Advertise Here

Friday, May 31, 2013

Mfahamu kiundani Mwimbaji wa Nyimbo za Injili Sam Batenzi.

SAM 1
Samwel Batenzi maarufu sana kwa jina la Sam Batenzi, ni Mwimbaji Chipukizi wa Nyimbo za Injili anayekuja kwa kasi ya Ajabu katika tasnia ya Muziki wa Injili Tanzania, kutokana na Uimbaji wake un avyowabariki watu wa Mungu. Kwa mara ya Kwanza, nilikutana na Sam Jijini Mwanza katika kituo cha Kazi yaani HHC ALIVE FM (91.9Mhz), na ndipo hapo nilipopata shauku ya Kumfahamu zaidi.

HISTORIA YAKE KIMAISHA
Sam alizaliwa miaka 25 iliyopita katika Mkoa wa Mwanza, katika familia ya kikuhani ya Bishop David Batenzi na Mama Batenzi. Sam ni mtoto wa 3 kati ya watoto 4 wa Askofu Batenzi, na kabila lake ni Mnyamwezi kwa Upande wa Baba, na Msukuma kwa Upande wa Mama.
 

                            HISTORIA YAKE KIMUZIKI
Sam alianza kujishughulisha na Maswala ya Kimuziki Mwaka 2000, lakini katika kujifunza vyombo vya Muziki huko Mkoani Mwanza. Na alianza rasmi uimbaji Mwaka 2004 huko Tabora katika shule moja iliyojulikana kama Umoja Secondary School.

Nilipotaka kufahamu ni Kwanini aliamua kuimba Muziki wa Injili na Si aina Nyingine ya Muziki, Sam alisema; “Nimeamua kumtumikia Mungu katika Uimbaji wa Muziki wa Injili kwa sababu Muziki wa Injili ndio muziki ambao umekuwa ukigusa maisha yangu kwa aina moja au nyingine, lakini naweza sema pia nilizaliwa katika familia ya kikristo na kukulia katika Malezi ya Kikristo.Na pia nilipompokea kristo kama mwokozi wa maisha yangu, ndipo nilipogundua nini Mungu amenizawadia, nami nikatumia zawadi hiyo kufanya kazi yake.”
 

Vipi kuhusu vikundi/kwaya ambazo Sam ameimbia?
Hapa Sam anasema; “Nilipokuwa shule niliimbia kikundi kimoja kilijulikana kama LPP (Long Pray Praise) ambacho naweza sema ndo waliendeleza kile Mungu ameweka ndani yangu, lakina pia nimewahi imbia Dar es Salaam Gospel Choir DGC ya Dar, na nimewahi kuwa member kwa muda katika kundi moja la kusifu na kuabudu linajulikana kama New Wine la Dar.
 


Nini ambacho Sam anafanya kwa Sasa?
“Kwasasa nimekuwa nafanya kazi za Uimbaji na vikundi ambavyo vimekuwa vinatengenezwa kwa muda kwa ajili ya kazi fulani tu baadae kinaisha baada ya hiyo kazi.
Kuhusu aina ya Muziki ambao Sam anaupenda sana ni African Music kama Zouk,Rhumba,Qwato,Sebene,Tradition music, lakini pia napenda pia Black Gospel,Jazz,RnB,Soul, na Soft rock.

Ni Mwimbaji gani wa Gospel unaempenda zaidi kwa Hapa Nyumbani?
“Mwimbaji wa Gospel kwa hapa nyumbani naweza sema Jackson Benty, Minza na John Lisu zaidi ya hapo labda vikundi kama Next Level, Sowers, Holy of Holies, Calvary Band, UGM. Ila napenda zaidi makundi.

Vipi ulishawahi kurekodi Wimbo wowote?
“Nilipoanza muziki tulirekodi na hilo kundi ambalo nilijiunga nalo la LPP, mbali ya hapo nimekuwa nafanya na watu tu, ila ndo nimeanza taratibu za kuandaa album yangu ya kwanza maana sikupenda sana muziki wa kurekodi studio. Napenda sana muziki wa live, na hata kama ni kurekodi iwe live on stage maana naamini ndo unakuwa na mguso wa aina yake na kuwa karibu na Mungu at a particular time”

Mbali ya Uimbaji, ni Kazi gani Nyingine unayojishughulisha nayo?
“Mbali ya Uimbaji, nafanya kazi ya Video Shooting pamoja na Editing. Maana nda Taaluma yangu hiyo.”
 

Vipi umeshajiunga na Chama cha Waimbaji wa Nyimbo za Injili?
“Kiukweli bado sijajiunga na chama cha waimbaji, maana sikuwa asilimia zote kwa muziki maana nimekuwa na shughuli zingine hasa za kimasomo labda kwa sasa ndo naweza kuanza taratibu za kujiunga.”
 

Ni aina gani ya Muziki unaofanya?
“Mimi nafanya muziki wa asili ya kiafrika ambao nimeupa jina la African Christian Soul (Afrocso), na hii ni kutokana na kugundua sisi Tanzania tumebarikiwa na miziki mbalimbali ya asili ambayo ikifanyiwa kazi, inakuwa mizuri sana badala ya kuanza kucopy nchi za magharibi. Kkwahiyo huo ndo aina ya muziki ambao mimi naimba katika kumtukuza Mungu.”

Ni vyombo gani vya Muziki unavyoweza kupiga?
“Napiga vyombo mbali kama bass guitar, acoustic guitar, kinanda, solo guitar na drums kidogo, ila zaidi chombo changu ni Bass guitar.”
 

Nini Malengo yako ya Baadae?
“Malengo yangu ni kumtukuza Mungu katika anga za kimataifa, na kundi ambalo nililianzisha mwaka jana kwa jina la “The Psalmists” ambalo hadi sasa tumeshafanya matamsaha mawili moja lilifanyika Dar 9 – 1 – 2011 katika kanisa la FPCT Kurasini, na la pili Mwanza 8 – 1- 2012 katika kanisa la FPCT kitangiri pia naanda matamasha mengi zaidi ambayo sasa hivi yatakuwa na muziki wa asili zaidi ili ku’promote such kind of music which is much blesses much”

Sasa sikiliza Mahojiano aliyoyafanya Sam Batenzi na Radio France International, April 13, 2013 akiwa na Mwimbaji wa Nyimbo za Injili toka Congo, Nyumba ya Mungu.

Monday, May 27, 2013

Yaliyojiri kwenye Tafes Saut Live DVD Recording Jana, Pale JB Belmont Hotel - Mwanza.

JANA ndiyo ilikuwa siku ya kufanya LIVE DVD RECORDING ya kundi la Kusifu na Kuabudu toka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino-Mwanza. Shughuli hiyo iliyofanyika katika Hotel ya JB Belmont Hotel, ilianza mida ya Saa 9 Jioni na Kumalizika Mida ya Saa 3 Usiku chini ya Vocal & Music Director Samuel Yonah toka Dar es salaam.

DvD hiyo iliyopewa jina la Revival Flames Praise & Worship - Season 1 ukamilifu wake umefanikiwa chini ya Udhamini wa SIFA TANZANIA, CLARA SALOON na Radio ya Kikristo ya HHC ALIVE FM (91.9Mh) na Tukio hilo lilirushwa LIVE kupitia Radio Sayuni. Sasa tazama jinsi tukio hili lilivyofana....
 








Hiki ndo Kikosi cha Tafes Saut Kilichofanya Mashambulizi siku ya Jana
Sasa kama Jana hukupata fursa ya kusikiliza kilichokuwa kikiendelea pale JB belmont hotel kupitia Radio Sayuni iliyokuwa ikirusha Matangazo LIVE kutoka eneo la Tukio, hebu sikiliza wimbo huu ambao nilipata kuurekodi LIVE Siku ya Jana pale JB Bemont Hotel

Hiyo ni "Sample" tu, Original yenyewe inakuja. Jiandae kujipatia Nakala yako HALISI ya DVD ya Kwao Tafes Saut siku chache Zijazo.

Saturday, May 25, 2013

Historia ya Askofu Dkt. Mosses Kulola.

Moses Kulola, alizaliwa mwezi Juni 1928, katika familia ya watoto kumi, na watano kati yao bado ni hai. alisajiliwa katika shule ya kwanza mwaka 1939 iitwayo Ligsha Sukuma shule ya misheni baada ya Ligsha, alijiunga na taasisi ya usanifu mwaka 1949. Alibatizwa mwaka 1950 katika Kanisa la AIC Makongoro.
Ni mume wa Elizabeth na wamezaa watoto10 ambapo saba bado hai.alianza kazi za kimisionari mwaka1950 japokuwa aliitwa mwaka 1949 mara tu baada ya kubatizwa.


Mwaka 1959 alianza kufanya kazi serikalini, wakati huo huo akihubiri Injili katika miji na vijiji. Utumishi wake mkubwa kwa nchi ulifika mwisho mwaka 1962, ambapo aliamua kujitolea moja kwa moja nguvu zake zote, mwili na nafsi. Mwaka 1964 alijiunga na chuo cha kiteolojia na 1966 alitunukiwa stashahada.
Hakuacha elimu pale tu, aliendelea na masomo mbalimbali ambapo alitunukiwa vyeti mbalimbali katika mataifa mbalimbali.
Alihudumu kikazi kwa miaka miwili kama Mchungaji kabla ya kuwa mpentekoste mnamo 1961-1962, alifanya kazi katika kanisa la TAG 1966 mpaka 1991 ambapo aliamua kuanzishaa makanisa Evangelistic Assemblies God (EAGT), ambapo yalifanikiwa kukua kwa kasi kubwa katika nchi za Tanzania, Zambia , Malawi na kwa ujumla kuna makanisa yapatayo 4000 katika nchi mbalimbali yakiwemo makubwa na madogo. Askofu Moses Kulola anayeongoza makanisa elfu nne, Askofu Msaidizi wake ni Mwaisabila.

Mchakato wa kuongoza makanisa elfu nne si rahisi na kwamba kumefanyika mgawanyiko wa majimbo yasiyopungua 34 ya kazi na kanda tano kwa ajili ya kurahisisha kazi na kila kanda na jimbo lina mwangalizi wake. Nampenda sana Askofu Moses Kulola maana anafanya kazi ya MUNGU kwa moyo na kwa mujibu wa kitabu cha historia yake Askofu Kulola amezunguka Tanzania nzima tena wakati mwingine kwa kutembea kwa miguu na kwenye mazingira magumu sana kiasi kwamba ni wito mkuu wa MUNGU mkuu alionao Askofu Kulola na kwa miaka zaidi ya 60 amekuwa akihubiri neno la MUNGU na hadi sasa MUNGU anamtumia sana, katika mkutano uliopita wa askofu Kulola pale viwanja vya jangwani jijini Dar es salaam maelfu ya watu walihudhulia na wengi sana kufunguliwa na injili anayohubiri askofu Kulola ni injili iliyonyooka na akiwataka wanadamu kumpa YESU KRISTO maisha yao ili wapate uzima wa milele bure.


Ukiacha mengi ambayo Mungu anaendelea kumtumia mtumishi wake huyu, kuna suala la nywele zake, askofu Kulola kama tulivyowahi kuandika siku zilizopita, hajanyoa nywele zake kwa takribani miaka 47 sasa, kwakuwa hakupendezwa na suala la kwenda salon kunyoa nywele zake hivyo akamwambia Mungu nywele alizokuwa nazo kwa wakati huo zisikue zaidi au kupungua, na ndivyo ilivyo mpaka sasa wembe haujapita kichwani mwake.
CHANZO: Maisha ya Ushindi & Gospel Kitaa

Thursday, May 16, 2013

Askofu Mkuu Norbert Mtega akubaliwa kustaafu.

BABA Mtakatifu Francis, amekubali ombi la Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Norbert Mtega (68),pichani, kustaafu katika utume wa kuongoza jimbo hilo. Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Anthony Makunde, kutoka kwa Balozi wa Papa nchini, Askofu Mkuu Frascisco Padilla, ilieleza kuwa, Papa amekubali ombi hilo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ombi la Askofu Mtega kwa Papa, lilitokana na kuwa na matatizo ya kiafya, hivyo kushindwa kuwahudumia waumini inavyopaswa.

Hata hivyo, kikanisa ni siri ya mtu mwenye hadhi ya Askofu, anapoomba kwa Papa kustaafu. “Baba Mtakatifu Francis amekubali ombi la Mhashamu Askofu Mkuu Norbert Mtega, kustaafu kutoka majukumu ya utawala wa kichungaji wa Jimbo Kuu la Songea, kwa sababu ya kiafya,” ilieleza taarifa hiyo.

Hata hivyo haikufafanuliwa maradhi yanayomsumbua Askofu Mtega, ambaye pia kiumri ni miongoni mwa maaskofu wakongwe katika kanisa hilo nchini. Katika hatua nyingine, Papa amemteua Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, wa Iringa, kuwa msimamizi wa kitume wakati kiti cha Askofu wa Jimbo Kuu la Songea, kikiwa wazi, kwa mamlaka ya kiti kitakatifu (Mamlaka ya Vatican).

Kwa kawaida, hakuna muda maalum wa uteuzi wa Askofu Mkuu mwingine kuongoza jimbo, panapotokea askofu amestaafu utume, lakini huchukua hata miezi sita hadi mwaka kufanyika uteuzi. Hivi sasa jimbo hilo linaongozwa moja kwa moja kutoka Vatican kwa usimamizi wa Askofu Ngalalekumtwa.

Askofu Mkuu Mtega alizaliwa katika kijiji cha Kinyika (Lupanga-Njombe), Agosti 17, 1945. Alipata daraja la Upadri Novemba 14, 1973, aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Iringa Oktoba 28, 1985. Aliwekwa wakfu na Papa John Paul II Januari 6, 1986, huko Roma II, na miezi miwilli baadae, Machi 9, 1986 alisimikwa Iringa. Aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Songea Julai 6, 1992 na kusimikwa huko Songea Septemba 20 mwaka huo huo. Mwisho.

Wednesday, May 15, 2013

Album mpya ya Goodluck Gozbert kuingia Sokoni Mwezi Huu.

Goodluck Gozbert
Mwimbaji wa Nyimbo za Injili toka Jijini Mwanza, ambaye pia ni Mtayarishaji wa Muziki, Goodluck Gozbert anategemea kuingiza sokoni album yake mwezi huu, Album hiyo itakuwa na jumla ya Nyimbo 8, ambazo ni 1.Nimeuona,2.Uko Sawa, 3.Wa Moyo 4.Nimwabudu nani, 5.Shika sana 6.Mpaka Lini 7.Umetamalaki 8.Atoshekaye.

 Kaa Mkao wa kupokea kitu kipyaaa toka kwa Mwimbaji huyu. Sikiliza wimbo wake huu

Mawasiliano ya Goodluck Gozbert
0762486168

Safari ya Mwisho ya Pastor David Yared.

 

Picha: G Sengo

Tuesday, May 14, 2013

Maiti mbili zaokotwa kanisani Tabora.

Picha hii, haihusiani na Habari hii
MIILI ya watu wawili akiwemo mtoto wa mchungaji wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililo kwenye kitongoji cha Rehani, kata ya Tutuo, wilayani Sikonge, Tabora imeopolewa kwenye dimbwi la maji katika mazingira ya kutatanisha.

Mtoto wa mchungaji huyo aliyetambuliwa ni Pascal Yasin (27) na Utukufu Stefano Bugore (16) ambao ni wanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari ya Tutuo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vifo hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Edward Bukombe alikiri kupokea taarifa hiyo kutoka kwa watu waliotembelea eneo hilo.

Alisema marehemu hao hawakuwa na jeraha lolote katika miili yao ila mmoja alikuwa akitoka damu puani huku akibainisha kwamba uchunguzi wa awali umeonyesha kwamba marehemu walikuwa wakiogelea kwenye dimbwi hilo.

“Marehemu mmoja alikuwa na nguo ya ndani tu huku mwenzake akiwa na suruali bila shati, hivyo inawezekana walishindwa kuogelea wakazama… kwa sababu hawana alama yoyote ile katika miili yao,” alisema kaimu kamanda huyo.

Kwa mujibu wa Bukombe Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Sikonge amebainisha kuwa marehemu walizama baada ya kushindwa kuogelea hivyo wakanywa maji mengi. Aidha uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Awali mchungaji wa kanisa hilo wilayani Sikonge, Michael Namba, alisema upo uwezekano watu hao wameuawa kwa vile mchungaji wa kanisa la Tutuo hutumiwa ujumbe wa vitisho.

“Meseji zote za vitisho tunazo na tumetoa taarifa kwa polisi wa hapa Sikonge ili ziwasaidie katika uchunguzi wao, kwani hili lilipangwa na vitisho hivyo vinaendelea,” Alisema mchungaji Michael Namba.

Chanzo: Tanzania Daima

Tuesday, May 7, 2013

Hongera Boniphace Magupa na Jessica Honore kwa kufunga ndoa.

Juzi ilikuwa ni Siku ya Furaha kwa Wanandoa hawa wapya Boniphace Magupa ambaye ni Mtangazaji wa kituo cha luninga cha Chanel 10 na Jessica Honore ambaye ni Mwimbaji wa Nyimbo za Injili.

Harusi hii ilifungwa katika Kanisa la Anglikani mkoani Shinyanga, na kufuatiwa na tafrija fupi nyumbani kwa akina Boniphace Magupa maeneo ya Ndala, Shinyanga kabla ya kuelekea Ukumbi wa NSSF kwa ajili ya kuwapongeza Maharusi hawa.

Shughuli hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali kutoka mikoa mbalimbali Tanzania.
 Mtandao huu, unawatakia Maharusi hawa Maisha mema na yenye Furaha tele.

Monday, May 6, 2013

Bomu larushwa kanisani Arusha, mmoja afariki.

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 59 kujeruhiwa akiwamo Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla jana asubuhi baada ya mtu asiyejulikana kurusha bomu wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Jengo la Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha.

Miongoni mwa majeruhi, imeelezwa kuwa wanne ni mahututi. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amelielezea kuwa tukio hilo kuwa ni la kigaidi hasa kutokana na kumlenga Balozi wa Papa nchini na kwamba mtu mmoja anashikiliwa akihusishwa nalo.

Wataalamu wa mabomu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanachunguza aina ya bomu lililotupwa lakini uchunguzi wa awali unaonyesha lilikuwa limetengenezwa kienyeji.

Watu walioshuhudia tukio hilo wanasimulia kuwa bomu hilo lilirushwa yapata saa nne asubuhi wakati mgeni rasmi akijiandaa kufungua jengo la kanisa baada ya ujenzi wake kukamilika.

Shambulio hilo lilitokea wakati balozi huyo akiwa amesimama na mwenyeji wake, Askofu Mkuu, Josephat Lebulu, mapadri na watawa kutoka mashirika mbalimbali ya Jimbo Kuu la Arusha kwa ajili ya kukata utepe wa uzinduzi.

Kamanda Sabas alisema mtu aliyerusha bomu hilo alitokea nyuma ya kanisa hilo la ghorofa na kurusha bomu hilo kwa mkono wa kulia... “Alifanya jitihada za kupenya ili awafikie viongozi lakini alishindwa kutokana na wingi wa waumini waliokuwapo kwenye eneo hilo.”

Padri Moses Mwaniki aliyemshikia Balozi Padilla maji ya baraka yaliyotumika kubariki kanisa hilo, alisema kilichosaidia bomu hilo kutomfikia mwakilishi huyo wa Papa ni kutua mgongoni mwa mmoja wa waumini na kuanguka chini kabla ya kulipuka na kujeruhi watu.

“Ingawa hatuwezi kusema kwa uhakika, tunaamini mlengwa mkuu alikuwa mgeni wetu, Balozi Askofu Mkuu Padilla. Tunatakiwa kuliombea sana Taifa liondokane na matukio mabaya kama haya,” alisema Padri Mwaniki.

Baada ya tukio hilo, Balozi Padilla, Askofu Lebulu na viongozi wa kanisa hilo waliondolewa na kuhifadhiwa katika moja ya vyumba vya kanisa hilo kabla ya kutolewa kwenye eneo hilo yapata saa 5.30 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Msemaji wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Padri Festus Mangwangi alisema aliyerusha bomu hilo alishuhudiwa na mtoto mdogo aliyekuwapo kanisani hapo.

“Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto huyo, mtu huyo alikuwa amevaa kanzu nyeupe pamoja na koti la mvua lenye rangi ya kahawia na alikimbia mara baada ya kulirusha katikati ya watu. Ametusimulia kuwa mtu huyo baada ya kurusha bomu lile alikimbia na kuwahadaa watu kwa kuita ‘mwizi mwizi mwizi…’ akionyesha mbele kama kuna mtu anayemfukuza jambo lililowazubaisha watu lakini mtoto aliyemwona akirusha bomu aliwaeleza kuwa ndiye mhusika.”

“Waliomshuhudia mhusika akikimbia wanasema walishindwa kumwona mwizi aliyekuwa akimfukuza na hivyo kubaki wakimkodolea macho, hali iliyomfanya atokomee katikati ya nyumba za watu,” alisema Padri Mangwangi, ambaye aliongeza kuwa katika kipindi hicho kulikuwa kuna mkanganyiko mkubwa kutokana na bomu kulipuka na mtu huyo kudai kuna mwizi.

Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Julius Mbaga ambaye mkewe, Concesa (42), ni mmoja wa majeruhi, alisema ni kudra za Mwenyezi Mungu pekee ndizo zimeepusha madhara na maafa makubwa

Aliyefariki ametambuliwa kuwa ni Regina Losioki (46), ambaye alikuwa anaimba kwaya katika kanisa hilo. Alifariki baada ya kufikishwa katika Hospitali ya St. Elizabeth, Arusha.
Mamia ya watu jana walifurika katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kushuhudia watu waliokuwa wakifikishwa hapo kutoka katika eneo la tukio.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa, Dk Frida Mokiti alisema majeruhi 41 walikuwa wamelazwa Mount Meru, 16 walikuwa Hospitali ya St Elizabeth huku mmoja akiwa katika Hospitali ya Selian na mwingine Hospitali ya Kaloleni... “Kuna mgonjwa mmoja, ambaye amepelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC (Moshi) kwa matibabu zaidi.”

Waliojeruhiwa ambao majina yao yalibandikwa katika ukuta wa Hospitali ya Mount Meru ni Christopher Raymond (10), Consensia Mbaga (53), Deborah Joachim (24), Elizabeth Isdori (24), Bertha Cosinery (49), Anna Didas (52), Edda Ndowo(77), Derick Cyprian (8), Faustine Andrea (35), Mary Okech na Neema Daud (13).

Alex Arnold, Agripina Alex (9), James Gabriel (16), Loveness Nelson (17), Amalone Pius (25), Frank Donatus (10), Alphonce Nyaland (26), Athanasia Reginald (14), Phillemon Ceressa (49), Neema Daud (13) Sophia Kanda (72), Theofrida Innocent (21), Regina Darnes (17).

Mesoit Siriri (33), Clenes Pius (22), Joyce Yohana (15), Restuta Alex (50), Mathias Riha (74), Magreth Andrew (45), James Gabriel (16), Regina James (17), Elizabeth Masawe (15), Elizabeth Sauli (18), Njau (35), Yasinta Msafiri (160) na Doreen Pancras (28).

Waliokuwa katika Hospitali ya St. Elizabeth kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Samwel Mlay ni Fatuma Tarimo, Glory Tesha, Rose Pius, Isabela Michael, Jenipher Joachim, Samwel Laswai, John James, Joan Temba, Joram Kisera, Novat John, Neema Kilusu, Regina Shirima, Inocent Charles, Lightness na Anna Edward.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Wednesday, May 1, 2013

Word Explosion Summit yaanza rasmi Mwanza.

Mch. Emmanuel Mchutah
Ile Semina ya WORD EXPLOSION SUMMIT inayoingia siku ya pili leo, Jana ilifanyika katika Kanisa la TAG Nyamalango, Malimbe Mwanza na kuhudhuriwa na Watu wengi sana. Semina hiyo ambayo wanenaji ni Mchungaji Emamuel Mchutah na Janeth Mchutah, itafanyika kwa Siku 5, ambapo siku ya jumamosi itakuwa ndiyo siku ya mwisho ya Semina hiyo.

Siku ya Jana ilikuwa ni Siku ya Utangulizi tu, na Mafundisho rasmi yanaanza leo kuanzia Saa 11:45 Jioni mpaka Saa 2 Usiku. Kwa siku ya Jana, Vijana wengi walijitokeza kukabidhi Maisha yao kwa Yesu(Kuokoka).

Tazama video hii, inayoonyesha baadhi tu ya Watu walioamua kumpokea Yesu huku Mchungaji Emmanuel akiwaongoza sala ya toba