Marehemu Padri Evarist Mushi enzi za Uhai Wake |
Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya St. Joseph,
Shangani, Unguja ameuwawa Jana mnamo saa moja asubuhi katika eneo la
Beit-El-Ras karibu na kanisa la Katoliki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud imeeleza kuwa kutokana na tokeo
hilo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeliagiza Jeshi la Polisi kufanya
uchunguzi wa kina ili kuwatambua wale wote waliohusika na tukio hilo kwa
ajili ya kuwachukulia hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria.
Aboud amesema kuwa wakati uchunguzi huo unaendelea, Serikali
inawaomba wananchi wote kuwa watulivu na kuliachia Jeshi hilo la Polisi
kutekeleza wajibu wake.
Aidha Serikali imetoa mkono wa pole kwa familia na wanafamilia wa
marehemu pamoja na waumini wa kanisa hilo kuwa wastahamilivu katika
kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
Wakati huo huo Raisi Jakaya Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa
Padri Evarist Mushi wa Parokia ya Minara Miwili ya Kanisa Katoliki mjini
Zanzibar, mauaji yaliyotokea Zanzibar.
Rais Kikwete ametoa pole za rambirambi kwa
Baba Askofu Augustino Shayo wa Jimbo Katoliki, Zanzibar, Maaskofu wote
nchini na waumini wote wa Parokia ya Minara Miwili kwa msiba huo mkubwa
uliowakuta.
Rais kikwete amemwambia Baba Askofu Shayo. ”Napenda kuwahakikishia
kuwa tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha Mpendwa Marehemu Padri
Evarist Mushin a kuwa msiba huu ni wa kwetu sote.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nimeligiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya
nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina
na wa haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na
kuwakamata ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.”
“Aidha, nimewaagiza Jeshi la Polisi washirikiane na vyombo vingine
vya Usalama nchini na mashirika ya upepelezi ya nchi rafiki katika
kufanya uchunguzi wa mauaji haya.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka ukweli wake ujulikane ili kama kuna
jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina.”
Vile vile, Rais Kikwete amewataka waumini wa Kanisa katoliki na wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali inashughulikia suala hili na kuwa hakuna mtu wala watu ama kikundi cha watu kitachoruhusiwa kuvuruga amani ya nchi yetu.
WATU WATATU WASHIKILIWA NA POLISI