Advertise Here

Saturday, January 12, 2013

Kuna Kuinuka tena katika Jina la Yesu.

 
"Kwa kuwa japo mtu mwenye haki huanguka mara saba, huinuka tena, lakini waovu huangushwa chini kwa maafa" -Mithali 24:16.

Mambo ambayo yamekuwa na tabia ya kuisonononesha mioyo ya wanadamu na pale tunapoona kuwa tumeshindwa kufanya jambo fulani tulilokusudia, na pale ambapo tumejikuta tukitenda mambo yasiyofaa katika sehemu mbalimbali za maisha yetu. Kwa wana wa Mungu, pale tunapomkosea Mungu kwa namna mbalimbali, mara nyingine tunakata tamaa na kuona kuwa hatuwezi kabisa kuishi katika uhusiano mzuri na Mungu wetu.

Kwa ujumla, kuna mambo kama haya ambayo yanatukatisha tamaa ya kuendelea mbele katika mambo ya mafanikio yetu. Ni wazi kuwa, tukiendelea kuyatafakari mambo hayo tuliyoshindwa, na tukaendelea kukata tamaa, basi hiyo itachangia sana sisi kukosa morale ya kusonga mbele na kufanikiwa katika maisha yetu.

Watu wengi wamekuwa wakifanya uamuzi wa kumkabidhi Mungu maisha yao yote na kuamua kuishi maisha yao kwa uongozi wa Neno la Mungu na kumcha Mungu kwa mioyo yao yote, lakini mara majaribu yajapo baadhi hushindwa kuhimili majaribu hayo na hivyo kujikuta wanaanguka katika dhambi.

Katika hali kama hiyo, watu wengi hukata tamaa na kuona kuwa hawawezi kabisa kuishi kwa kumcha Mungu, na hata wengine kusema kuwa haiwezekani kuokoka ukiwa hapa duniani. Kwa ujumla wake, kuvunjika moyo limekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa wana wa Mungu ulimwenguni pote.

Lakini je, Neno linasemaje kuhusu watu wanaojaribu kufanya jambo jema na kuanguka? Je, inawaruhusu kukata tamaa na kuamua kurudi nyuma? Hebu tutafakari maandiko yafuatayo: "Kwa kuwa japo mtu mwenye haki huanguka mara saba, huinuka tena,lakini waovu huangushwa chini kwa maafa" -Mithali 24:16.

Katika mstari huu, Neno latuambia kuwa, mtu mwenye haki anaweza akaanguka (akashindwa kutimiza jambo fulani katika maisha yake) hata mara saba, lakini katika mara zote hizo huinuka tena. Neno halisemi kuwa baada ya kuanguka mtu huyo ataendelea kubaki chini, bali, huinuka tena.

Mtu huyo aliyenenwa katika mstari huo hapo juu, yeye anapoanguka hiyo huwa ni nafasi ya kujifunza zaidi kutokana na kuanguka kwake ili asianguke tena,na kisha huinuka tena. Hujifunza kutokana na makosa.

Je, umejaribu kufanya bidii kuimarisha uhusiano wako na Mungu (maombi, kusoma Neno, kuhudhuria Ibadani) lakini mara nyingi umekuwa ukianguka dhambini na sasa umekata tamaa? Je, kuna mambo ambayo umeshindwa kuyatimiza katika mipango ya maisha yako na sasa umekata tamaa?

Je, kwa makosa uliyoyatenda huko nyuma moyo wako umehuzunika na umekataa tamaa hata ya kunia kutenda makubwa katika mwaka huu wa 2012? Kama ni ndiyo, basi hili ni Neno la Bwana kwa ajili yako siku ya leo: "Inuka tena". Kumbuka huo mstari tuliosoma "Kwa kuwa mtu mwenye haki huanguka mara saba,huinuka tena."

Jipe moyo katika Yesu Kristo, jitie nguvu katika Bwana upate morali ya kusonga mbele tena na kutenda makuu katika mwaka huu. Jifunze kutokana na makosa yako na kisha inuka uendelee mbele. Mwombe Mungu na umwamini tena mwaka huu naye atakusaidia na kukufanikisha, mradi tuu usizimie moyo.

Wewe ni Askari wa Kristo na mwana wa Mungu aliye hai, usivunjike moyo kamwe, Amen?

TUOMBE ...
"Baba katika Jina la Yesu Kristo, nakushukuru sana kwa ajili ya Neno lako hili uliloniletea kwa njia hii. Baba, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutenda mambo makuu katika maisha yangu. Asante kwa yale yote ambayo nimeweza kuyatenda kwa mafanikio, na ninaomba unipe macho ya rohoni, nipate kujifunza kutokana na makosa yote niliyoyafanya katika maisha yangu na niweze kuwa bora zaidi. Ninaomba unipe nguvu kwa Jina la Yesu Kristo, ili nisizimie moyo kamwe kwa sababu ya madhaifu yangu, bali nipate kuwa hodari katika Bwana na nitende makuu kwa uwezo wako Mungu Baba. Nimeomba haya na kuamini, katika Jina la Yesu Kristo, Amen."

- Frank Lema -