Advertise Here

Monday, January 27, 2014

Safu ya James Kalekwa: Ongeza Maana/Thamani kwenye maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea. - Part 4

James Kalekwa
R  -(Realistic). Lengo zuri lazima liwe na uhalisia, ambao huja kutona  na kuangalia hali halisi ya pale ulipo, majukumu na nafasi yako. Mfano mzuri ni huo hapo juu kwenye sifa ya kufikika. Unapoweka malengo juu ya jambo fulani haimaanishi kwamba umeacha kufanya mambo mengine.

Unapoweka malengo ya kihuduma haimaanishi kuwa umeacha kuwa baba au mama (kama Mungu amekupa watoto) kwahiyo usijitoe kwenye wajibu mwingine uliopewa na Mungu, haimaanishi kwamba utastaafu kuwa mme au mke (ikiwa umeoa kama mimi au umeolewa), haimaanishi kwamba wewe si mtoto wa wazazi wako (ikiwa bado wa hai) kwahiyo unawajibu huo.

Lakini jambo jingine la msingi kufahamu, ni je, utapata muda wa kutathmini kazi yako au unaenda kienyeji kienyeji tu, Je, utapata muda wa kufuatilia mavuno hayo na kuyaombea au kuyalea (hakuna umuhimu wa kuzaa kama huwezi kulea), Je kuna mafundisho ya kutosha kwa watu hao? Lazima uzingatie kanuni ya kuwa mkweli juu ya nafsi yako?

Watoto wengine wa Mungu wamekwama sehemu si kwasababu hawana Yesu. Yesu wanae, Roho Mtakatifu yupo pamoja nao na wanaenda mbinguni lakini wamekwama sehemu kwasababu hawana maarifa juu ya jambo hilo. Mtumishi mmoja wa Mungu aliandika, "Upako unaletwa na maombi lakini maarifa ya neno huja kwa kusoma.

Maombi kamwe hayawezi kufuta ujinga na kukupa maarifa. Neno la Mungu limeweka bayana kuwa watu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa Hosea 4:6. Ina maana upako siyo tiketi ya kukuzuia kuangamizwa kama huna maarifa ya neno la Mungu."



T  -(Time bound). Kitu cha kuzingatia katika kuweka malengo ni swala la muda, yaani tamati ya malengo husika. Hii itasakusaidia sana kupima mafanikio na kuweza kufanya tathmini juu ya maendeleo wakati wote wa utekelezaji wa malengo husika. Hebu fikiria nini kilimfanya Bwana Yesu aseme “…hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.", kwasababu malengo yake yalikuwa yamefungwa katika muda wa kuyakamilisha, alikuwa anaujua mwisho tangu mwanzo, kama ni msafiri basi alikuwa anajua stendi au kituo cha mwisho cha safari yake.

Hebu jiulize nini kinaweza kutokea kama malengo yako hayatakuwa na muda wa kuyaona yakitimilika, ”time of their realization.”?. Ngoja nikupe mfano wa kawaida sana ndipo utaelewa nini ninamaanisha, hebu fikiri pamoja na mimi itakuwaje kama mwanafunzi wa darasa la tano akibakia darasa hilo siku zote, bila kuhitimu wala kwenda darasa jingine, siku zote ni darasa la tano?

Ingefika wakati mwanafunzi huyu angechoka na masomo kwasababu hayana mwisho, lakini pia mzazi wake pia angechoka kulipia gharama za kitu kisicho na ukomo au utimilifu. Maana yangu hapa ni kwamba kinachomfanya mwanafunzi wa darasa la tano asome kwa bidii ni kwasababu kuna darasa la sita mbele na la saba yaani kuna kipindi cha kuhitimu hatua husika ya masomo la sivyo asingesoma kwa bidii.

Hebu fikiri nini kitatokea kama inatokea wanawake wanakuwa wajawazito siku zote, bila mwisho!!! Najua wengine wasingetamani kuwa na hali hiyo, kwasababu hakuna kuhitimu hali hiyo, yaani kujifungua.


Mfano wa lengo ambalo ni SMART: Kuihubiri injili kwa watu 1000 nchini Tanzania katika wilaya 4 kwa mwaka mmoja.


Je, lengo hilo ni hususani (Specific)? Ndiyo kwasababu limetaja idadi ya watu,idadi ya wilaya na nchi.

Je, lengo hilo Linapimika (Measurable)? Ndiyo kwasababu ya idadi, eneo la kijiografia (mahali) yaani mwisho wa siku unaweza kukaa chini na kuangalia kama wilaya 4 zimefikiwa na kwa kiasi gani, vilevile kuona kama watu 100 wamefikiwa.


Je, lengo hilo linafikika (Attainable)? Ndiyo, kwa Jiografia ya Tanzania inawezekana kuzifikia wilaya hizo kwa muda huo. Pia unaweza kupata muda wa kujiandaa, kifedha, kimaombi, ujumbe kwani mwalimu mzuri ni mwanafunzi wa kudumu, kwahiyo lazima ujifunze ili ukafundishe.


Je,lengo hilo linauhalisia  (Realistic)? Ndiyo, kwasababu muda unaruhusu kufanya mambo mengine kama maandalizi ya uwanja/ukumbi wa mikutano, mahali pa kufikia, watu wa kushirikiana nao (si unajua huwezi kushirikiana na watu wote na kwa upande mwingine huwezi kushirikiana na kila mtu?) n.k yaani kwa lugha ya kiingereza wanaita "logistics", pia unaweza kuwa na muda wa kutimiza wajibu wako mwingine kama baba/mama (mzazi), kama mme/mke, kama mtoto na vitu vya msingi kama hivyo lakini pia kuna jambo la muhimu ambalo watu wengi hulipuuzia,lakini ni la muhimu sana.

MAPUMZIKO! Mungu baada ya kutenda kazi siku sita alipumzika! Umuhimu wa kupumzika ni kwamba unaporudi tena kwenye utekelezaji, unakuja na nguvu mpya "fresh". Mungu akusaidie kuyaelewa haya na kuyatendea kazi na maisha yako hayatakuwa kama yalivyo, na hayo ndiyo maombi yangu kwa Mungu kwaajili yako msomaji wangu.

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764

Monday, January 20, 2014

Safu ya James Kalekwa: Ongeza Maana/Thamani kwenye maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea. - Part 3

James Kalekwa
Kwahiyo, somo hili litaanza kwenye mzunguko wa malengo na ni wajibu wako kujua kusudi lako, maono na dhamira yako.
 Ninaanza kwa kuamini kwamba (based on the assumption that), wewe, ndugu msomaji wangu, umekwishawekeza muda wako kulitafuta kusudi la Mungu juu ya maisha yako, unayajua maono yako na umeyafikisha kwenye hatua ya dhamira (utume).

Malengo ni nini?
 Binafsi nimekuwa na changamoto kubwa sana kutafuta maana rahisi na ya kueleweka juu ya neno “malengo.” Huwa ninawaambia watu wengi ya kwamba inawezekana kwamba usiwe na maana (definition) ya malengo, lakini ukiyaona ni lazima utayafahamu.

Lakini, huwa ninaamini ya kwamba huwezi kuanza kutenda/kushughulika na kitu, jambo au hali usiyoijua. Na kwa misingi hiyo basi, ninawiwa kujenga ufahamu ndani yako juu ya malengo. Katika mzunguko niliouonyesha hapa awali kwenye taswira, malengo huzaliwa kutoka kwenye dhamira (utume).

Lazima dhamira ikusukume kuumba malengo! Sasa, malengo ni nini basi? Malengo ni ajenda au mahitaji husika/mahususi ambayo mtu fulani hujiwekea kwa kipindi cha muda fulani ili kumzalishia matokeo yanayoonekana, matunda na/au mabadiliko yaliyokusudiwa… hupimika, huweza kufanyiwa tathmini!

Weka malengo kwa vigezo hivi:
 Malengo mazuri huwa na sifa ya “SMART”, neno la kiingereza linalomaanisha nadhifu, -enye uelewa mzuri. Kwahiyo malengo yako yanapaswa kuwa nadhifu, sasa neno smart linabeba maana kubwa sana kwa kila herufi yake:

S   -(Specific), kwanza lazima lengo liwe ni maalum au hususani juu ya jambo, mtu au hali fulani. Kwa mfano mtu anaposema, “Mimi ninataka kupambana na umaskini.”. Ni sawa hilo ni lengo lakini si hususani, yaani halina mwelekeo… Je, mtu huyo anataka kupambana na umaskini wa aina gani (umaskini wa kifikra, kifedha…), Je, anapambana nao katika ngazi ipi? (mtu binafsi, kijiji, familia, nchi…) lazima uainishe.

Na ndivyo ilivyo katika huduma, unaweza kusema nina wito wa kuhubiri injili, ni sawa lakini ni katika ngazi gani? Ni wazi kwamba kuizungukia dunia yote ni jambo ambalo si rahisi (nchi zote, mikoa yote, majimbo yote, wilaya zote, vijiji vyote na kaya zote za dunia.) Si jambo rahisi, ukijaribu utaumia tu na matunda hayatakaa.

Mfano: Lengo langu ni kuihubiri injili nchini Tanzania.
Kumbuka kuwa Tanzania ni nchi kubwa, ina mikoa zaidi ya ishirini na wilaya zake na tarafa, kata, mitaa/vijiji na kaya (familia) kwahiyo unatakiwa kuwa specific zaidi. Kwahiyo waweza kusema, kuhubiri injili nchini Tanzania katika ngazi ya wilaya.

M   -(Measurable), Pili lengo lolote linatakiwa kupimika, Je unaweza kuuona ufanisi, matokeo au matunda ya lengo hilo? Kwa mfano lengo la kuihubiri injili nchini Tanzania katika ngazi ya wilaya…Baada ya muda je unaweza kupima matokeo ya lengo hilo.

Sasa kuna njia mbalimbali za kuyapima malengo yetu, baadhi ya njia ni kuangalia mabadiliko katika maisha ya watu, je, kuna mabadiliko yoyote,njia nyingine ni kuangalia je, idadi iliyokusudiwa imefikiwa? Tukiendelea kuutumia mfano wetu wa kuihubiri injili nchini Tanzania katika ngazi ya wilaya ili tuufanye kuwa SMART; Ili kuweza kupima lengo hilo waweza kusema:
Kuihubiri injili kwa watu 1000 nchini Tanzania katika wilaya 4 (unapaswa kuzitaja wilaya ulizokusudia kuzifikia) kuanzia Januari mpaka Juni.

Je, unaweza kuyapima matokeo ya lengo hilo? Kwasababu unaijua idadi ya watu unaotaka kuwafikia ni watu 1000 na tayari unajua wapi pa kuwapata (wilaya 4, Tanzania) kwa maana hiyo basi ni watu 250 kwa kila wilaya. Kwahiyo hatimaye unaweza kuangalia Je, hizo wilaya 4 zilifikiwa na injili na Je, watu 1000 walifikiwa pia? Hivyo ndiyo kupima malengo!

A    (Attainable), Jambo jingine la tatu na la msingi kufahamu ni kwamba lengo lolote linapaswa kufikika. Hapa unapaswa kuangalia kwamba Je ,ninao uwezo wa kukamilisha lengo hilo kwa kiwango hicho, Je,ninao watu wa kushirikiana nao kufika huko,Je ninahitaji maandalizi ya kimaombi, kifedha, kifursa n.k kiasi gani?

Kuna malengo mengine ukiyatazama unatambua tu kwamba mtu huyu anaota ndoto za mchana, kwa kutumia mfano wetu wa injili nchini Tanzania, unakuta mtu anasema: Lengo langu ni kuihubiri injili nchi yote ya Tanzania kwa mwaka. Hilo ni lengo zuri na lina nia njema lakini Je, unaweza kuifikia nchi yote ya Tazania kwa mwaka? maana yake mikoa zaidi ya 20, yaani wastani wa wilaya 5 kila mkoa, sawasawa na wilaya 100. Mwaka una siku 365, ambapo ni sawasawa na wastani wa siku 3 kila wilaya.

Unaweza? Vipi kuhusu  muda wa kujiandaa? gharama? familia? mapumziko? Usafiri,si unajua wakati mwingine inachukua siku nzima kusafiri toka mkoa mmoja kwenda mwingine? Mikutano hiyo au huduma hiyo utaiandaaje? Je, lengo hilo linafikia?, basi hata kama likifikika halitakuwa na ufanisi.

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764

Friday, January 17, 2014

Papa Francis atimua Makadinali.

MAKADINALI wote isipokuwa mmoja waliokuwa wakisimamia benki ya Vatican wamefutwa kazi na Papa Francis. Waliokumbwa na ‘fagio hilo la chuma’ ni makadinali wanne ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Kadinali Tarcisio Bertone SDB, Kadinali Odilo Scherer kutoka Brazil, Telesphore Toppo kutoka India na Domenico Calcagno kutoka Vatican.

Kadinali Jean-Louis Tauran ambaye ni Mkuu wa Baraza la Upapa linalohusika na Mijadala ya Kidini, amenusurika kwa mujibu wa gazeti la kila wiki la Kikatoliki la The Tablet.

Gazeti hilo lilieleza jana kuwa isipokuwa Calcagno, makadinali hao wote ndio kwanza walikuwa wametimiza miezi 11 tangu wateuliwe katika kipindi cha pili cha miaka mitano, wakiwa wameteuliwa na Papa Benedict XVI muda mfupi kabla ya kujiuzulu.

Benki hiyo ya Vatican ilikumbwa na kashfa ya utakatishaji fedha mwaka 2010 baada ya waendesha mashitaka wa Italia kugundua shughuli zenye shaka zihusuzo fedha chafu ndani ya benki.

Mwenyekiti wa Benki hiyo, Ettore Gotti Tedeschi na naibu wake, Paolo Cipriani walichunguzwa baada ya polisi kukamata euro milioni 23 kutoka kwenye akaunti ya benki hiyo.

Ilidaiwa kuwa ingawa benki hiyo ilikuwa inadai kupambana na utakatishaji fedha, ilivunja sheria kwa kujaribu kuhamisha fedha hizo bila kutambulisha mtumaji wala mpokeaji, au zilikuwa zinatumika kwa shughuli gani.

Tuhuma hizo zilikanushwa kwa nguvu zote na Vatican. Papa Francis ameteua makadinali wengine kuziba nafasi za aliowatimua na kuunda alichokiita Tume ya Makadinali ya Kusimamia Taasisi kwa ajili ya Kazi ya Dini (IOR), ambao ni makadinali Christoph Schönborn (Vienna), Thomas Collins (Toronto); Santos Abril y Castillo´ (St Mary Major) na Kadinali Pietro Parolin (Waziri wa Mambo ya Nje).

- Habari Leo -

Monday, January 13, 2014

Safu ya James Kalekwa: Ongeza Maana/Thamani kwenye maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea. - Part 2

James Kalekwa
Kisa mkasa (Scenario) #2
Mchezo wa mpira wa miguu bila magoli

Kama wewe ni mpenzi, mshabiki au mfuatiliaji wa mchezo wa mpira wa miguu basi uanelewa fika juu ya muundo wa viwanja vya mchezo huo… Moja ya vitu muhimu sana kwenye ujenzi wa kiwanja ni milingoti minne mikubwa isimamayo pande mbili tofauti (zinazokabiliana) za uwanja. Bila shaka umekwisha baini ya kwamba ninazungumza kuhusu magoli.


Hebu fikiri, mchezo wa mpira wa miguu pasipo magoli uwanjani… Je, inawezekana kuwa na mchezo huo? Hata ule mpira wa “mchangani” huwa na magoli, hata kama ni ya mawe au vijiti…

Hauwezi kuwa mpira wa miguu bila magoli. Hebu jiulize wachezaji wangekuwa wanakimbiakimbia uwanjani, wanapiga chenga, wanapeana pasi, wanakaba/wanazuia mashambulizi… ili iweje sasa???

Kuna umuhimu gani wa kuwa na mchezo wa mpira wa miguu pasipo magoli? Lengo kuu la mpira wa miguu ni magoli. Ukiyatoa malengo hayo, umeondoa maana, umeondoa thamani iambatanayo na mchezo huo.


Kabla hatujachukua hatua kubwa sana katika kujifunza haya, ninaomba tujenge uelewa wa pamoja juu ya maswala kadhaa ambayo yana uhusiano wa moja kwa moja na maswala mazima ya malengo.


Kusudi – ni sababu kuu ya kuwepo kwako. Hii hujibu swali la “Kwanini ninaishi?” mfano: Ninaishi ili kuudhihirisha utukufu wa Mungu kwenye kizazi changu.


Maono – ni taswira/picha kubwa uionayo juu ya mwisho wa maisha yako. Ni mkusanyiko wa mwisho wa maisha yako. Hii hujibu swali la “ninakwenda wapi?” mfano: … Kumtukuza Mungu kwa kufanya ugunduzi, uvumbuzi na utatuzi chanya wa mahitaji ya kizazi changu.



Dhamira – ni namna gani utafanya ili kuyafikia maono hayo kivitendo. Hii hujibu swali la “Namna gani nitatekeleza?” Mfano: … Kufungua taasisi ya utafiti wa uwezo wa mwanadamu na uelimishaji wa vijana.

N.B Unaweza kuwa na dhamira zaidi ya moja… Hakuna ukomo ilimradi tu dhamira zinafanikisha ufikiaji wa maono yako.



Malengo/Mipango – ni kuweka namna/njia za kivitendo na zinazopimika ili kufanikisha dhamira yako/zako Mfano: … Kufanya usajili wa taasisi yangu ifikapo March 28 ili kuanza utendaji rasmi.



Mkakati – ni mchanganuo wa hatua kwa hatua na uratibu wa rasilimali ili kufanikisha malengo yako. Hii hujibu maswali mengi “Nifanye nini, nifanye wapi, wakati gani?...” Mfano:


Mkakati wa usajili wa taasisi:

#
Jukumu
Yatakayohitajika
Kinachotarajiwa
Muhusika
Lini
Hali ya utendaji

Kuandika katiba ya taasisi.

Katiba ya taasisi
Frida
1-23 January, 2014
Inaendelea

Kualika wajumbe waanzilishi na kuwashirikisha wazo

Kikao/mkutano wa kwanza
James
28 January, 2014
Bado

Kufanya shughuli za usajili wa taasisi

Cheti cha usajili
Charisa & Joshua
19 February, 2014
















Kutoka kwenye mkakati huu unaweza kutengeneza bajeti (maelezo juu ya uratibu wa rasilimali fedha).


Lengo la kuainisha, walau kwa ufupi tu, tofauti ya mambo hayo ni ili uwe na uhakika na kitu gani unakiendea na unapaswa kufanya. Ni muhimu sana ufahamu ya kwamba kusudi ndilo huwa sababu ya maono; maono huzaa dhamira (utume) na dhamira ndiyo huleta malengo ambayo huzaa mikakati tayari kwa utekelezaji. Ili kurahisisha uelewa juu ya mambo haya, tazama na kujifunza kwenye Taswira ifuatayo:


Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764