Advertise Here

Tuesday, February 19, 2013

Namna ya Kumtumia Roho Mtakatifu kama Msaidizi kupitia kazi zake.

Yohana 14:16-18 … Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni, wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”.

Katika somo hili nataka kuandika juu ya kazi za Roho Mtakatifu na kukuonyesha namna unavyoweza kumtumia Roho Mtakataifu kama Msaidizi kupitia kazi zake. Labda niseme kwa lugha hii, kama unataka kuona msaada wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yako, ni lazima kwanza uzijue kazi zake, maana kazi zake ndizo zinazotuonyuesha maeneo ya msaada wake, kazi zake ndizo zinazofafanua kwa namna gani Roho Mtakatifu ni Msaidizi.

Roho Mtakatifu ni nani?
Roho Mtakatifu ni Mungu, mwenye nguvu zote, maarifa yote, anayepatikana kila mahali. Yeye anayo nafsi na ameamua kuishi ndani ya mwili wa mwanadamu. Kusudi kubwa la ujio wake ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu kwenye ulimwengu huu wa mwili, ili kumsaidia kuishi katika mapenzi ya Mungu.

Roho Mtakatifu amemamua kuishi ndani ya mwili wa mtu kwa sababu, Mungu hana namna ya kutawala kwenye ulimwengu wa kimwili bila kuwa na mwili wa damu na nyama, kwa kuwa yeye ni Roho (Yohana 4:24). Hivyo hana budi kuingia kwenye mwili wa mtu na kufanya makao yake hapo, ili kutawala na kumuongoza mwanadamu katika mapenzi yake. (Yohana 14:23, Yohana 14:18, Ufunuo 3:20, 1Wakorinto 3:16-17, 6:19).

Kinachotusaidia kujua kwamba Roho Mtakatifu ana nafsi, ni tabia zake, maana kwenye kila nafsi kuna hisia, nia, kumbukumbu, akili nk. Baadhi ya sifa na tabia za Roho Mtakatifu ni; anapatikana kila mahali (Omnipresence), Zaburi 139:7, ana maarifa/anajua yote (Omniscient, Intelligence), 1 Wakorinto 2:10-11, ni mwenye nguvu zote/wa umilele (Omnipotent), Mwanzo 1:2, ni Mtakatifu, Luka 11:13, ana hisia (Waefeso 4:30, Mwanzo 6:3) – Wala msimuhuzunishe Roho wa Mungu…, Roho yangu haitashindana na Mwanadamu milele, ana nia (will), 1Wakorinto 12:11 – Hutenda kazi kama apendavyo.

Kazi za Roho Mtakatifu
  • Kufundisha, Mwalimu (Yohana 14:26) … Atawafundisha yote…
  • Kuongoza, Kiongozi (Warumi 8:14, Yohana 16:13) – Atawaongoza awatie kwenye kweli yote, wote wanaoongozwa na Roho hao ndio … Mfano (Matendo ya Mitume 13:4, Acts 8:29)
  • Ni mfunuaji wa mambo/mafumbo/siri za Mungu (1Wakorinto 2:10) – Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote. Usipoteze muda kumtaka Mungu akufunulie siri zake, wewe mwambi Roho Mtakatifu hiyo ndiyo kazi yake.
  • Muombezi (Warumi 8:26) – Roho hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.
  • Mtoa/mpasha habari za mambo yajayo (Yohana 16:13f) – Na mambo yajayo atawapasha habari yake.
  • Ni msemaji wa mambo ya Mungu/Yesu (Yohana 15:26, 2 Petro 1:21) – Yeye atanishuhudia (he will speak about me), Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.
  • Ni mtetezi/msemaji wa mambo yetu (Marko 13:11) – Kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu.
  • Ni mkumbushaji wa yale uliyojifunza au uliyoagizwa na Mungu (Yohana 14:26)… Atawakumbusha yote niliyowaambia.
  • Kutia/kuwapa nguvu watu wake nguvu/uwezo (Matendo1:8) – Lakini mtapokea nguvu akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu…
  • Kuuhakikisha (convict, make aware, sadikisha) ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu (Yohana 16:8) e.g unajuaje kwamba kuna hukumu? Warumi 8:16
Naam kazi hizi za Roho Mtakatifu zinatufikisha mahali pa kujua kwamba jukumu lake kubwa ni kuwa Msaidizi wa mwanadamu. Kufanyika msaada wa mwanadamu katika mambo hayo hapo juu pale mwanadamu atakapohitaji msaada huo. Hivyo ni jukumu lako kumpa nafasi kwa kuboresha mahusiano yako na yeye ili akusaidie. Hata hivyo Roho Mtakatifu kuitwa Msaidizi haina maana kwamba ndio umvunjie heshima, bali fahamu kwamba, Roho Mtakatifu ni Msaidizi kwa namna ambayo bila yeye mimi na wewe hatuwezi kutenda neno lolote.

Kazi hizi zinatupa kujua kwamba Roho Mtakatifu yupo tayari kutusaidia katika kila eneo la maisha yetu. Ni jukumu letu kumpa nafasi hiyo na kutambua kwamba bila msaada wake sisi hatuwezi lolote. Watu wengi leo hawaoni msaada wa Mungu kwao kwa sababu ya kutokumpa Roho Mtakatifu nafasi ya kuwasaidia katika maisha yao na pia kwa kutokujua maeneo ya kumtumia Roho Mtakatifu kama Msaidizi.

Je, unahitaji msaada wa Roho Mtakatifu eneo gani la maisha yako?, ni ndoa, kazi, madeni, huduma, kanisa, utawala nk mpe nafasi akusaidie, akufundishe na kukuongoza katika kweli yote. Kumbuka yeye ni Mungu ambaye ni Mwalimu na Kiongozi pasina yeye mimi na wewe hatuwezi neno lolote. Unataka kumjua Mungu, kuwa na maombi yenye matokeo mazuri na kufanikiwa katika maisha yako kiroho na kimwili pia mwambie Roho Mtakatifu akusaidie.

Msaada wa Roho Mtakatifu hauna mipaka maadam unahitaji msaada katika yale ambayo ni mapenzi ya Mungu. Hivyo haijalishi unapita katika jambo gani mpe nafasi Roho Mtakatifu akusaidie. Na ili uweze kuthamini msaada wa Roho Mtakatifu jifunze siku zote kufikiri kwa dhana kwamba bila msaada wake wewe huwezi lolote, na kwa sababu hiyo utaona umuhimu wa yeye kukusaidia katika maisha yako.

Usisubiri mambo yako yaharibike au usiachague mambo unayofikiri magumu ndio umshirikishe akusaidie, yeye anataka kuwa Bwana wa maisha yako, akusaidie kwa kila kitu hata mambo madogo kabisa kwenye maisha yako. Kina-muumiza Mungu kuona watoto wake chini ya jua wanahangaika katika maisha yao, wakati yeye amemleta Roho Mtakatifu ili awasaidie katika maisha hayo. Tumia vizuri fursa ya Roho Mtakatifu sasa maadam anapatikana, kuna wakati hatapatikana.

Neeme ya Kristo iwe Nawe!

Imeandikwa na Mwl. Patrick Sanga
0715 816800, 0755 81680

Kifo cha Padri Evarist Mushi, Jukwaa la kikristo Mbeya latoa Tamko.

JUKWAA la Kikristo Tanzania (TCF) katika Mkoa wa Mbeya, limetoa tamko la kuitahadharisha Serikali na kuitaka ichukue hatua za haraka za kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote waliohusika na mauaji ya Padri, Evarist Mushi.

Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliohudhuriwa na maaskofu, mapadri na wachungaji, Katibu wa Jukwaa hilo, Askofu Damianus Kongoro, alisema kuna mambo yanayotendeka waziwazi yakiwa na athari kubwa kwa amani na ustawi wa nchi na wananchi kwa jumla.

Alisema mambo hayo ni pamoja na uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa wazi unaofanywa na baadhi ya watu wasiopenda amani lakini hakuna hatua za makusudi zinazochukuliwa na Serikali kuwashughulikia.

Askofu Kongoro alisema kuuawa kwa wachungaji, mapadri na maaskofu kuanza kutoa matokeo mabaya.

Alisema hatua zinazochukuliwa na Serikali haziridhishi wala kukidhi matakwa ya wananchi wapenda amani na badala yake, Serikali inakaa kimya au inachukua hatua ambazo kimsingi, hazitatui tatizo.


- Mwananchi -

Kanisa lachomwa Moto Zanzibar.

Taarifa za kuaminika Zilizorushwa na Radio Wapo katika kipindi chake cha Patapata leo asubuhi, ni kwamba watu wasiojulikana wamevamia kanisa moja linalojulikana kama SHALOM huko Zanzibar na kulirushia kitu kama bomu kilicholipuka moto japo majirani waliamka na kuuzima moto huo kabla haujaleta madhara makubwa.

Tukio hilo limetokea leo Alfajiri ya leo na Hakuna chombo cha dola kilichowahi kufika eneo hilo la tukio. Tukio hili limetokea ikiwa ni Siku chache tu baada ya Kuuliwa Padri Evarist Mushi kwa kupigwa Risasi huko huko Zanzibar.
Kwa Mujibu wa Kamishna wa Polisi wa Mjini Zanzibar Musa Ali Musa, kuna baadhi ya Vitu vya Kanisa hilo vimeungua.

Monday, February 18, 2013

Watu Watatu washikiliwa na Jeshi la Polisi kwa Mahojiano Juu ya Kifo cha Padri Evarist Mushi.

mushi
Marehemu Padri Evarist Mushi enzi za Uhai Wake
Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya St. Joseph, Shangani, Unguja ameuwawa Jana mnamo saa moja asubuhi katika eneo la Beit-El-Ras karibu na kanisa la Katoliki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud imeeleza kuwa kutokana na tokeo hilo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwatambua wale wote waliohusika na tukio hilo kwa ajili ya kuwachukulia hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria.

Aboud amesema kuwa wakati uchunguzi huo unaendelea, Serikali inawaomba wananchi wote kuwa watulivu na kuliachia Jeshi hilo la Polisi kutekeleza wajibu wake.

Aidha Serikali imetoa mkono wa pole kwa familia na wanafamilia wa marehemu pamoja na waumini wa kanisa hilo kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.

Wakati huo huo Raisi Jakaya Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Evarist Mushi wa Parokia ya Minara Miwili ya Kanisa Katoliki mjini Zanzibar, mauaji yaliyotokea Zanzibar.

Rais Kikwete ametoa pole za rambirambi kwa Baba Askofu Augustino Shayo wa Jimbo Katoliki, Zanzibar, Maaskofu wote nchini na waumini wote wa Parokia ya Minara Miwili kwa msiba huo mkubwa uliowakuta.

Rais kikwete amemwambia Baba Askofu Shayo. ”Napenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha Mpendwa Marehemu Padri Evarist Mushin a kuwa msiba huu ni wa kwetu sote.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Nimeligiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.”

“Aidha, nimewaagiza Jeshi la Polisi washirikiane na vyombo vingine vya Usalama nchini na mashirika ya upepelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji haya.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka ukweli wake ujulikane ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina.”

Vile vile, Rais Kikwete amewataka waumini wa Kanisa katoliki na wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali inashughulikia suala hili na kuwa hakuna mtu wala watu ama kikundi cha watu kitachoruhusiwa kuvuruga amani ya nchi yetu.

WATU WATATU WASHIKILIWA NA POLISI
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjnfyYrTkIHYZBrbeswwAAznTUERbZYwcmm9JXuy9m5xI7DYDm9OGdqczB7EbO6fqSutexpIhyphenhyphenF7Me66puAKZpXyKLi89iar4YGqyO9KfWZ8l_JNMgn_uHx5aKMT0qSao_5Zvduazll3o25/s1600/_DSC3465.JPG 
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjPoWQqtVodAGRn26XHWVtebs7hrs_ojXmboADVkWxv0wQugoFa4L_BJbqm2MeJPvbWXjezO7gYZW2uUoc04Nt64Rw-TshFPCzZ-yt5REw-PuRuSm0EOT5JkGcpKednr0FeDOu5ohM-tMEI/s1600/_DSC3469.JPG

Saturday, February 16, 2013

Dr. Nchimbi kuwasaka wale wote walioanzisha vurugu Mkoani Geita.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dr. emmanuel Nchimbi
Serikali imemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Hezron Kigondo, kuongoza uchunguzi kubaini watu waliohusika na vurugu zilizosababisha mauaji ya Mchungaji wa Kanisa la Pentecoste Assemblies of God Tanzania (PAGT), Mathayo Kachila, ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo alipotembelea mkoani geita na kukutana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo na viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo Siku chache zilizopita. Alisema serikali inalaani vurugu hizo, ambazo alisema iwapo zitafumbiwa macho zinaweza kulipasua Taifa vipande vipande.
 
Waziri Nchimbi alisema anashangazwa na matukio hayo kutokea hivi sasa kwa kuwa hapo awali, haukuwapo kwa Watanzania utamaduni na chuki na vurugu.
 
Kutokana na hali hiyo, alisema huenda matukio hayo yakawa ni mbinu za watu wachache zinazolenga kuibua vurugu kwa kutumia kivuli cha dini kuliangamiza taifa, kitendo ambacho alisema serikali haiwezi kukikubali.
 
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Nchimbi alisema itawasaka kwa hali na mali watu wote waliohusika na vurugu hizo na kwamba, tayari watuhumiwa wawili wameshakamatwa.
 
Akiwa mkoani hapo, Waziri Nchimbi alikutana na kamati ya ulinzi na usalama iliyo chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Mh. Said Magalula.
 
Baadaye, alikutana na wawakilishi wa viongozi wa dini ya Kikristo, wakiwamo Mapadri na Maaskofu kabla ya kukutana na viongozi wa dini ya Kiislamu, wakiwamo Masheikh kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
 
Waziri Nchimbi alikutana na viongozi hao kwa lengo la kusikiliza maoni na mapendekezo yao juu ya kupatikana ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro uliosababisha vurugu Mkoani humo.