Advertise Here

Monday, January 21, 2013

Waumini KKKT Usharika wa Mjini Kati Arusha, wagoma kusali Kanisani.

Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Arusha wakiandamana kwenda Usharika wa Mjini Kati ambako ni ofisini kwa Mchungaji wa Usharika huo, Titus Laroya kupinga kile walichodai ni ufisadi katika ujenzi wa Kanisa hilo jana. (Picha na John Mhala).
Washarika wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati wakiwa kwenye Maandamano kuelekea Usharika wa Mjini Kati kwenye Ofisi ya Mchungaji wa Usharika huo.
KATIKA hali isiyo ya kawaida waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Mjini Kati Arusha, wamesusia Ibada ya Jana Jumapili kushinikiza kupata taarifa ya fedha ya ujenzi wa Kanisa la Usharika huo.
 
Tofauti na ilivyo kila Jumapili, jana waumini hao baada ya kujikusanya katika viwanja vya Kanisa linalojengwa  na kufikia zaidi ya 500, waliamua kuandamana hadi ofisini kwa Mchungaji wa Usharika huo, Titus Laroya kumtaka aeleze fedha za ujenzi wa kanisa hilo zilikokwenda.
 
Wakizungumza na mwandishi, waumini hao wamedai wamekuwa wakichangia ujenzi huo kwa miaka miwili sasa lakini hawaoni hatua zinazolingana na michango yao na kwa sasa ujenzi umesimama.
 
Wakiwa na mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali, baadhi ya waumini hao walibeba vifaa vya ujenzi vilivyodaiwa kununuliwa na Mchungaji  Laroya na kuvipeleka katika ofisi hiyo kwa madai kuwa ni feki na, havifai kwa matumizi ya ujenzi wa kanisa hilo.
 
Awali waumini hao walifika katika viwanja vya kanisa hilo saa 12.30   kuhudhuria ibada ya kwanza, lakini hali ilikuwa ya wasiwasi na baada ya muda walihamasishana kugoma kuingia kanisani.
 

Kutokana na hali hiyo ya wasiwasi huku wakionekana wazi kuwa na jazba, Mchungaji huyo aliamua ‘kuingia mitini’ kimya kimya huku akiacha gari lake katika maegesho ya kanisa hilo.
 
Baada ya kugoma kuingia kanisani na bila kumuona Mchungaji, ilipofika saa 1.45 waumini hao walifikia uamuzi wa kuandamana kwenda Ofisi ya Mchungaji Laroya iliyopo mbali kidogo na kanisa hilo, katikati ya Jiji la Arusha, Barabara ya  Goliondoi meta  chache karibu na Ofisi Kuu ya Dayosisi.
 
Polisi walifika katika kanisa hilo wakati waumini hao wakijiandaa kuandamana na kuangalia hali halisi na kuwaacha waumini hao kuendelea na maandamano huku wakiimba nyimbo mbalimbali za mapambio za  kupiga vita ulaji na ufisadi unaoshika kasi katika Kanisa hilo kwa sasa bila viongozi wa juu kuchukua hatua.
 
Akizungumza na mwandishi mara baada ya kumalizika kwa maandamano hayo, mmoja wa waumini hao,  Elibariki Mbise alisema tangu waanze kutoa michango ya ujenzi wa kanisa hilo kwa zaidi ya miaka miwili na nusu, hakuna kinachoendelea na kila wakiuliza wanatishiwa kutengwa katika usharika huo.
 
Mbise alidai mbali ya vitisho hivyo, kibaya zaidi ni hatua ya Kamati ya Ujenzi wa Kanisa hilo kukosa taarifa juu ya kiasi kilichopatikana kwa muda wote huo kwa kuwa majukumu hayo yanafanywa na Mchungaji Laroya mwenyewe.
 
Alidai Kamati ya Ujenzi na baadhi ya wazee wa usharika huo wakihoji mara kadhaa juu ya michango na sadaka za ujenzi wa kanisa hilo, wamekuwa wakitishiwa kutengwa hatua inayoonesha kuwa Kanisa linaendesha shughuli zake kibabe na si kwa uwazi kwa manufaa ya wote.
 
Msharika mwingine, Richard Mollel alidai kinachowaudhi   ni Mchungaji Laroya kuacha kuendelea na ujenzi wa kanisa hilo kwa muda wa miaka miwili na zaidi na kununua vifaa ‘feki’ kwa gharama kubwa huku baadhi  ya vifaa hivyo vikiozea ndani ya stoo ya kanisa hilo.
 
Mollel aliendelea kudai kuwa Mchungaji huyo kambadilisha mhandisi wa awali aliyekuwa akijenga kanisa hilo na kumtafuta wa kwake bila kuitaarifu Kamati ya Ujenzi ambayo haijui sababu za kutimuliwa kwa mhandisi wa awali.
 
‘’Hapa Kamati ya Ujenzi ni hewa kwa sababu haijui chochote na kila kitu anafanya Mchungaji, sasa ndio maana tumeamua kumpelekea vifaa vyake vyote feki ofisini kwake na tunataka maelezo ya kiasi cha fedha kilichopatikana kwa muda wa miaka hiyo miwili vinginevyo hakitaeleweka, ’’alidai Mollel.
 
Mchungaji Laroya pia anatuhumiwa na Kwaya ya Vijana ya Uinjilisti ya Usharika huo kwa kula fedha za harambee ya ununuzi wa basi la kwaya zaidi ya Sh milioni 80 zilizochangwa mara tatu kwa nyakati tofauti; mara mbili harambee ikiongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Makuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri.
 
Baada ya kubanwa na wana kwaya hao, Mchungaji Laroya aliwapooza wanakwaya hao kwa kuwanunulia basi chakavu lenye thamani ya Sh milioni 60 lakini basi hilo lilisusiwa na kwaya hiyo na hadi leo limeegeshwa katika uwanja wa Kanisa hilo la Mjini Kati.
 
Juhudi za kumpata Mchungaji Laroya kuzungumzia
shutuma hizo zilizoelekezwa kwake, zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kufungwa kutwa nzima ya jana huku akiwa haonekani ofisini kwake kila alipotafutwa.

- Habari Leo -