Advertise Here

Thursday, April 18, 2013

Baraza la Makanisa Zimbabwe launda Tume ya Wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu.

Wananchi wa Zimbabwe wameanza maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, baada ya kupitisha Katiba kwa kura ya maoni na hivyo kufanya mabadiliko makubwa yanayopania pamoja na mambo mengine, kupunguza madaraka makubwa aliyokuwa nayo Rais, kusimamia haki msingi za binadamu pamoja na kudumisha misingi ya haki na amani.

Kwa kuzingatia historia ya Zimbabwe kwa miaka ya hivi karibuni, iliyopelekea machafuko ya kisiasa na hatimaye kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Baraza la Makanisa Zimbabwe limeunda Tume ya Kiekumene ya Wasimamizi wa Uchaguzi mkuu, yenye dhamana ya kukoleza moyo wa majadiliano, ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Tume hii inatekeleza wajibu wake kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu na inasimamiwa na Tenda Maregere. Haya ni malengo ambayo Baraza la Makanisa Zimbabwe lilijiwekea kwa kitambo kidogo, kwa sasa yanafanyiwa utekelezaji wake, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la Misna.

Makanisa nchini Zimbabwe yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na umoja wa kitaifa, bila kusahau upatanisho pale ambapo kinzani na migogoro ya kisiasa ilipojitokeza; mambo ambayo yamekuwa ni sehemu ya historia ya wananchi wa Zimbabwe tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru kutoka katika utawala wa Mwingereza.

Tume ya Mabaraza ya Makanisa pamoja na mambo mengine inapania kukuza moyo wa majadiliano miongoni mwa wananchi wa Zimbabwe, kudhibiti mchakato mzima wa upigaji kura ili haki, uhuru na ukweli viweze kutawala na hatimaye, Zimbabwe iweze kuwapata viongozi watakaochaguliwa kwa kura halali wakitambua dhamana na wajibu wao katika kuiendeleza nchi yao. Tume itakuwa na wajibu wa kusema haraka iwezekanavyo pale ambapo kutakuwepo na ukiukwaji wa haki msingi za binadamu.

Vyama vikuu vya upinzani vinavyotoana jasho kwa sasa ni ZANU-PF kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe pamoja na Chama cha Democratic Movement for Change kinachoongozwa na Waziri mkuu wa Zimbabwe Bwana Morgan Tsvangirai; wapinzani wakuu waliopelekea machafuko ya kisiasa nchini Zimbabwe kunako mwaka 2008.

Saturday, April 13, 2013

Namna ya Kuongeza Imani unapokuwa kwenye Jaribu.

2 
Mpenzi msomaji Shalom,

Biblia katika kitabu cha Mathayo 17:18 inasema‘..Ni kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana amini nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. Hii ni habari ya yule kijana aliyekuwa na pepo bubu na kiziwi, mzazi wake akamleta kwa wanafunzi wa Yesu wamwombee. Biblia inatueleza kwamba wanafunzi walijaribu kumtoa yule pepo wasiweze, wakati huo Yesu alikuwa amepanda Mlimani kwenda kuomba.
 
Yesu aliporudi alielezwa kilichotokea, akawakemea wanafunzi wake na kisha akamuombea yule kijana akapona. Baadaye wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, kwa nini sisi hatukuweza kumtoa yule pepo. Ndipo Yesu akawajibu akasema ‘Ni kwa sababu ya upungufu wa imani yenu… Neno upungufu lina ya isiyo – tosheleza, yaani imani yao ilikuwa ina upungufu na kwa hiyo wasingeweza kumtoa yule pepo. Jambo ninalotaka tuliangalie ni kwamba kwa kuwa tatizo lilikuwa ni upungufu wa imani yao, ina maana walitakiwa kuongeza imani yao wakati wanaendelea kukemea. Sasa swali muhimu ni je wangeongezaje imani yao wakati wako kwenye jaribu/vitani?

Naam licha ya swali hili kuna maswali mengine ambayo ni muhimu kuyatafakari ili tuweze kuwa na ufahamu mzuri wa imani. Je upungufu huu wa imani kwa wanafunzi walikuwa nao kabla hawajaanza kukemea yule pepo au ulikuja wakati wanaendelea kuomba. Naam Yesu anatuonyesha kwamba kosa la hawa wandugu wenzetu lilikuwa upungufu wa imani yao?

Ni kwa namna gani walikuwa na upungufu wa imani?
Biblia katika Waebrania 11:1 inaeleza kwamba ‘imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana’. Kwa hiyo endapo Yesu alisema ni kwa sababu ya upungufu wa imani yao ina maana ndani yao walipungukiwa uhakika wa kile walichokitarajia, ambacho ni kufunguliwa/kuponywa kwa kijana mwenye pepo. Naam upungufu wao wa imani ulitokana na  mashaka juu ya uhakika wa yule kijana kufunguliwa.

Nini kilipelekea wao kuingiza hofu/mashaka?
  • Kukosekana kwa dalili za kijana kufunguliwa – Ni imani yangu kwamba wanafunzi walipoanza kukemea walikuwa na uhakika kwamba Yule kijana atafunguliwa. Naam kadri walivyoendelea kuomba na kuona kwamba hakuna mabadiliko ya aina yoyote kwa mgonjwa yule ndipo hofu/mashaka yakawaingia mioyoni mwao. 
  • Maneno ya kusikia – Ikumbukwe kwamba chanzo cha imani yoyote ni kusikia (Warumi 10:17)?  Kumbuka wakati wanendelea kuomba kulikuwa kuna kundi kubwa la watu ambao walikuwa wanamsubiri Yesu pamoja nao. Hivyo huenda wakati wanafunzi wanaaendelea kuomba walisikia watu wakisema, wanafunzi wa Yohana wenyewe walishindwa kumuombea, wao wataweza, wamejaribu watumishi wa kila aina wameshindwa, huyu hawezekani anasubiri kifo, naam haya yote yakapunguza uhakika ndani yao kwamba kwa jina la Yesu yule kijana anaweza kupona.
  • Maneno yao wenyewe – Biblia haituelezi namna/approach waliyoitumia kuomba/kukemea. Huenda walianza kuomba mmoja mmoja/ au waliomba wachache na mwishowe ndipo wakaomba kama kundi. Kwenye kundi lolote kuna mengi, huenda walipokemea kwa muda kadhaa na bila kijana kuonyesha dalili za kupona baadhi ya wanafunzi wakaingiwa na hofu na wakawaambukiza na wengine na hivyo kushindwa kumtoa pepo. Hebu jaribu kufikiri mtu kama Yuda Iskariote alikuwa anafanya nini wakati wenzake wanakemea?

Nini cha kufanya?
Hofu/mashaka ni silaha kubwa sana ambayo Shetani huitumia kuwafanya watu washindwe kupata majibu ya maombi/miujiza yao kutoka kwa Mungu. Shetani anafahamu kwamba imeandikwa ‘Mwenye haki wangu ataishi kwa imani, naye akisstasita roho yangu haina furaha naye’ (Wabrania 10:38). Hivyo ili kuharibu/kuondoa imani ya mtu kwa Mungu, silaha anayotumia ni kuingiza mashaka moyoni mwake dhidi ya ahadi za Mungu/neno la Mungu kwenye maisha yake. Yesu aliwaambia hivi wanafunzi wake ‘… amini nawaambia yeyote atakayeuambia mlima huu ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake’ (Marko 11:22).  

Mpenzi msomaji kamwe usimruhusu Shetani kwa kutumia silaha hii ya mashaka azuie baraka zako na wale wanaokuhusu maishani mwako. Haijalishi jaribu limesimama mbele yako kwa kiwango gani usiondoe imani yako juu ya kile ambacho Yesu amekisema kwenye neno lake juu yako. Naam Mungu wetu si mtu hata aseme uongo, ahadi zake ni amina na kweli.   Naam katikati ya jaribu/changamoto wewe ongeza imani yako kwa kupambana na roho ya mashaka/hofu, naam tumia Biblia ili ikuongoze kukupa mistari ambayo itakuongezea uhakika wa kufanikiwa katika lile ulifanyalo.

Zaidi kuwa makini na maneno ya kusikia kwa habari ya imani yako. Wanafunzi wa Yesu walipaswa kutokujali maneno ya kusikia kutoka kwa watu, au kwa wenzao walioingia mashaka, naam walipswa kudumu kuamini kwamba kijana atapona naam ingekuwa hivyo. Je si unakumbuka habari za Petro alivyoambiwa na Yesu atembee juu ya maji. Awali alianza vema na akatembea hatua kadhaa juu ya maji.    Biblia inasema dhoruba ilipompiga akaona shaka na kuanza kuzama. Kwa nini alizama? si kwa sababu Yesu hakuwepo, bali ni kwa sababu aliona shaka.

Naam kitu kilichopungua kwenye imani ya wanafunzi, ni uhakika kwamba yule kijana atapona. Na kilichopelekea upungufu wao wa imani, si   kutokumwamini/kumjua Yesu, bali ni kuruhusu hofu ichukue nafasi ya imani/uhakika waliokuwa nao kwamba yule mgonjwa atapona. Naam kwa mara nyingine tena ‘usirihusu hofu iharibu muujiza/future yako’.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nawe daima.

Mwl. Patrick Samson Sanga
+255 755 816 800

Friday, April 12, 2013

Mwimbaji wa Bongo Flavour Kenya Aokoka.

http://themonsterradio.com/wp-content/uploads/2012/10/size-81-440x248.jpgMwimbaji wa Muziki wa kizazi kipya Nchini Kenya Linet Munyali a.k.a Size 8, ametangaza rasmi ya kuwa Ameokoka na hivyo kuachana na Muziki wa Kizazi kipya.
 
Akiongea na Mtangazaji wa Clouds Fm Millard Ayo kupitia kipindi cha Amplifier cha leo April 12, Size 8 amesema, "Nimeamua kuokoka kwasababu Maisha yangu yalikuwa hayana Amani. Mara nyingi nilikuwa Mtu wa Huzuni na kuna kipindi nilikuwa nikitoka kufanya Show Usiku najikuta nalia mwenyewe".

"Pamoja na kwamba pesa ninayo lakini maisha yangu yalitawaliwa na Huzuni" aliongeza Size 8. Akitoa sababu ya yeye kutokuwa na Amani, Size 8 amesema kuwa, hali hiyo ilikuwa ikimtokea tu, na yeye pia hajui sababu ilikuwa ni nini.

Huyu atakuwa si Mwimbaji wa kwanza wa Muziki wa kizazi kipya Nchini Kenya kutangaza kuokoka. Mwimbaji mwingine aliyewahi kuokoka ni DNA aliyetamba sana na Wimbo wa Banjuka. Kwa Tanzania Mwimbaji Stara Thomas pia aliwahi kutangaza kuokoka lakini akaamua kurudi nyuma tena na kuimba Bongo Flavour tena.

Swali la Msingi la kujiuliza, ni; Je! Nini kinafanya Waimbaji hawa kurudi nyuma na kuimba tena Bongo Flavour? Ni jukumu la Kanisa sasa kuhakikisha kuwa watu kama hawa wanalelewa vizuri Kiroho ili waweze kudumu katika Wokovu.

Papa Francis kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kanisa la Mt. Paulo Jumapili hii.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 14 Aprili 2013 kuanzia saa 11:30 jioni, anatarajiwa kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya Kuta za Roma na baadaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Katika Maadhimisho ya Ibada hii, Baba Mtakatifu atasaidiana na Kardinali James Michael Harvey, Kardinali Codero Lanza di Montezemolo, Kardinali Francesco Monterisi pamoja na Abate Edmund Power, OSB.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita majira ya jioni aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma na kuanza utume wake rasmi kama Askofu wa Jimbo la Roma. Ibada hii ilihudhuriwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika ndani na nje.

Kama inavyoonekana kuwa ni sehemu ya utaratibu wake, Baba Mtakatifu Francisko huanza kwa kusalimiana na waamini na watu wenye mapenzi mema, ambao wamekuwa wakifurika katika matukio kama hawa tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa. Huu ni upepo mpya wa imani na matumaini ndani ya Kanisa.

Thursday, April 11, 2013

Spacio: Mwimbaji wa Nyimbo za Injili aliyeishi na Jini Mahaba kwa Miaka 17.

Kwa jina naitwa Spacio Abubakary Ngalla, nimezaliwa na kukulia Dar es salaam, Sinza. Na ni mtoto wa 3 katika familia ya kiislamu.

Kiukweli mimi nilikuwa mmoja wa watu ambao hawakutaka kusikia Jina la YESU na nilikuwa siamini miujiza yeyote na kuona ni mazingaombo tu wachungaji wanafanya kuwateka watu akili. Ila hadi siku ambayo mungu aliponionesha njia ya uzima na kuniponya tatizo lililonisumbua mda mrefu, ndipo nikaamini uwepo wa UKRISTO

NILIVYOKUTANA NA JINI MAHABA
Nakumbuka ilikuwa mwaka 1996, nikiwa na miaka 7, Mimi na marafiki zangu tulikuwa na tabia ya kwenda kuogelea coco beach siku za weekend, siku moja baada ya kumaliza kazi zangu za nyumbani majira ya saa 6 hivi nikaenda kuwapitia marafiki zangu (4) ili twende beach kuogelea ikifika jioni turudi nyumbani. Tulipofika beach watu walikuwa ni wengi sana kila mmoja alikuwa yupo busy na yake, sisi tulijigawa wengine walienda kuogelea sehemu nyingine, mimi na mwenzangu Ali tulibaki upande wa mwanzoni kwa kuwa hatukuwa tunajua kuogelea vizuri.

Majira ya saa 10, hivi nikiwa na Ali, nilisikia harufu nzuri kweli ikiwa inavuma kuja kwetu, ambayo siku wahi kuisikia kabla, ni nzuri kwa kweli, nikamuuliza Ali “unaisikia harufu hii?” yeye akajibu ndio ninaisikia ila sijui inatoka wapi!

Baada ya dakika kadhaa nilisikia sauti ya kike ikinisalimia “hujambo?” nikashtuka, kugeuka nyuma nikakutana na msichana sijui nimuelezeeje, ni mweupe kiasi, ana nywele ndefu, sura yake ipo serious na ukiiangalia tena ni kama anatabasamu, macho yake ni ang’avu, ni mzuri kiufupi akiwa amevaa nguo za kawaida tu ila kichwani amejitanda baibui. Aliniambia jina anaitwa MAIMUNA!

Mwili uninisisimka huku kidogo nikiwa na natetemeka japo sikutaka kumuonesha kwa kuwa hilo jina halikuwa geni kwangu, cha ajabu kadri alivyokuwa anaongea na mimi uoga ulizidi kunipungua hadi nikawa najiskia kawada na kucheka pamoja. Aliomba tuogelee wote nikamwambia, mimi siwezi kuogolea vizuri, akaniambia “Usiwe na wasi wasi nitakufundisha usijali” basi akaanza kunishika mikono na kuanza kunivuta ili niweze kujifunza kupiga mbizi taratibu. Siku hiyo ilikuwa ni tofauti sana kwani tulifurahi sana.

Saa 12 na nusu jioni ilipofika tukaanza kujiandaa kwa safari, siku hiyo tulichelewa kweli kuondoka! Ghafla Maimuna nikawa simuoni, nikaita sana “Maimunaaaaa uko wapi sisi tunataka kuondokaaaaa!” Kimyaa! Basi  sisi tukaanza kuondoka pale beach, kuna sehemu huwa ina miti mingi sana na ni shortcut kwenda kituoni, kwa mchana ni salama lakini kama ni giza giza si pazuri huwa kunakuwa na wahuni. Sisi tukiwa tunakaribia hiyo njia roho ilisita kupita pale, kumbe nyuma kulikua na wahuni wakitufatilia. Na sisi tupo watato tu, wao walikuwa watatu.

Heee mara tukashangaa kundi la watu zaidi ya 15 nao wakawa wanapita hiyo hiyo njia, basi sisi tukaongozana nao hadi kupita ile njia salama, kushtuka tunajiona tupo wa tano tu mbele tunakajiuliza “wale watu wameenda wapi?” Wahuni kumbe walikimbia katikati! sasa hatukujua ni kwa kwa sababu gani. Ila mimi nikahisi kundi la watu wale hawakuwa watu bali ni majini ndo waliotusindikiza, nikawaambia wenzangu “jamani tukimbie wale ni majini” kwa sauti kubwa ya uoga”.


URAFIKI NA JINI MAIMUNA
Tukafika nyumbani kila mmoja hoi, mimi bado nilikuwa na mawazo ya yule msichana niliyekutana nae baharini. Usiku nikiwa ndotoni nilimuota akija kunitembelea nyumbani na kufurahi pamoja.

Hali ile iliendelea hadi nafika form 1, ambapo nilikuwa nasoma Azania Sec School, haipiti siku moja lazima niote tuko pamoja tunafurahi pamoja hadi nikazoea,

Mwaka 2004, Maimuna alijitokeza tena kwa mara ya pili nikiwa niko chumbani, niliogopa sana nilipiga kelele mama akaja Maimuna akaondoka. Mama alishushwa sana na hali hiyo akaniuliza tatizo ni nini lakini nikamwambia nilikuwa naota tu, niliogopa kusema kwa kuwa Maimuna aliniambia nisiseme chochote kuhusu yeye la sisivyo nitakiona cha moto.

Baada ya muda nikazoea, akija tunaongea tu vizuri na kazi zingine alikuwa ananisaidia kama kutengeneza computer za baba, alikuwa ananisaidia kama tatizo ni kubwa sana namwita kimoyo moyo anakuja ktk mwili wangu kisha naanza kutengeneza computer, watu wengi walinishangaa sana uwezo niliokuwa nao lakini kumbe walikuwa hawajui JINI ndie alikuwa mara nyingi ananifundisha usiku.

Alinipa hela nyingi tu kiasi kwamba nilikuwa naenda shule nikiwa elfu 50, laki, ILA ole wangu nitumie na mwanamke au nimnunulie mtu sigara, pombe, basi hela zote zinapotea na nitahangaika hata shilingi 100 sipati zaidi ya kupewa hela ya shule, na nitahangaika hadi basi.

KAMA kawaida ukisha fikia umri fulani lazima uanze utundu wa kufatilia wasichana, kuwapa hela au kuwanunulia zawadi hasa katika siku kuu vile au valentine day, mimi iliponza sana hiyo tabia, kwani niliteseka sana.Kwani maimuna alikuwa hapendi

Kitu kilichonifanya nitafute wasichana wengine ni kwamba Maimuna hakuwa anakuja kila wakati, ni mara moja tu kwa siku tena hasa usiku. Na pia ukiangalia hata nikija kukua yeye anabaki jini na mimi binadamu kwa hiyo si rahisi kuja kuishi pamoja.

ILA chochote kilichokuwa kibaya kwangu kilichotegeshwa kichawi hakikuweza kunipata na hata usiku wachawi hawakuweza kunifata fata, japo mwanzoni nilihangaika sana na wachawi kwani walikuwa wanatusumbua sana nyumbani, waganga walidai nyumba haikuwa na zindiko!

Kiukweli alinifundisha vitu vingi pamoja na uchoraji, utayarishaji muziki, computer ambavyo hadi sasa vinanisaidia ktk maisha yangu, baada ya kutoka darasani yeye hunifuata usiku na kunielekeza zaidi. MIAKA YOTE HIYO TULIISHI KAMA WACHUMBA.Mengine siwezi kuyataja lakini mtakuwa mshaelewa nini ninamaanisha.


UGOMVI NA JINI KUANZA
Mwaka 2009, nina miaka 20 nikiwa nafanya kazi Cellulant Tanzania, kuna dada mmoja alikosea namba na kupiga kwangu, alijitambulisha kwa jina anaiwa UPENDO, mara ndio ukawa mwanzo wa urafiki wetu ambae hadi sasa tunaishi pamoja tukijipanga kwa ajili ya kufunga ndoa. Nilitokea kumpenda sana dada huyo japo hatukuwa tumeonana, na hata yeye pia alitokea kupenda kuongea na mimi mda wote. Maimuna alikuwa hapendi tabia ya mimi kuongea na huyo dada na mara nyingi alikuwa ananionya sana, ila mimi ilikuwa vigumu mno kukubali kwani nilikuwa nimshapenda tayari.

Siku moja nikasema hataa lazima nionane na huyu dada, hadi lini tutaishia kuongea kwa simu tu. Kwa mara ya kwanza kukutana na dada huyo, usiku wake sikulala! Nilipatwa na homa hadi asubuhi yake sikuweza kwenda kazini ikabidi nipumzike. Mara mwili unachoma, mara kifua kinanibana, mara kichwa kinaniuma, kikitulia nyama za mwili zinatikisika kama mtu anani vibrate vile.Niliteseka sana wiki nzima nilkuwa mgonjwa. Maimuna akaniambia hiyo ni bakora moja nimekupa, nataka uachane na UPENDO.

Baada ya kuseka sana kwa hali hiyo kwani mara kwa mara ilikuwa inanitokea, nikaanza kwenda kwa waganga kutafuta tiba ya kumuondoa jini huyo katika mwili wangu,kwani alikuwa kero kwangu, zaidi ya waganga 15 nilikwenda lakini bila mafanikio.


                                                    KUOKOKA KWANGU
Baada ya kuchoka kuvumilia nikamfuata rafiki yangu wa karibu Robert na kuanza kumueleza,  akaniambia kwanini usiende kuombewa, mbona wengi tu wanapona na hata mjomba wangu alikuwa anaumwa miguu alipoombea akapona. Nikamwambia sasa nikienda huko wazazi wangu waanifikiriaje? Akanijaza moyo na kunipa ujarisi kuwa “IMANI YAKO NA MUNGU SI YA WAZAZI WAKO BALI NI WEWE NA MUNGU WAKO NA HATA UKIFA UTAENDA NAO? SI WEWE NDIE UTAKAYE ENDA KUJIBU HUKO? FANYA MAAMUZI YALIYO SAHIHI”

Nikakubali! Basi nikasubiri jumapili ilipofika nikajiandaa na kwenda kanisani kuombewa, hakika nilipoombewa kila kitu kili badilika na kijisikia mwepesi kama vile nilikuwa nimebeba viroba vya michanga! Nilipoombewa nikadondoka chini na kupoteza fahamu. Baada ya dakika kadhaa nikaamka na kujikuta nikochini nimelala huku nikijishangaa nini kilichotokea.

Toka hapo nikaamini na nikaamua kuimba Nyimbo za Injili ili kueneza Neno la Mungu kwa wasiofahamu utamu wake.

Kwasasa nipo huru na ni kweli Yesu anatenda na Roho Mtakatifu yupo kwa ajili yako endapo utaamua kumpokea! Mungu ni mwema, Mungu anatenda. NAMSHUKURU KWA KUNIOKOA!