Kadinali Timothy Dolan wa Kanisa Katoliki |
Kadinali Timothy Dolan ambaye ni mmoja wa maaskofu wanaotarajiwa
kumrithi Papa Benedict wa XVI aliyejiuzulu hivi karibuni amesema kuwa
kuanzia sasa watu wote wanaotarajiwa kuwa mapadri na maaskofu watakuwa
wanachunguzwa tabia zao tokea utotoni.
Matamshi hayo yamekuja baada ya
mchungaji mwingine mmoja wa mji wa Milwaukee ambao ni moja ya miji
mikubwa ya jimbo la Wisconsin nchini Marekani kuwatumia vibaya kijinsia
watoto wadogo. Kwa upande wake, Frank Lokoko, mtaalamu wa masuala ya
sheria wa mji wa Milwaukee amesema kuwa, Kadinali Dolan alihojiwa kwa
muda wa masaa matatu na mawakili wa watoto waliotumiwa vibaya kijinsia
na makasisi wa mji huo.
Amesema, Timothy Dolan alikuwa Askofu mkuu
katika kipindi cha miaka ya 2002 hadi 2009 na ni mmoja wa makadinali 10
wanaowania nafasi ya kurithi kiti cha Papa Benedict wa XVI.
Ijapokuwa
limekuwa ni jambo la kawaida kwa wakuu wa Kanisa Katoliki kufanya
vitendo vichafu vya kijinsia huko Magharibi, lakini kuongezeka vitendo
viovu vya ufisadi wa kimaadili na ubadhirifu wa fedha, vitendo ambavyo
vimewahusisha hata viongozi wa ngazi za juu kabisa wa kanisa hilo, ni
jambo ambalo limeyatumbukiza makanisa hayo ya Magharibi katika mgogoro
mwingine mkubwa zaidi, tangu ule wa karne za kati wakati kanisa hilo
lilipofanya mauaji makubwa ya watu kwa imani za kidini.
Watu wengi hivi
sasa wamekuwa wakiyapa nguvu madai kuwa maaskofu wa kieneo na hata wa
Vatican kwenyewe wanafanya kwa siri vitendo viovu vya udhalilishaji wa
kijinsia na ni kwa sababu ndio maana maaskofu wa chini nao wakapata
nguvu za kuwatumia vibaya hata watoto wadogo. Hali hiyo imejitokeza
katika hali ambayo tangu miaka mingi nyuma, wachungaji walikuwa na
heshima kubwa kati ya wananchi wa Magharibi.
Hata hivyo imani hiyo ya
watu imepungua hasa baada ya kugunduliwa kashfa za kimaadili za wakuu wa
Kanisa tena basi dhidi ya watoto wadogo. Takwimu zinaonesha kuwa watu
wenye imani na Kanisa hasa kati ya wanawake, inazidi kupungua huko
Magharibi huku idadi ya wanaokwenda kanisani nayo ikizidi kushuka chini.
Yamkini majibu ya sababu za kushuhudiwa hali hiyo yakawa yamo ndani ya
matamshi ya Kadinali Martini ambaye hakuona tabu hata kidogo kutangaza
malalamiko yake kuhusiana na utendaji mbaya wa Kanisa Katoliki. Kadinali
Martini wa Milan, Italia, alikuwa askofu kwa muda wa miaka 20 na hata
alitajwa kuwa ndiye Papa wa baadaye wa Kanisa Katoliki.
Alisema miaka
michache kabla ya kufariki kwake dunia na katika mahojiano yake ya
mwisho kwamba, Kanisa Katoliki liko nyuma kwa miaka 200. Alisema kama
mabadiliko ya kimsingi hayatafanyika katika Kanisa Katoliki, basi kizazi
kipya kitajitenga na kanisa hilo na kwamba mabadiliko hayo inabidi
yaanze kwa Papa mwenyewe na kufuatiwa na maaskofu.