Advertise Here

Thursday, April 11, 2013

Spacio: Mwimbaji wa Nyimbo za Injili aliyeishi na Jini Mahaba kwa Miaka 17.

Kwa jina naitwa Spacio Abubakary Ngalla, nimezaliwa na kukulia Dar es salaam, Sinza. Na ni mtoto wa 3 katika familia ya kiislamu.

Kiukweli mimi nilikuwa mmoja wa watu ambao hawakutaka kusikia Jina la YESU na nilikuwa siamini miujiza yeyote na kuona ni mazingaombo tu wachungaji wanafanya kuwateka watu akili. Ila hadi siku ambayo mungu aliponionesha njia ya uzima na kuniponya tatizo lililonisumbua mda mrefu, ndipo nikaamini uwepo wa UKRISTO

NILIVYOKUTANA NA JINI MAHABA
Nakumbuka ilikuwa mwaka 1996, nikiwa na miaka 7, Mimi na marafiki zangu tulikuwa na tabia ya kwenda kuogelea coco beach siku za weekend, siku moja baada ya kumaliza kazi zangu za nyumbani majira ya saa 6 hivi nikaenda kuwapitia marafiki zangu (4) ili twende beach kuogelea ikifika jioni turudi nyumbani. Tulipofika beach watu walikuwa ni wengi sana kila mmoja alikuwa yupo busy na yake, sisi tulijigawa wengine walienda kuogelea sehemu nyingine, mimi na mwenzangu Ali tulibaki upande wa mwanzoni kwa kuwa hatukuwa tunajua kuogelea vizuri.

Majira ya saa 10, hivi nikiwa na Ali, nilisikia harufu nzuri kweli ikiwa inavuma kuja kwetu, ambayo siku wahi kuisikia kabla, ni nzuri kwa kweli, nikamuuliza Ali “unaisikia harufu hii?” yeye akajibu ndio ninaisikia ila sijui inatoka wapi!

Baada ya dakika kadhaa nilisikia sauti ya kike ikinisalimia “hujambo?” nikashtuka, kugeuka nyuma nikakutana na msichana sijui nimuelezeeje, ni mweupe kiasi, ana nywele ndefu, sura yake ipo serious na ukiiangalia tena ni kama anatabasamu, macho yake ni ang’avu, ni mzuri kiufupi akiwa amevaa nguo za kawaida tu ila kichwani amejitanda baibui. Aliniambia jina anaitwa MAIMUNA!

Mwili uninisisimka huku kidogo nikiwa na natetemeka japo sikutaka kumuonesha kwa kuwa hilo jina halikuwa geni kwangu, cha ajabu kadri alivyokuwa anaongea na mimi uoga ulizidi kunipungua hadi nikawa najiskia kawada na kucheka pamoja. Aliomba tuogelee wote nikamwambia, mimi siwezi kuogolea vizuri, akaniambia “Usiwe na wasi wasi nitakufundisha usijali” basi akaanza kunishika mikono na kuanza kunivuta ili niweze kujifunza kupiga mbizi taratibu. Siku hiyo ilikuwa ni tofauti sana kwani tulifurahi sana.

Saa 12 na nusu jioni ilipofika tukaanza kujiandaa kwa safari, siku hiyo tulichelewa kweli kuondoka! Ghafla Maimuna nikawa simuoni, nikaita sana “Maimunaaaaa uko wapi sisi tunataka kuondokaaaaa!” Kimyaa! Basi  sisi tukaanza kuondoka pale beach, kuna sehemu huwa ina miti mingi sana na ni shortcut kwenda kituoni, kwa mchana ni salama lakini kama ni giza giza si pazuri huwa kunakuwa na wahuni. Sisi tukiwa tunakaribia hiyo njia roho ilisita kupita pale, kumbe nyuma kulikua na wahuni wakitufatilia. Na sisi tupo watato tu, wao walikuwa watatu.

Heee mara tukashangaa kundi la watu zaidi ya 15 nao wakawa wanapita hiyo hiyo njia, basi sisi tukaongozana nao hadi kupita ile njia salama, kushtuka tunajiona tupo wa tano tu mbele tunakajiuliza “wale watu wameenda wapi?” Wahuni kumbe walikimbia katikati! sasa hatukujua ni kwa kwa sababu gani. Ila mimi nikahisi kundi la watu wale hawakuwa watu bali ni majini ndo waliotusindikiza, nikawaambia wenzangu “jamani tukimbie wale ni majini” kwa sauti kubwa ya uoga”.


URAFIKI NA JINI MAIMUNA
Tukafika nyumbani kila mmoja hoi, mimi bado nilikuwa na mawazo ya yule msichana niliyekutana nae baharini. Usiku nikiwa ndotoni nilimuota akija kunitembelea nyumbani na kufurahi pamoja.

Hali ile iliendelea hadi nafika form 1, ambapo nilikuwa nasoma Azania Sec School, haipiti siku moja lazima niote tuko pamoja tunafurahi pamoja hadi nikazoea,

Mwaka 2004, Maimuna alijitokeza tena kwa mara ya pili nikiwa niko chumbani, niliogopa sana nilipiga kelele mama akaja Maimuna akaondoka. Mama alishushwa sana na hali hiyo akaniuliza tatizo ni nini lakini nikamwambia nilikuwa naota tu, niliogopa kusema kwa kuwa Maimuna aliniambia nisiseme chochote kuhusu yeye la sisivyo nitakiona cha moto.

Baada ya muda nikazoea, akija tunaongea tu vizuri na kazi zingine alikuwa ananisaidia kama kutengeneza computer za baba, alikuwa ananisaidia kama tatizo ni kubwa sana namwita kimoyo moyo anakuja ktk mwili wangu kisha naanza kutengeneza computer, watu wengi walinishangaa sana uwezo niliokuwa nao lakini kumbe walikuwa hawajui JINI ndie alikuwa mara nyingi ananifundisha usiku.

Alinipa hela nyingi tu kiasi kwamba nilikuwa naenda shule nikiwa elfu 50, laki, ILA ole wangu nitumie na mwanamke au nimnunulie mtu sigara, pombe, basi hela zote zinapotea na nitahangaika hata shilingi 100 sipati zaidi ya kupewa hela ya shule, na nitahangaika hadi basi.

KAMA kawaida ukisha fikia umri fulani lazima uanze utundu wa kufatilia wasichana, kuwapa hela au kuwanunulia zawadi hasa katika siku kuu vile au valentine day, mimi iliponza sana hiyo tabia, kwani niliteseka sana.Kwani maimuna alikuwa hapendi

Kitu kilichonifanya nitafute wasichana wengine ni kwamba Maimuna hakuwa anakuja kila wakati, ni mara moja tu kwa siku tena hasa usiku. Na pia ukiangalia hata nikija kukua yeye anabaki jini na mimi binadamu kwa hiyo si rahisi kuja kuishi pamoja.

ILA chochote kilichokuwa kibaya kwangu kilichotegeshwa kichawi hakikuweza kunipata na hata usiku wachawi hawakuweza kunifata fata, japo mwanzoni nilihangaika sana na wachawi kwani walikuwa wanatusumbua sana nyumbani, waganga walidai nyumba haikuwa na zindiko!

Kiukweli alinifundisha vitu vingi pamoja na uchoraji, utayarishaji muziki, computer ambavyo hadi sasa vinanisaidia ktk maisha yangu, baada ya kutoka darasani yeye hunifuata usiku na kunielekeza zaidi. MIAKA YOTE HIYO TULIISHI KAMA WACHUMBA.Mengine siwezi kuyataja lakini mtakuwa mshaelewa nini ninamaanisha.


UGOMVI NA JINI KUANZA
Mwaka 2009, nina miaka 20 nikiwa nafanya kazi Cellulant Tanzania, kuna dada mmoja alikosea namba na kupiga kwangu, alijitambulisha kwa jina anaiwa UPENDO, mara ndio ukawa mwanzo wa urafiki wetu ambae hadi sasa tunaishi pamoja tukijipanga kwa ajili ya kufunga ndoa. Nilitokea kumpenda sana dada huyo japo hatukuwa tumeonana, na hata yeye pia alitokea kupenda kuongea na mimi mda wote. Maimuna alikuwa hapendi tabia ya mimi kuongea na huyo dada na mara nyingi alikuwa ananionya sana, ila mimi ilikuwa vigumu mno kukubali kwani nilikuwa nimshapenda tayari.

Siku moja nikasema hataa lazima nionane na huyu dada, hadi lini tutaishia kuongea kwa simu tu. Kwa mara ya kwanza kukutana na dada huyo, usiku wake sikulala! Nilipatwa na homa hadi asubuhi yake sikuweza kwenda kazini ikabidi nipumzike. Mara mwili unachoma, mara kifua kinanibana, mara kichwa kinaniuma, kikitulia nyama za mwili zinatikisika kama mtu anani vibrate vile.Niliteseka sana wiki nzima nilkuwa mgonjwa. Maimuna akaniambia hiyo ni bakora moja nimekupa, nataka uachane na UPENDO.

Baada ya kuseka sana kwa hali hiyo kwani mara kwa mara ilikuwa inanitokea, nikaanza kwenda kwa waganga kutafuta tiba ya kumuondoa jini huyo katika mwili wangu,kwani alikuwa kero kwangu, zaidi ya waganga 15 nilikwenda lakini bila mafanikio.


                                                    KUOKOKA KWANGU
Baada ya kuchoka kuvumilia nikamfuata rafiki yangu wa karibu Robert na kuanza kumueleza,  akaniambia kwanini usiende kuombewa, mbona wengi tu wanapona na hata mjomba wangu alikuwa anaumwa miguu alipoombea akapona. Nikamwambia sasa nikienda huko wazazi wangu waanifikiriaje? Akanijaza moyo na kunipa ujarisi kuwa “IMANI YAKO NA MUNGU SI YA WAZAZI WAKO BALI NI WEWE NA MUNGU WAKO NA HATA UKIFA UTAENDA NAO? SI WEWE NDIE UTAKAYE ENDA KUJIBU HUKO? FANYA MAAMUZI YALIYO SAHIHI”

Nikakubali! Basi nikasubiri jumapili ilipofika nikajiandaa na kwenda kanisani kuombewa, hakika nilipoombewa kila kitu kili badilika na kijisikia mwepesi kama vile nilikuwa nimebeba viroba vya michanga! Nilipoombewa nikadondoka chini na kupoteza fahamu. Baada ya dakika kadhaa nikaamka na kujikuta nikochini nimelala huku nikijishangaa nini kilichotokea.

Toka hapo nikaamini na nikaamua kuimba Nyimbo za Injili ili kueneza Neno la Mungu kwa wasiofahamu utamu wake.

Kwasasa nipo huru na ni kweli Yesu anatenda na Roho Mtakatifu yupo kwa ajili yako endapo utaamua kumpokea! Mungu ni mwema, Mungu anatenda. NAMSHUKURU KWA KUNIOKOA!