Advertise Here

Tuesday, September 11, 2012

Mchungaji Vinac Mwakitalu; Matatizo ya Serikali ya Tanzania, Chanzo ni Kanisa.

Mchungaji Vinac Mwakitalu
 
WAKRISTO wametakiwa kujua kwamba matatizo makubwa katika serikali ya Tanzania yanatokana na wao kutokuwa waaminifu mbele za Mungu katika kufanya Ibada ya Utoaji.
 
Akihubiri katika Ibada ya Jumapili Mchungaji na Mwalimu Vinac Amnon Mwakitalu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Ilomba Christian Centre Mbeya amesema serikali nyingi ulimwenguni ikiwemo Tanzania zimejikuta katika changamoto mbalimbali kutokana na kanisa kutokuwa waamini katika utoaji wa mafungu ya 10 na sadaka mbalimbali. 

Mchungaji Mwakitalu ameongeza kusema Mungu ndiye anayejua kipimo halisi cha utoaji kwa mtu wa Mungu na kwamba kwa kufanya hivyo hakuna anayeweza kumdanganya Mungu. Pia Mchungaji Mwakitalu amesema wengi wamefikiri kuwa kufunga na kuomba sana ndio miujiza itafanyika huku wakisahau utoaji wa Mafungu ya 10 na sadaka mbalimbali. 

Aidha Mchungaji Mwakitalu alibainisha Baraka za mwamini anayekuwa mwamini katika utoaji wa sadaka na mafungu ya 10 kuwa Mungu atafungua madirisha ya mbinguni na Baraka zake zitamiminika kwa mja wake.

Sunday, September 9, 2012

Kanisa la Anglikana lataka kuwa na Raisi.

Archbishop Rowan Williams
ASKOFU Mkuu wa kanisa la Anglikana, Rowan Williams, amefichua siri kuwa kanisa hilo linaandaa mpango wa kumteua rais wa kanisa, ambaye atabeba sehemu ya jukumu la kuongoza kanisa duniani.

Alisema mtu atayechukua nafasi hiyo ataweza kusafiri kwa urahisi, na hivyo kumuacha Askofu Mkuu kushughulika zaidi na kuongoza kanisa.

Doctor Williams, ambaye anastaafu mwezi Disemba baada ya uongozi wa miaka 10, alikiri kuwa hakuweza kufanya mengi kuzuia mgawanyiko kanisani juu ya swala la uhusiano wa jinsia moja.

BBC Swahili

Mchungaji aliyebadili Dini kuwa mkristo, aachiwa huru baada ya kifungo cha Miaka 3 gerezani.


MCHUNGAJI wa Kanisa moja Nchini Iran Mch. Youcef aliyekuwa kifungoni kwa zaidi ya miaka mitatu kwa kukabiliwa na kosa la kuuasi uislam na kubadili dini kuwa mkristo, sasa ameachiwa huru. Mchungaji huyo alipata hukumu ya kunyongwa ili kuwatisha watu wengine wasibadili dini kuwa wakristo.

Sehemu mbalimbali Duniani kulikuwa na maombi ya mnyororo ya kufunga kwa wakristo ili kumuomba Mungu awezeshe kuachiwa huru kwa Mchungaji huyo na hilo Mungu amefanya leo kwani Mchungaji Youcef ameachiwa huru na kuungana na familia yake.

Glory to God!

Friday, September 7, 2012

Mahakama Mkoani Arusha yaitupilia mbali kesi ya Kanisa Anglikana.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha, imetupilia mbali kesi ya kupinga kusimikwa kwa Askofu Stanley Hotay kuwa askofu wa Kanisa la Anglikani Dayosisi ya Mlima Kilimanjaro, iliyofunguliwa mahakamani hapo na waumini watatu wa kanisa hilo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Fatma Massengi, aliyesikiliza shauri hilo la madai namba 118/2011 na jinai namba 48/2011 yaliyofunguliwa na waumini wa kanisa hilo, Parokia ya Mtakatifu James, Lothi Oilevo, Godfrey Mhone na Frank Jacob, dhidi ya bodi ya wadhamini wa kanisa hilo pamoja na askofu huyo.

Hata hivyo baadaye mahakama ilimuengua kwenye shauri hilo Mhone baada ya kushindwa kukidhi vigezo kisheria.

Katika hukumu yake jana, Massengi alisema kuwa alifikia uamuzi wa kuliondoa shauri hilo mahakamani hapo bila gharama wala kutoa maagizo yoyote baada ya kuridhika na pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa wadaiwa, Albert Msando na Joseph Thadayo.

Mawakili hao walidai kuwa mahakama hiyo haina nguvu kisheria kusikiliza shauri hilo kwani katiba ya kanisa hilo iko wazi kuwa masuala yote ya uchaguzi ndani ya taasisi hiyo yatashughulikiwa na ngazi mbalimbali ndani ya kanisa, ambapo mamlaka ya mwisho ya rufaa ni nyumba ya maaskofu wa kanisa hilo inayojumuisha maaskofu kutoka dayosisi zote.

Jaji Massengi alisema kuwa hata mambo yanayobishaniwa kisheria hayapo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali yako kwenye Katiba ya Kanisa la Anglikani, ambayo mahakama hiyo haina nguvu kisheria kuyaingilia.

Aliongeza kuwa kutokana na msingi huo mahakama haiwezi kuingilia suala hilo huku akikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa wadai hao walifanya makosa ya kisheria kwenye hati ya kufungua madai mahakamani hapo ambapo badala ya kuandika namba ya usajili wa bodi ya udhamini ya kanisa waliweka namba ya cheti cha usajili ya kanisa SO 4757.

Katika kesi ya msingi wadai hao kwa pamoja waliomba mahakama itoe tamko kuwa Hotay waliyedai alidanganya katika cheti chake cha kuzaliwa cha Februari 12, 2010 na kwamba cheti hicho kilitolewa kwa njia ya udanganyifu, hivyo mchakato wote wa uchaguzi ukiwamo wa Aprili 15 mwaka huu uliomweka madarakani ni batili.

Wadai hao kupitia wakili wao, Meinrad D’Souza, walidai kuwa Katiba ya Kanisa la Anglikani, inaeleza kuwa mchungaji wa kanisa hilo anayeweza kufikiriwa kutwaa cheo hicho cha juu, anatakiwa awe na miaka kati ya 40 na 60 wakati inadaiwa mchungaji huyo mwaka jana alikuwa ana miaka 38 .

Katika kesi yao ya pili, waliiiomba mahakama kuzuia sherehe za kusimikwa kwake zilizopangwa kufanyika Juni 12 mwaka huu jijini Arusha, hadi kesi zote zitakaposikilizwa na kutolewa maamuzi na mahakama hiyo.

Aidha, shauri hilo lilisimama kwa muda baada ya Juni 10 mwaka huu, Jaji Sambo aliyekuwa akisikiliza shauri hilo kutoa amri ya zuio la muda kuzuia Hotay asisimikwe kushika wadhifa huo katika sherehe zilizopangwa kufanyika siku mbili baadaye ili kumwezesha kutoa uamuzi wa mapingamizi hayo Juni 13, mwaka huu.

Licha ya zuio hilo, sherehe za kusimikwa Hotay ziliendelea na akapewa daraja la uaskofu bila kupangiwa kituo rasmi cha kazi, hatua iliyoibua mvutano mkali wa kisheria kati ya kanisa hilo na Idara ya Mahakama baada ya Jaji Sambo kutoa amri ya kukamatwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini , Dk. Valentino Mokiwa na askofu Hotay ambao walikata rufaa Mahakama ya Rufani.

Tanzania Daima

KKKT laitaka Serikali kuweka sheria Madhubuti Juu ya Unyanyapaaji wa Walemavu.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ) Dayosisi ya Kaskazini limeitaka serikali na jamii kwa ujumla kuweka sheria madhubuti zitakazowalinda watu wenye ulemavu dhidi ya unyanyapaa.

Katibu mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini bwana Julius Mosi ametoa kauli hiyo wakati akikabidhi viti mwendo nane kwa watu wenye ulemavu vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Gabriella Children Rehabilitation center katika kijiji cha Uhuru kata ya Arusha chini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Bwana Mosi amesema kutokana na kuendelea kubaguliwa kwa watu wenye ulemavu na kunyimwa haki zao za msingi ni vyema serikali ikaweka mkazo wa kuwalinda watu hao ikiwa pamoja na kuwapatia elimu maalumu itakayowawezesha kutumia viungo vyao ili waweze kujitegemea.

Nae mkurugenzi wa shirika la Gabriella Children Rehabilitation centre lenye makao yake mjini linalojihusisha na utoaji huduma kwa jamii kwa watu wenye ulemavu Bi.Brenda Shuma, amesema shirika lake litaendelea kutoa misaada kwa watu wenye ulemavu ili kuwajengea uwezo wa kutumia viungo vyao katika kufanya kazi mbalilimbali za kujiletea maendeleo.