DINI mpya iitwayo Matengenezo inayozuia
waumini wake kwenda sekondari na hospitali, imeingia wilayani Kakonko
mkoani Kigoma. Inakataza waumini wasiende sekondari na hospitali, kwa
madai kuwa Biblia inawakataza kufanya hivyo. Mkuu wa Wilaya hiyo, Peter
Toima alibaini hayo juzi katika Kijiji cha Rumashi Kata ya Nyabibuye
wilayani humo.
Alikuwa kwenye ziara katika shule za
sekondari za wilaya hiyo mpya, ambapo kwanza aligundua wanafunzi wengi
hawajaripoti shuleni kuanza Kidato cha Kwanza.
Toima alipohoji kulikoni hawajaripoti
katika shule walizopangiwa huku wale walioandikishwa darasa la kwanza,
pia nao hawaripoti, alielezwa kuwa sababu za kiimani zinazokataza
wengine kusoma.
Mkuu huyo wa Wilaya alikatiza ziara yake
na kuanza msako wa kuwasaka wanafunzi hao ambao hawajaripoti shuleni
pamoja na waumini wa dini hiyo ya Matengenezo.
Alisema aliamua kufanya hivyo, kwa
sababu dini hiyo inawakosesha watoto haki yao ya msingi na kukiuka
sheria za nchi, kwani ni haki ya kila mtoto kupata elimu.
Katika msako huo, aliongozana na Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo na watendaji wa Halmashauri wakiwemo
Maofisa Elimu Msingi na Sekondari.
Viongozi hao walifika katika familia ya
Mchungaji wa Kanisa la Matengenezo, Medad Laurent (40). Baada ya kufika
hapo, Toima aliwakuta mabinti watatu waliochaguliwa kujiunga na Kidato
cha Kwanza mwaka huu lakini hawajaenda, kutokana na kile Mchungaji huyo
alichodai kuwa sekondari wanafundisha uongo, kinyume na maandiko
matakatifu yanavyosema.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya
aliamuru Mchungaji huyo na mabinti zake wawili, kushikiliwa na Jeshi la
Polisi huku utaratibu wa kuwapeleka mabinti hao shule ukiendelea. Pia,
aliamuru Mchungaji huyo kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za
elimu.
Siku iliyofuata Toima na Kamati ya
Ulinzi na Usalama, walifanya kikao na kukubaliana kuwapeleka mabinti
hao, Naomi Medard (16) na Anastazia Medard (14) katika shule za
sekondari zenye mabweni kwa kuwatenganisha ili wasiendelee kusambaza
sumu ya kukataa shule.
Naomi alipelekwa Shule ya Sekondari
Nyamtukuza na Anastazia Shule ya Sekondari Kanyonza. Hata hivyo, katika
familia hiyo binti mmoja Beatrice Merdad (19) alibaki nyumbani kwa madai
kuwa hakuchaguliwa kuendelea na Kidato cha Kwanza.
Alidai kuwa hata angechaguliwa,
asingeweza kuendelea kwani wanafundisha uongo na siku akifa hatakuwa na
la kwenda kumwambia Muumba wake, kutokana na elimu hiyo ya dunia
kuwapotosha.
Katika familia hiyo ya watoto saba,
wawili walifariki dunia kutokana na kutokwenda hospitali. Mama wa watoto
hao, Julitha Sebastian (39) alipohojiwa baada ya mtoto wake mchanga
kuonekana kudhoofika na nywele kubadilika rangi, alisema kuwa dini yao
haiwaruhusu kwenda hospitali.
Alisema hakuwahi kumpatia mtoto huyo
chanjo ya aina yoyote wala hakuwahi kujifungulia hospitali. Kuhusu
watoto wake waliokufa, alisema Biblia inasema “Ni heri wafao katika
Bwana”.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya
hiyo, Florida Gandye alisema waumini wa kanisa hilo, awali walikuwa
Wakristo Wasabato, kisha wakajiengua na kuanzisha dini hiyo yenye imani
za ajabu.
- Habari Leo -