MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim,
ametupilia mbali uchunguzi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa
na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Upelelezi
la Marekani (FBI) na kusema mtuhumiwa hana kesi ya kujibu mahakamani.
Padri Mushi ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili
aliuawa kwa kupigwa risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi
mjini hapa akiwa ndani ya gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya
Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Theresia, mjini Zanzibar.
Baada ya mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha kukaribisha maafisa wa FBI kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa mauaji hayo na Machi 17, mwaka huu Jeshi la Polisi lilimkamata Omar Mussa Makame kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Uchunguzi umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, DPP aliliandikia barua Jeshi la Polisi na kukabidhiwa juzi ikieleza sababu za ofisi yake kutofungua hati ya mashtaka hadi sasa dhidi ya mtuhumiwa wa mauaji hayo.
Jeshi la Polisi limethibitisha kuipokea barua ya DPP ambayo inaeleza kuwa ushahidi uliokusanywa katika jalada la kesi hiyo hauna mashiko na kwamba mtuhumiwa hahusiki na mauaji hayo.
Chanzo cha habari kutoka Jeshi la Polisi kilieleza kuwa DPP hajaridhishwa na uchunguzi wote uliokusanywa dhidi ya mtuhumiwa pamoja na watuhumiwa watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya askari polisi, Said Abdulrahman aliyeuawa kwa kupigwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar Oktoba 17, mwaka jana.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alithibitisha hatua ya DPP kutupa uchunguzi wote wa jalada la mauaji ya Padri Mushi na kuwataka waandishi wa habari kumtafuta DPP azungumzie sababu za uamuzi wake wa kutokubaliana na uchunguzi wa Polisi.
Hata hivyo, alisema kwamba Jeshi la Polisi bado linaamini uchunguzi walioufanya kwa kushirikiana na FBI hauna shaka na kwamba mtuhumiwa huyo ana kesi ya kujibu mahakamani na wataendelea kumshikilia.
Alisema kwamba kwa mujibu wa sheria, Jeshi la Polisi jukumu lake ni
kuchunguza kesi na ofisi ya DPP jukumu lake ni kufungua hati ya
mashtaka na kutetea kesi mahakamani.
Hata hivyo, Mwandishi wa habari hii alipofika katika ofisi ya DPP, Katibu muhtasi wake alisema amepokea maagizo kutoka kwa bosi wake kuwa waandishi wote wa habari wanaofuatilia suala hilo, wamuone Kamishna wa Polisi kwa vile kazi aliyopewa ya kupitia jalada la uchunguzi kabla ya kufungua kesi ameikamilisha.
“Kamishna ndiye aliyeitisha mkutano na waandishi wa habari kuelezea hatua iliyofikiwa pamoja na kukamatwa kwa mtuhumiwa, sasa awaite tena amalizie kazi yake ya kuwaeleza hatua iliyofikiwa baada ya Mkurugenzi kurejesha jalada la mauaji,” alisema Katibu muhtasi huyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Yusuph Ilembo, jana alifika katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, kufuatia ombi lililofunguliwa mahakamani na wakili anayemtetea mtuhumiwa wa mauaji, Abdallah Juma Mohamed.
Abdallah Juma amefungua ombi katika Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu cha sheria 390 cha sheria namba 7 ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004, akitaka Jeshi la Polisi litoe maelezo kwa nini mteja wake hajafikishwa mahakamani ndani ya saa 24 tangu alipokamatwa Machi 17, mwaka huu.
Wakili Abdallah Juma akisaidiwa na mawakili Shaban Juma Bakari na Shaibu Ibrahim Shaibu waliitaka Mahakama Kuu itoe amri ya kuachiwa kwa mteja wao kutoka mikononi mwa Jeshi la Polisi. Hata hivyo, Ilembo alisema kuwa kutokana na uzito wa kesi hiyo, anaomba kupewa muda wa kutayarisha majibu ya hati ya kiapo kwa maandishi na kuuwasilisha kwa upande wa utetezi na mbele ya mahakama hiyo kabla ya ombi hilo kuanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
“Tunaomba mtuhumiwa aendelee kushikiliwa na Polisi, wakati tukifanya matayarisho ya kujibu hati ya kiapo,” alisema Ilembo.
Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema baada ya kusikiliza pande zote mbili, alimtaka Ilembo awe amejibu kwa maandishi hati ya kiapo ya maombi hayo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo Aprili 8, mwaka huu.
Aidha, Jaji alisema wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo, ametaka mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani, baada ya hoja za upande wa mawakili wanaomtetea kutaka dhamana kwa mteja wao, kwa vile bado hajafikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.
Kutupwa kwa uchunguzi wa jalada la mauaji hayo pamoja na jalada la uchunguzi wa mauaji ya Polisi kunadhihirisha kuwapo kwa mvutano mkubwa baina ya Jeshi la Polisi Zanzibar na ofisi ya DPP.
Chanzo: Nipashe