Advertise Here

Thursday, April 11, 2013

Kanisa Katoliki launga mkono tafiti zinazozingatia Maadili.

KANISA Katoliki linaendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo na sayansi katika tiba ya mwanadamu kwa kuzingatia maadili, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mafano wa Mungu. Linawashukuru wadau mbali mbali wanaowezesha kufanikisha tafiti za kitaalam kwa ajili ya mafao ya binadamu.

Kanisa tangu mwaka 2011 limejiwekea utaratibu wa kutaka kuelewa, kufahamu na kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na masuala ya viini tete kama sehemu ya tiba kwa kuangalia madhara yake katika Jamii husika, ndiyo maana Kanisa linaendelea kujitaabisha kufuatilia kwa makini tafiti za kisayansi katika tiba ya mwanadamu, kwa kuzingatia: zawadi ya maisha, maadili na utu wema.

Haya ni kati ya mawazo makuu yaliyojitokeza wakati Kardinali Gianfranco Ravasi Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka katika Mfuko wa Sterm For Life Foundation, kama sehemu ya Maandalizi ya Mkutano wa kimataifa unaojadili kuhusu viinitete ulioanza leo mjini Vatican na Kumalizika 13 Aprili 2013.

Tangu Mwaka 2011 wataalam wa masuala ya viinitete na maadili kutoka ndani ya Kanisa iliwabidi kupanua zaidi ufahamu wao kwa kuangalia juu ya: tafsiri, majiundo na usambazaji wa tafiti zinazofanywa kuhusiana na tiba ya mwanadamu, ili ziweze kueleweka na watu wa kawaida. Ni changamoto iliyotolewa na Monsinyo Tomasz Trafny, Kiongozi mwandamizi kutoka kitengo cha Baraza la Kipapa la Utamaduni, Imani na Sayansi. Tafiti hizi ziliweza kuchapwa katika kitabu na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, akapata nakala moja.

Mkutano wa Kimataifa kuhusu tiba ya viinitete kwa mwaka huu unalenga zaidi kutoa upembuzi yakinifu kuhusu: ushawishi, utegemezaji na ushirikiano; ili kujenga Jamii inayosimikwa katika ushawishi wa tafiti zinazozingatia maadili na utu wema; kwa kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba, tumboni mwa mama yake.

Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuungwa mkono na wadau mbali mbali wanaopania kuendeleza tafiti za kisayansi kwa muda mrefu katika masuala ya maadili ya kibayolojia na tafiti za kitamaduni.

Yote haya wanasema wawezeshaji wa mkutano huu kwamba, yamewasaidia kujenga na kuimaarisha utamduni wa majadiliano na ushirikiano katika ngazi mbali mbali: kwa kuanzia na Maajalim waliobobea katika fani hizi, taasisi za tafiti za kisayansi pamoja na vyuo vikuu kadhaa kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Wednesday, April 10, 2013

Tamko la Kundi la Glorious Celebration.

Wapendwa katika Bwana na wapenzi wote wa Glorious Celebration (GC), BWANA YESU ASIFIWE!
Kwanza kabisa tunamshukuru MUNGU wetu muumba mbingu na nchi kwa vile ambavyo amekuwa mwaninifu kwetu, kimblilio na nguvu nyakati zote za huduma na kuzidi kutupa kibali na kutusimamisha kama Walawi wa zama hizi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Hakika nafsi zetu hazitachoka kumhimidi Bwana wala kuzisahau fadhili zake zote. (Zaburi 103:2).

Pili, kwa niaba ya GC family nzima tunapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru ndugu wapendwa katika KRISTO YESU BWANA wetu na wapenzi wote wa GC kwa ujumla, kwa upendo, maombi na ushirikiano na saburi mliyoonyesha kwetu tangu kuanza kwa GC.
Wapendwa, kama mtume Paulo anaenavyo katika 1 Wakorintho 2:4, nasi pia tunajaribu kuongea pasipo maneno ya kuvutia na ya hekima sana, bali kwa uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho Mtakatifu kwa kusudi kwamba imani yenu ipate kutegemea nguvu ya MUNGU, na si hekima wala husuda za binadamu.

Ndugu wapendwa, kuna mambo kadhaa yamejitokeza hivi karibuni ndani ya GC, na hatimaye kupelekea baadhi ya wana GC kujiengua na kuanzisha kundi lingine linaloitwa Glorious Worship Team (GWT). Kama nilivyokwisha kusema hapo juu, hatutapenda sana kuzungumzia mgawanyiko huo katika namna ya kushambulia upande fulani, kwani tunafurahia zaidi kuzungumzia umoja na mshikamano uliopo ndani ya GC ili Kristo na azidi kutukuzwa. Hii ndio maana juzi tulipokuwa Radio Clouds FM 88.5, tulighairi kuzungumzia juu ya mgawanyiko huu tofauti na wengi mlivyoomba tufanye hivyo.

Mbeba maono na mwanzilishi wa GC, baba yetu Bishop Ayoub Mwakang’ata mara zote amesisitiza kuwa, kusudi kuu la huduma hii ni kuihubiri injili, na hivyo basi injili izidi kusonga mbele bila kumpa ibilisi nafasi. Wapendwa, GC tunafurahia kuwa vijana wenzetu waliolelewa GC leo wamekua na kujulikana na hata wameweza kuanzisha kundi lao, hivyo ni mtazamo na furaha yetu kuwa kazi ya MUNGU imepanuka.

Mgawanyiko huo ulipotokea GC ilitulia na kutafuta kujua nini kusudi la MUNGU. Hatimaye iliazimiwa kuongeza safu mpya kuungana na wana GC waliokataa kusaliti maono ya GC. Tangu Mwanzo hadi Ufunuo, siku zote MUNGU anao watu na siku zote anajisazia watu watakaomwangukia JEHOVAH no matter what! Hivyo, tulimwomba MUNGU na hatimaye akajiinulia vyombo vingine vilivyo tayari kuifanya kazi yake. Kisha tulienda kambini kwa wiki nzima ili kuutafuta uso wa Mungu, na kumwambia BWANA usitutenge na uso wako, wala ROHO WAKO MTAKATIFU, usituondolee (Zaburi 51:11). Tulipokuwa huko tulimling'ang'ania BWANA na hatukumwacha BWANA mpaka alipotubariki. 
BWANA alisema utukufu wa sasa hautakuwa kama ule wa kwanza. Baada ya hapo tukauona wigo mpana zaidi wa maono ya GC. Na kwa sasa GC ina timu kubwa zaidi. Mpaka sasa tayari ina waimbaji 24, yaani ukijumuisha WAPIGA VYOMBO, WAIMBAJI, AKAPELA, na DANCERS. Na makudi haya yatajumuika katika shughuli mbalimbali za injili. Yaani, uimbaji, huduma kwa wagonjwa waliotelekezwa mahospitalini, kutembelea yatima na baadaye wazee na wajane waliotelekezwa.

Tunamshukuru MUNGU, hatimaye juzi, Jumapili ya tarehe 07/04/2013 GC nzima iliwekwa wakfu tayari kwa kuanza kazi rasmi tena. (Matendo ya Mitume 1:8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi).

Neno moja ambalo tumelitaka kwa BWANA MWAKA HUU, HATUENDI KUIFANYA KAZI PEKE YETU, BALI TUNAKWENDA KUIFANYA KAZI PAMOJA NAYE. BILA NGUVU, KIBALI NA UWEPO WAKE KATIKATI YETU HATUTAENDA! (Kutoka 33:15). KILIO NA MAOMBI YETU NI KUIFANYA KAZI YA BWANA KUPITA WAKATI WOTE TULIOWAHI, TUNATAKA KUONA MUNGU AKIINULIWA TANZANIA, AFRIKA NA HATA MIISHO YA NCHI. (Yohana 12:32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.)
Wapendwa, GC ni maono kutoka kwa MUNGU. GC ilianzia madhabahuni, na hivyo MUNGU aliyeanziisha kazi hii ndani ya mtumishi wake ndiye atakayeitimiza.

GC iko tayari na kuanzia mwezi ujao tutaanza ziara za mikoani na kwingineko.

CEO, Glorious Celebration

Thursday, April 4, 2013

Mauaji ya Padri, DPP na Polisi Wakorogana.


Picture


MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, ametupilia mbali uchunguzi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na kusema mtuhumiwa hana kesi ya kujibu mahakamani.


Padri Mushi ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili aliuawa kwa kupigwa risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi mjini hapa akiwa ndani ya gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Theresia, mjini Zanzibar.

Baada ya mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha kukaribisha maafisa wa FBI kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa mauaji hayo na Machi 17, mwaka huu Jeshi la Polisi lilimkamata Omar Mussa Makame kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

Uchunguzi umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, DPP aliliandikia barua Jeshi la Polisi na kukabidhiwa juzi ikieleza sababu za ofisi yake kutofungua hati ya mashtaka hadi sasa dhidi ya mtuhumiwa wa mauaji hayo.

Jeshi la Polisi limethibitisha kuipokea barua ya DPP ambayo inaeleza kuwa ushahidi uliokusanywa katika jalada la kesi hiyo hauna mashiko na kwamba mtuhumiwa hahusiki na mauaji hayo.

Chanzo cha habari kutoka Jeshi la Polisi kilieleza kuwa DPP hajaridhishwa na uchunguzi wote uliokusanywa dhidi ya mtuhumiwa pamoja na watuhumiwa watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya askari polisi, Said Abdulrahman aliyeuawa kwa kupigwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar Oktoba 17, mwaka jana.

Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alithibitisha hatua ya DPP kutupa uchunguzi wote wa jalada la mauaji ya Padri Mushi na kuwataka waandishi wa habari kumtafuta DPP azungumzie sababu za uamuzi wake wa kutokubaliana na uchunguzi wa Polisi.

Hata hivyo, alisema kwamba Jeshi la Polisi bado linaamini uchunguzi walioufanya kwa kushirikiana na FBI hauna shaka na kwamba mtuhumiwa huyo ana kesi ya kujibu mahakamani na wataendelea kumshikilia.
Alisema kwamba kwa mujibu wa sheria, Jeshi la Polisi jukumu lake ni kuchunguza kesi na ofisi ya DPP jukumu lake ni kufungua hati ya mashtaka na kutetea kesi mahakamani.

Hata hivyo, Mwandishi wa habari hii alipofika katika ofisi ya DPP, Katibu muhtasi wake alisema amepokea maagizo kutoka kwa bosi wake kuwa waandishi wote wa habari wanaofuatilia suala hilo, wamuone Kamishna wa Polisi kwa vile kazi aliyopewa ya kupitia jalada la uchunguzi kabla ya kufungua kesi ameikamilisha.

“Kamishna ndiye aliyeitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea hatua iliyofikiwa pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa, sasa awaite tena amalizie kazi yake ya kuwaeleza hatua iliyofikiwa baada ya Mkurugenzi kurejesha jalada la mauaji,” alisema Katibu muhtasi huyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Yusuph Ilembo, jana alifika katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, kufuatia ombi lililofunguliwa mahakamani na wakili anayemtetea mtuhumiwa wa mauaji, Abdallah Juma Mohamed.

Abdallah Juma amefungua ombi katika Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu cha sheria 390 cha sheria namba 7 ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004, akitaka Jeshi la Polisi litoe maelezo kwa nini mteja wake hajafikishwa mahakamani ndani ya saa 24 tangu alipokamatwa Machi 17, mwaka huu.

Wakili Abdallah Juma akisaidiwa na mawakili Shaban Juma Bakari na Shaibu Ibrahim Shaibu waliitaka Mahakama Kuu itoe amri ya kuachiwa kwa mteja wao kutoka mikononi mwa Jeshi la Polisi. Hata hivyo, Ilembo alisema kuwa kutokana na uzito wa kesi hiyo, anaomba kupewa muda wa kutayarisha majibu ya hati ya kiapo kwa maandishi na kuuwasilisha kwa upande wa utetezi na mbele ya mahakama hiyo kabla ya ombi hilo kuanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

“Tunaomba mtuhumiwa aendelee kushikiliwa na Polisi, wakati tukifanya matayarisho ya kujibu hati ya kiapo,” alisema Ilembo.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema baada ya kusikiliza pande zote mbili, alimtaka Ilembo awe amejibu kwa maandishi hati ya kiapo ya maombi hayo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo Aprili 8, mwaka huu.

Aidha, Jaji alisema wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, ametaka mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani, baada ya hoja za upande wa mawakili wanaomtetea kutaka dhamana kwa mteja wao, kwa vile bado hajafikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.

Kutupwa kwa uchunguzi wa jalada la mauaji hayo pamoja na jalada la uchunguzi wa mauaji ya Polisi kunadhihirisha kuwapo kwa mvutano mkubwa baina ya Jeshi la Polisi Zanzibar na ofisi ya DPP.

Chanzo: Nipashe

Wednesday, April 3, 2013

Mgogoro wa Uchinjaji nyama waibuka Tunduma Mbeya.

MGOGORO mkubwa umeibuka kuanzia asubuhi siku ya leo jijini Mbeya wilayani Tunduma ukihusisha suala la uchinjaji wa nyama kwa ajili ya kitoweo, baina ya wakristo na waislam kwenye machinjio ya ng'ombe wilayani Tunduma.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari kilichopo eneo la tukio kimeeleza kuwa Vurugu hizo zimekuja baada ya tamko alilolitoa Mkuu wa mkoa wa Mbeya siku moja kabla ,mh.Abas Kandoro tamko lililoruhusu siku ya leo shughuli za uchinjaji wa nyama kwa ajili ya kitoweo katika machinjio mkoani hapo zifanywe na wakristo.

Sintofaham iliibuka siku ya leo ambapo Wakristo waliamkia kwenye machinjio wakiwa wamejiandaa kwa shughuli za uchinjaji rasmi,lakini kinyume na matarajio yao ghafla walipokelewa na Askari wa kutuliza Ghasia FFU wakiwa eneo la tukio kuzuia wakristo kuingia kwenye machinjio kwa kile kilichoelezwa kuwa wamepewa amri hiyo toka kwa mkuu wa wilaya ya Tunduma.

Baada ya zuio hilo ndipo Utaratibu wa siku zote ukafanyika ambapo waislam wakaendelea na shughuli ya uchinjaji chini ya ulinzi wa FFU na baada ya kumaliza kuchinja nyama zote ndipo FFU wakaondoka.

Kufuatia kitendo hicho wakristo walijawa na jazba na ndipo yalipoibuka maandamano makubwa barabarani yaliohusisha uchomaji wa matairi kupinga kitendo hicho kilichotokea siku ya leo.



 

SOURCE: Mjap Inc 

Monday, April 1, 2013

Waumini wakaguliwa kabla ya kuingia ibadani.

KATIKA hali isiyo ya kawaida Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, juzi liliimarisha ulinzi kwa kila aliyeiingia kukaguliwa na walinzi kwa kutumia machine maalumu ya utambuzi wa vitu vya hatari.

Ukaguzi huo ulifanyika kwenye lango la geti kuu kabla ya kuingia ndani ya kanisa hilo kwa ibada ya mkesha wa sikukuu ya Pasaka ukihusisha Waumini, Watawa, Mapadri, Askofu na watumishi wengine wa kanisa kabla ya kuanza kwa ibada. 

Walinzi wa kampuni binafsi walionekana wakiendelea na kazi hiyo kuhakikisha kila anayeingia kanisani humo haingii na silaha yoyote ambayo ni tishio kwa usalama wa kanisa na waumini wake.

Hatua hiyo imekuja kukiwa tayari kumetokea matukio ya kuchomwa moto makanisa, kuibwa mali za kanisa, na hujuma nyinginezo kwa makanisa maeneo ya Zanzibar na Dar es Salaam na kushambuliwa na kuuwawa kwa viongozi wa kanisa.

Wakizungumzia hatua hiyo, baadhi ya waumini, Neema John na Joseph Mwaipopo, walisema kwa kiasi fulani inashangaza lakini kwa kujiridhisha kwenye suala la ulinzi ni vyema likawa zoezi endelevu hasa ikizingatiwa hali tete iliyopo dhidi ya makanisa.

"Hatukuwahi kufikiri wakristo tutafikia hatua hii ya kutoaminina, tuliabudu kwa wazi bila hofu yoyote, kwa imani za dini zetu Watanzania tunapaswa kumuomba Mungu lulu ya amani tulioyonayo isitoweke," alisema Mwaipopo.

Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Polcarp Kadinali Pengo, aliwataka waumini waliobatizwa kwa siku hiyo na wengine kusisimama kwenye imani yao kuwa mfano mzuri kwa wanajamii wengine.

Chanzo: Nipashe