HATIMAYE Jiji la Dar es Salaam limeshinda katika mchakato wa
kuchagua mkoa wa kwanza kati ya saba ambayo Tamasha la Pasaka mwaka huu
litafanyika.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa Kamati
ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, ilisema kamati yake
iliendesha kura za maoni kwa mashabiki wao, wa eneo lipi tamasha hilo
lifanyike.
“Tulifanya kura za maoni kwa njia ya simu za mkononi, pia tulikuwa na
vipindi maalumu kwenye baadhi ya redio kwa mashabiki kutoa maoni yao.
“Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma na Mwanza ilikuwa ikichuana
vikali katika kupata mahali ambapo tamasha litafanyika, maana tulikuwa
bado hatujatangaza.
“Lakini leo tumechagua Dar es Salaam, ambapo zaidi ya mashabiki 15,000
walichagua tamasha lifanyike Dar es Salaam, mashabiki 13,000 walitaka
lifanyike Mbeya, mashabiki 7,000 walitaka Mwanza na mashabiki 3,000
walitaka Dodoma,” alisema Msama.
Alieleza kuwa hivi sasa wanatazama mkoa upi lifanyike Jumatatu ya Pasaka na siku zingine zitakazofuata.
“Siku yenyewe ya Pasaka tushapata kwamba ni Dar es Salaam, sasa
tunajipanga kwa siku zingine, maana mwaka huu tunataka mikoa saba
tufanye tamasha letu,” alisema Msama na kuongeza kuwa kwa Dar es Salaam
litakuwa Machi 31.
Pia alisema bado wanaendelea na mazungumzo na wasanii mbalimbali kwa ajili ya kushiriki tamasha la mwaka huu.
- Elizabeth John -