Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dr. emmanuel Nchimbi |
Serikali imemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi
(SACP), Hezron Kigondo, kuongoza uchunguzi kubaini watu waliohusika na
vurugu zilizosababisha mauaji ya Mchungaji wa Kanisa la Pentecoste
Assemblies of God Tanzania (PAGT), Mathayo Kachila, ili kuwafikisha
mbele ya vyombo vya sheria.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo
alipotembelea mkoani geita na kukutana na kamati ya ulinzi na usalama ya
mkoa huo na viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo Siku chache zilizopita. Alisema serikali
inalaani vurugu hizo, ambazo alisema iwapo zitafumbiwa macho zinaweza
kulipasua Taifa vipande vipande.
Waziri Nchimbi alisema anashangazwa na matukio hayo kutokea hivi sasa
kwa kuwa hapo awali, haukuwapo kwa Watanzania utamaduni na chuki na
vurugu.
Kutokana na hali hiyo, alisema huenda matukio hayo yakawa ni mbinu za
watu wachache zinazolenga kuibua vurugu kwa kutumia kivuli cha dini
kuliangamiza taifa, kitendo ambacho alisema serikali haiwezi kukikubali.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Nchimbi alisema
itawasaka kwa hali na mali watu wote waliohusika na vurugu hizo na
kwamba, tayari watuhumiwa wawili wameshakamatwa.
Akiwa mkoani hapo, Waziri Nchimbi alikutana na kamati ya ulinzi na usalama iliyo chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Mh. Said Magalula.
Baadaye, alikutana na wawakilishi wa viongozi wa dini ya Kikristo,
wakiwamo Mapadri na Maaskofu kabla ya kukutana na viongozi wa dini ya
Kiislamu, wakiwamo Masheikh kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Geita.
Waziri Nchimbi alikutana na viongozi hao kwa lengo la kusikiliza maoni
na mapendekezo yao juu ya kupatikana ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro
uliosababisha vurugu Mkoani humo.