uamuzi, ndoa ni uamuzi, kuokoa ni uamuzi… Ungeweza kuwa tofauti na hivyo ulivyo, lakini sivyo kwasababu ya maamuzi.
Ni jambo la msingi sana kufahamu pia ya kwamba maamuzi huathiri si tu maisha ya mtu husika bali huyagusa mpaka maisha ya wale wanaomuhusu sawasawa na nafasi yake – familia, jamaa, jamii, taifa, taasisi n.k
Kwakuwa maamuzi ni jambo la Muhimu kiasi hiki, fuatana nami kwenye mfululizo wa mafundisho haya juu ya maamuzi ili uwe na ufahamu juu ya nini unakiendea kila fursa ya kufanya maamuzi inapojihudhurisha mbele yako. Watu wasio na maarifa na ufahamu hukutwa na kushangazwa na mambo (they are caught by surprise) pindi yanapoanza kutokea. Ni maombi yangu kwa Mungu kwamba Roho Mtakatifu akusaidie kuyatambua yote haya, kwa jina la Yesu Kristo!

Dhana ya Maamuzi kwenye Neno la Mungu

Yoeli 3:14
“Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya BWANA i karibu, katika bonde la kukata maneno.”

1 Korintho 6: 5
“Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake?”

Matendo ya Mitume 24:22
Basi Feliki aliwaahirisha, kwasababu alijua habari za Njia ile kwa usahihi zaidi, akasema, Lisia jemedari atakapotelemka nitakata maneno yenu.

Mith. 16:10
Kukata maneno huwa katika midomo ya mfalme; Kinywa chake hakitakosa katika hukumu.”

Nabii Yoeli anatutambulisha dhana muhimu sana kwenye maisha ambayo amechagua kuiita “kukata maneno”. Nimeambatanisha mistari mingine ili kupana wigo wa uelewa juu ya dhana ya kukata maneno. Ukiisoma mistari inayotangulia na inayofuata baada ya hiyo niliyoambatanisha hapo, utang’amua mara moja ya kwamba kukata maneno si dhana mpya bali ni neno linalowasilisha maana ya kufikia maamuzi ya kimahakama (kunapokuwa na pande mbili zinazokinzana na inatakiwa pande hizo zifike uelewa wa pamoja “consensus”  juu ya jambo fulani); kufikia neno la mwisho juu ya, ama kuhitimisha  mjadala unaoendelea juu ya hoja fulani… Kwa lugha rahisi na ya kueleweka kwa wengi, maelezo yote hayo yaliyotangulia juu ya dhana ya kukata maneno yanaweza kufupishwa kwa neno hili: kufanya maamuzi
Pia ukitazama kwa umakini utagundua ya kwamba Yoeli anatambulisha mahali “venue” pa kufanyia maamuzi. Si kila mahala ni maalum kwa maamuzi… La hasha! Kuna sehemu maalum kwa shughuli hii, na hiyo sehemu inaitwa “Bonde la Kukata maneno”.  Ili tuweze kumuelewa vyema Yoeli, basi karibu ujifunze juu ya dhana ya mihula mitatu kwenye maisha ya mwanadamu ambayo hiyo itatupa kujua wajibu wetu katika zoezi hili Muhimu… Kufanya maamuzi!

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

Somo limeandaliwa na:
Mwl. James Kalekwa
0714 762669/0754917764 
Email: jameskalekwa@gmail.com

Sunday, September 1, 2013

Harusi ya Mwimbaji Emmy Kosgei na Mtume Anselm yafana.

Mtume Anseln Madubuko na Emmy Kosgei wakifunga ndoa
Jana ilikuwa ndiyo siku ya Harusi ya Mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za Injli kutoka Nchini Kenya, Emmy Kosgei alipofunga ndoa na Mtume Anselm Madubuko raia wa Nigeria anayehudumu katika Kanisa la Revival Assembly Church lililopo Lagos, Nigeria.

Harusi yao ilifanyika katika hotel ya Safari Park na wamefunga ndoa huku Mtume Anselm Madubuko akiwa na umri wa Miaka 55 na Emmy Kosgei akiwa na umri wa Miaka 33.

Mke wa awali wa Mtume Anselm Madubuko alifariki mwezi wa 7. Jambo linalowashangaza wengi ni kuwahi kwake kuoa baada ya mke wake kufariki. Katika kuondoa utata huo, Mtume Anselm Madubuko amesema: “It is how I have chosen to do it. I have decided to move on. I found out that 10 years and even 20 years will not be enough to forget my late wife. The time anybody remarries has nothing to do with your former partner.”

Akiongelea namna walivyokutana na Emmy Kosgei alisema: “I met her in one of my trips abroad. We were both invited as guest ministers in an event. I was to minister as a preacher, while she as a music minister. When she ministered, I said to myself this girl has a good spirit. Later, I invited her as a guest artiste to perform in Azusa. People loved her and her music. I never knew things would turn out this way.”

Naye Emmy Kosgei alipohojiwa kuhusu uamuzi wake wa kuolewa na Mtume Anselm Madubuko alisema: “He loves me as I am and understands what I do. I wish people would mind their own business and let us be. He approached me and asked for my hand in marriage. He is the only man who had the confidence to approach me.”

Zifuatazo ni Picha za Harusi yao iliyofanyika Jumamosi ya Jana
High Table



 



Mtandao huu unawatakia Maisha Mema na yenye Baraka tele.

Mwili wa Marehemu Askofu Mosses Kulola wawasili Mwanza.

Msafara wa Mapokezi ya Mwili wa Marehemu Askofu Dr. Mosses Kulola kutoka Airport Mwanza

Mwili wa Marehemu Askofu Dr. Mosses Kulola umewasili Mwanza tayari kwa taratibu zingine kufuatwa ikiwa ni kuwapa nafasi wakazi wa Mwanza na Mikoa jirani kutoa heshima zao za Mwisho kabla ya Mazishi yatakayofanyika siku ya Jumatano.

Kwa mujibu wa maelezo ya awali, Mwili wa Askofu Dr. Mosses Kulola utaagwa Siku ya Jumanne katika Uwanja na CCM Kirumba na Mazishi yatafanyika Siku ya Jumatano katika Kanisa la EAGT Bugando.

Endelea kutembelea Mtandao huu, na tutakufahamisha kila linalojiri Mkoani Mwanza kuhusiana na Msiba huu wa Baba/Babu yetu mpendwa Askofu Dr. Mosses Kulola. Picha za Mapokezi ya Mwili wa Marehemu tutaziweka muda mfupi ujao.