WAZIRI Mkuu mstaafu
Edward Lowassa amesema kuwa mbali
ya kuwa
yeye si tajiri ila bado
ataendelea kufanya kazi yake kwa
ukaribu zaidi na jamii ikiwa ni pamoja na kushirikiana na marafiki
zake kusaidia na kuwataka wale
wote wenye kusema dhidi yake kuendelea
kusema ila hatarudi nyuma katika
kutoa misaada kama njia ya kutafuta baraka
za Mungu.
Lowasa ambae pia
alikabidhiwa tuzo ya heshima kwa ajili ya kuendeleza
kulipigania Taifa la Tanzania, huku mwenyewe akichangia kiasi cha Tsh milioni
15 na mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe akichangia milioni 9
kati ya fedha
zote zaidi ya Tsh milioni 75
zilizochangwa kwa ajili ya kuendeleza
ujenzi wa kanisa la OPC mkoani Iringa
kama njia ya kuhamasisha amani katika
Taifa ametaka watanzania kuwapuuza
wale wote wanaoeneza siasa za uchochezi .
“Nataka kuwaomba leo wachukieni wachochezi na pia niwaelezeni kuwa mimi si tajiri ila nina utajiri wa
watu na ushawishi na ninafanya
mambo haya ili kumbukumbu yangu
iweze kuandikwa Mbinguni na nimekuwa
nikialika watu wengi na nimekuwa nikifika wacha wenye kusema waseme watasema ila usiku watalala wenyewe ....sitaacha kusaidia kwa kuogopa kusemwa”
Akizungumza katika hafla
hiyo iliyoandaliwa na kituo cha maombezi na uponyaji mkoani Iringa
Overcomers Power Center (OPC) na
kufanyika katika ukumbi wa St Dominic mjini Iringa leo Lowassa
alisema kuwa yeye si tajiri kama
ambavyo watu wanavyofikiri ila amekuwa akipewa nguvu na rafiki zake ambao
wamekuwa wakimuunga mkono pindi
anapoalikwa katika hafla mbali mbali.
“Nataka kwanza kuwashukuru
ndugu zangu wa mkoa wa Iringa na napenda kumshukuru
zaidi Askofu Dkt Boaz Sollo kwa
kunialika mkoani Iringa …..ila
napenda kuwaeleza kuwa
si kwamba nachangia michango mbali mbali katika jamii kama mimi ni
tajiri ila mimi ni mtumishi nisiye na
faida na nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu Pia nawashukuru
sana wabunge wenzangu ambao wamepata
kushiriki name leo katika ziara
hiyo akiwemo mbunge machachari bungeni Deo
Filikunjombe, Kagi Lugola na
dada yangu Ritta Kabati bila kumsahau mbunge Mendradi Kigola kwa
kuungana nami leo naamini nao
wamepanda mbegu bora”.
Lowassa alisema kuwa
anatambua bado ana mialiko migi sana na lazima ataifanyia kazi mialiko yote
kama ambavyo jamii imepata kumwalika na
kuwa hata hatua ya mkoa
wa Iringa kumpa tuzo
hainamanishi kuwa ni mwisho wa yeye
kualikwa.
Hata hivyo Lowassa
alisema kuwa kwa upande
wake anapongeza jitihada za Askofu Dkt Sollo kwa kuwa na mipango na mitazamo ya kulisaidia
Taifa kwa kuanzisha ujenzi
wa kanisa kwa ajili ya kudumisha
amani na kwenda mbali zaidi kwa
kuanzisha kituo cha radio
Overcomers Fm chombo ambacho kitatumika
kudumisha amani ya mkoa wa Iringa na Taifa pia
Kuhusu amani ya Taifa
la Tanzania Lowassa alisema kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu walioalikwa Kenya katika sherehe ya kuapishwa Rais mpya wa Kenya Uhuru Kenyatta ila sehemu kubwa ya wote
waliotoa salam zao walitumia muda mwingi kupongeza vyombo vya habari kwa kulinda amani na
hivyo kuvitaka vyombo
vya habari za Tanzania na wanahabari
kuendelea kuandika habari bila
kuhatarisha amani ya Taifa
“Tusiruhusi amani ya nchi
yetu iyumbishwe na mtu awaye
yeyote na kila mtanzania
anapaswa kulinda amani hii
kwa nguvu zote ….Nawaombeni wanahabari
tunzeni amani yetu…wapuuzeni wale
wote wanaoch0chea machafuko
katika Taifa hili ….tuachane na udini
wala ukabila katika taifa letu"
Katika hatua nyingine
Lowassa aliwapongeza wabunge wa CCM ambao wameendelea
kupigania wanyonge bungeni
akiwemo Deo Filikunjombe mbunge wa
Ludewa na mbunge wa jimbo la Mwibara Kagi Lugola kuwa ni miongoni mwa wabunge ambao amekuwa akiwapenda kutokana na kusema ukweli bungeni.
Kwa upande wake
mbunge Filikunjombe alisema kuwa mbali
ya kutoa ahadi ya kuchangia kiasi cha Tsh milioni 9 ila bado
atamwalika Lowassa jimboni kwake
Ludewa na kuwa kanisa hilo la OPC
halijakosea kumpa tuzo ambayo ni ramani ya
Tanzania kutokana na Lowassa kuwa ni mtu
wa watu mpendwa na watu na kuwa tuzo hiyo ina maana kubwa na hawajakupa ramani ya
jimboni kwako Monduli.
Filikunjombe alimtaka Lowassa
kuendelea kuchapa kazi na kuwa hajakosea kuwaalika
wao kwani bungeni kuna wabunge
zaidi ya 300 ila amewachagua
wao pekee, hivyo ni jambo la kumshukuru na
kumfananisha Lowassa na mti unaopigwa mawe kuwa ni mti wenye matunda.
“Nakuomba Lowassa simama
Imara sisi wana Iringa
tupo nyuma yako na niseme tuna
kazi kubwa ya kuifanya katika Taifa hili
kubwa ni kumwomba Mungu na makanisa na
dini zote kuungana katika maombi zaidi kwani
vita ni kubwa mbele “
Kwa upande Askofu
Dkt Sollo mbali ya
kumpongeza Lowassa bado alisema
kuwa wao kama kanisa wataendelea kumwombea
afya njema na kuona kuwa mambo yake yanafanikiwa na ndio maana ya
kumpa tuzo hiyo
ya heshima.
Sollo alisema kuwa mchango
wa TSh milioni 15 ulioahidiwa na
Lowassa na ule wa milioni 9 ulioahidiwa na mbunge wa jimbo la Ludewa
Deo Filikunjombe ni mchango ambao wao wanaupongeza na kuwapongeza wabunge
wengine akiwemo Ritta Kabati aliyeahidi Tsh milioni 2 ,Benki ya wananchi Mufindi milioni 2 , mwenyekiti wa CCM mkoa
wa Iringa Jesca Msambatavangu milioni 2
mfanyabiashara Salim Abri milioni
1 na wengine wengi ambao wamepelekea
kupata zaidi ya Tsh milioni zaidi
ya 75 pesa taslim na ahadi.
Chanzo: Francis Godwin