Millioni 200 kutumika kwa ajili ya Tamasha la Pasaka Mwaka huu.
|
Bw. Alex Msama |
KIASI cha Sh. Milioni200 kitatumika kwa
ajili Tamasha la Pasaka mwaka huu, ambalo kwa mara ya kwanza
litafanyika katika mikoa saba tofauti.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya
Tamasha hilo, Alex Msama alisema fedha hizo zitatumika kwa masuala
mbalimbali ikiwemo kulipa wasanii, misaada katika masuala mbalimbali ya
kijamii na gharama za kawaida mahali watakapofanya maonesho.
“Kila mwaka Tamasha la Pasaka linafanyika
katika mikoa miwili, kwa maana ya Dar es Salaam na mkoa mwingine
tutakaouchagua, lakini mwaka huu kwa mara ya kwanza litafanyika katika
mikoa saba.
“Kwa hiyo gharama zake kidogo
zitaongezeka na tunakadiria kwa mikoa yote hiyo kiasi cha Sh. Milioni
200 kitatumika maana tutakuwa na wasanii zaidi ya 30, tunaamini wengi
watajumuika nasi kulipa viingilio ili kuwezesha dhamira yetu ya kupeleka
ujumbe kwa njia ya muziki ufike,” alisema Msama.
Alisema tayari wamekubaliana Machi 31
mwaka huu ambayo ni siku ya Pasaka tamasha lifanyike Dar es Salaam,
lakini baada ya hapo mikoa mingine itakayofuata wataitangaza.
Msama alisema dhamira yao safari hii
kwenye tamasha hilo ni kuhamasisha umoja, amani na mshikamano miongoni
mwa jamii ya kitanzania.
“Kila mwaka huwa tuna jambo ambalo
tunaliangazia, safari hii tumeamua kuwa tamasha letu litasisitiza amani
na upendo,” alisema Msama.
Tamasha la mwaka jana baadhi ya waimbaji
mahiri waliokuwepo ni Rose Muhando, Rebecca Malope, Christina Shusho,
Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Atosha Kissava, Ephraim
Sekeleti na kundi la Glorious Celebration.
Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival, Mwinjilisti Faraja Ntaboba
kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zilikuwa miongoni mwa
burudani zilizokuwepo siku hiyo.