Advertise Here

Wednesday, April 10, 2013

Tamko la Kundi la Glorious Celebration.

Wapendwa katika Bwana na wapenzi wote wa Glorious Celebration (GC), BWANA YESU ASIFIWE!
Kwanza kabisa tunamshukuru MUNGU wetu muumba mbingu na nchi kwa vile ambavyo amekuwa mwaninifu kwetu, kimblilio na nguvu nyakati zote za huduma na kuzidi kutupa kibali na kutusimamisha kama Walawi wa zama hizi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Hakika nafsi zetu hazitachoka kumhimidi Bwana wala kuzisahau fadhili zake zote. (Zaburi 103:2).

Pili, kwa niaba ya GC family nzima tunapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru ndugu wapendwa katika KRISTO YESU BWANA wetu na wapenzi wote wa GC kwa ujumla, kwa upendo, maombi na ushirikiano na saburi mliyoonyesha kwetu tangu kuanza kwa GC.
Wapendwa, kama mtume Paulo anaenavyo katika 1 Wakorintho 2:4, nasi pia tunajaribu kuongea pasipo maneno ya kuvutia na ya hekima sana, bali kwa uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho Mtakatifu kwa kusudi kwamba imani yenu ipate kutegemea nguvu ya MUNGU, na si hekima wala husuda za binadamu.

Ndugu wapendwa, kuna mambo kadhaa yamejitokeza hivi karibuni ndani ya GC, na hatimaye kupelekea baadhi ya wana GC kujiengua na kuanzisha kundi lingine linaloitwa Glorious Worship Team (GWT). Kama nilivyokwisha kusema hapo juu, hatutapenda sana kuzungumzia mgawanyiko huo katika namna ya kushambulia upande fulani, kwani tunafurahia zaidi kuzungumzia umoja na mshikamano uliopo ndani ya GC ili Kristo na azidi kutukuzwa. Hii ndio maana juzi tulipokuwa Radio Clouds FM 88.5, tulighairi kuzungumzia juu ya mgawanyiko huu tofauti na wengi mlivyoomba tufanye hivyo.

Mbeba maono na mwanzilishi wa GC, baba yetu Bishop Ayoub Mwakang’ata mara zote amesisitiza kuwa, kusudi kuu la huduma hii ni kuihubiri injili, na hivyo basi injili izidi kusonga mbele bila kumpa ibilisi nafasi. Wapendwa, GC tunafurahia kuwa vijana wenzetu waliolelewa GC leo wamekua na kujulikana na hata wameweza kuanzisha kundi lao, hivyo ni mtazamo na furaha yetu kuwa kazi ya MUNGU imepanuka.

Mgawanyiko huo ulipotokea GC ilitulia na kutafuta kujua nini kusudi la MUNGU. Hatimaye iliazimiwa kuongeza safu mpya kuungana na wana GC waliokataa kusaliti maono ya GC. Tangu Mwanzo hadi Ufunuo, siku zote MUNGU anao watu na siku zote anajisazia watu watakaomwangukia JEHOVAH no matter what! Hivyo, tulimwomba MUNGU na hatimaye akajiinulia vyombo vingine vilivyo tayari kuifanya kazi yake. Kisha tulienda kambini kwa wiki nzima ili kuutafuta uso wa Mungu, na kumwambia BWANA usitutenge na uso wako, wala ROHO WAKO MTAKATIFU, usituondolee (Zaburi 51:11). Tulipokuwa huko tulimling'ang'ania BWANA na hatukumwacha BWANA mpaka alipotubariki. 
BWANA alisema utukufu wa sasa hautakuwa kama ule wa kwanza. Baada ya hapo tukauona wigo mpana zaidi wa maono ya GC. Na kwa sasa GC ina timu kubwa zaidi. Mpaka sasa tayari ina waimbaji 24, yaani ukijumuisha WAPIGA VYOMBO, WAIMBAJI, AKAPELA, na DANCERS. Na makudi haya yatajumuika katika shughuli mbalimbali za injili. Yaani, uimbaji, huduma kwa wagonjwa waliotelekezwa mahospitalini, kutembelea yatima na baadaye wazee na wajane waliotelekezwa.

Tunamshukuru MUNGU, hatimaye juzi, Jumapili ya tarehe 07/04/2013 GC nzima iliwekwa wakfu tayari kwa kuanza kazi rasmi tena. (Matendo ya Mitume 1:8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi).

Neno moja ambalo tumelitaka kwa BWANA MWAKA HUU, HATUENDI KUIFANYA KAZI PEKE YETU, BALI TUNAKWENDA KUIFANYA KAZI PAMOJA NAYE. BILA NGUVU, KIBALI NA UWEPO WAKE KATIKATI YETU HATUTAENDA! (Kutoka 33:15). KILIO NA MAOMBI YETU NI KUIFANYA KAZI YA BWANA KUPITA WAKATI WOTE TULIOWAHI, TUNATAKA KUONA MUNGU AKIINULIWA TANZANIA, AFRIKA NA HATA MIISHO YA NCHI. (Yohana 12:32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.)
Wapendwa, GC ni maono kutoka kwa MUNGU. GC ilianzia madhabahuni, na hivyo MUNGU aliyeanziisha kazi hii ndani ya mtumishi wake ndiye atakayeitimiza.

GC iko tayari na kuanzia mwezi ujao tutaanza ziara za mikoani na kwingineko.

CEO, Glorious Celebration