JUKWAA la Kikristo Tanzania (TCF) katika Mkoa wa Mbeya, limetoa
tamko la kuitahadharisha Serikali na kuitaka ichukue hatua za haraka za kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote waliohusika na mauaji
ya Padri, Evarist Mushi.
Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliohudhuriwa na maaskofu, mapadri na wachungaji, Katibu wa Jukwaa hilo, Askofu Damianus Kongoro, alisema kuna mambo yanayotendeka waziwazi yakiwa na athari kubwa kwa amani na ustawi wa nchi na wananchi kwa jumla.
Alisema mambo hayo ni pamoja na uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa wazi unaofanywa na baadhi ya watu wasiopenda amani lakini hakuna hatua za makusudi zinazochukuliwa na Serikali kuwashughulikia.
Askofu Kongoro alisema kuuawa kwa wachungaji, mapadri na maaskofu kuanza kutoa matokeo mabaya.
Alisema hatua zinazochukuliwa na Serikali haziridhishi wala kukidhi matakwa ya wananchi wapenda amani na badala yake, Serikali inakaa kimya au inachukua hatua ambazo kimsingi, hazitatui tatizo.
- Mwananchi -