Advertise Here

Tuesday, March 12, 2013

Kuna Ushindi katika Kusamehe.

 
Bwana Yesu asifiwe sana, namshukuru Mungu kwa fursa hii tena ninapokukaribisha katika somo letu linalohusu Msamaha.

Ndugu yangu, Dhana ya Kusamehe inaweza kufasiliwa kama hali ya huachilia, yaani kupuuza, hili ni jambo ambalo kila mmoja wetu analijua na pengine kila mmoja wetu limemkuta, aidha kwa kusamehe au kusamehewa! KWA UFUPI, GHARAMA YA MSAMAHA HUWA NI YA ANAYESAMEHE, JAPO ANAYELIPA NI ALIESAMEHEWA.
Naomba unielewe vizuri, unaposamehe, kwako huna dukuduku, ila aliyesamehewa hubaki na maswali aghalabu kama hakutegemea kusamehewa.Hii inadhihirisha kuwa, mara unaposamehe, anayesamehewa anabaki na maswali kichwani kuwa kweli kasamehewa au la, na hii ndiyo gharama halisi.

Wengine husema, katu siwezi kusamehe, na hata nikisamehe siwezi kukusahau, lakini Biblia inatueleza (Mathayo 6:12)"Msipowasamehe wengine Makosa yao,wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu" Hii ina maana gani? Hapa Mungu anatudhihishia kuwa, Kanuni anayotumia katika kukusamehe, ni ile ile uliyotumia katika kuwasamehe wengine; Yaani kwamba, kama hujawasamehe wengie, hata wewe huwezi kusamehewa

Ni wazi kuwa kumsamehe mtu aliyekuumiza sio jambo la mzaha na wala si suala la dogo lakini hapo hapo ndipo Mungu anapotaka kuona utu wako na uvumilivu wako. Wengine machoni pa watu hudiriki kusema "Yameisha" mara nyingi baada ya USULUHISHO, lakini ndani ya mioyo yao bado hajasamehe.

Rafiki, naomba ujue kuwa, kabla mtu hajakuudhi, kuna nguvu inayokuwa nyuma yake ambayo humwongoza ili akuumize! Usipojua hilo, utaangamizwa na nguvu hiyo, kwasababu nguvu hiyo ni ya roho iliyotumwa kukuangamiza hata kupitia hasira, chuki na kutokusamehe.
Angalia mfano huu wa gari linapomgonga mtu serikali haishtaki gari bali anayeshtakiwa ni dereva. Hii ina maana kwamba, anayekukosea huwa ana anayemhimiza kufanya hivyo! Vivyohivyo ukiumizwa unatakiwa uangalie ile nguvu iliyopo nyuma ya aliyekuumiza. Kimsingi kuna nguvu inayotenda kazi nyuma ya aliyekuumiza na usipoijua hiyo nguvu utajikuta unashindwa kusamehe.

Usichoke kusamehe, kwa kuwa neno linasema samehe saba mara sabini tena kwa kwa kutwa, tena linaongeza, usichoke kutenda wema maana Bwana atatulipa tusipozimia mioyo, Naomba unielewe vizuri hapa, Hii inamaana kuwa, kwanza una kheri wewe uliyepewa ufunuo hata ukajua kuwa yule kakutendea uovu, je si kazi yako kumsamehe na ndipo uanze kumuelimisha?
Hili linaenda hata Kwa wazazi, nawaombeni watoto wenu wanapowakosea wakati mwingine mtumie njia mbadala kuwaadhibu na siyo kuwachapa tu, kwani huyu pengine hajui kama ametenda kosa na pengine ni bahati mbaya tu, kwani sisi kama tungekuwa tunaadhibiwa mara tutendapo dhambi hata kwa kiboko kimoja tu, si wengine tungekuwa hatuna ngozi kabisa?

Mpendwa, naomba nikwambie kuwa, kwa kusamehe, unajipatia kibali mbele za Mungu na kukuondolea magonjwa yako yote. Zaburi 103:3 "Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote".
Magonjwa haya si lazima uwe hoi kitandani, pengine unaweza hata ukawa na hasira tu, basi wee samehe ili Mungu akuondolee hasira hiyo, Samehe ili Mungu afute kumbukumbu ya ulivyokosewa na wala usije ukakumbuka tena. Tena ukimsamehe ongea nae vizuri, mtolee ushuhuda mzuri na umwombee sana ili Mungu amrehemu-Haleluya!

Nawasiki,tuepuke misamaha ya kinafiki ya kusema eti sitakusahau, huu si msamaha wa kweli., msamaha huu hautoki kwa Mungu, huu umetoka kwa shetani.Epuka na mizigo hiyo. Kumbuka Isaya 1:18,....dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji, zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa nyeupe kama sufu, na kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi. Rafiki yangu, inakuwaje wewe ukisamehe ukumbuke, ebu uache moyo wako mweupe usio na madoamadoa, usio na kinyongo! 
Kwanini Mungu amesema dhambi zako zitakuwa nyeupe wala si njano, orange au hata kahawia? Yesu anataka aweke utukufu ndani yako kupitia msamaha, achilia moyo wako, ili Bwana aingie akuponye magonjwa yote, aoundoe BP zako zote, aondoe vidonda vya tumbo katika jina la Yesu Kristo. Samehe uwekwe huru.
Waefeso 1:7 Katika yeye huyo (YESU) kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha (yaani mingi na mikubwa) ya dhaambi sawa sawa na wingi wa neema yake. Nakuomba usihesabu makosa bali uhesabu utukufu wa Mungu unaoupata kupitia Masamaha.
 
WEWE ULIYEGUSWA MAFUNDISHO HAYA RUDIA SALA HII HAPA CHINI.

Baba katika Jina la Yesu Kristo ninaomba nguvu ya msamaha wako; leo nimetambua kuna nguvu inayotenda kazi nyuma ya mtu aliyenikwanza,ninawasamehe wote walionikwaza katika Jina la Yesu. Ninatangaza msamaha, ninavunja madhabahu ya makwazo na kutokusamahe ndani yangu katika jina la Yesu Kristo. Baba ninaomba uniponye na matatizo yaliyoingia ndani yangu kwasababu ya kutokusamehe katika Jina la Yesu.

BASI BAADA YA KUPOKEA NGUVU YA ROHO MTAKATIFU NAOMBA NIKUOMBEE SASA ILI UDUMU KATIKA PENDO LA KRISTO.

Baba katika Jina la Yesu Kristo ninakushukuru kwa neno lako na msamaha wako kwa watoto wako, Ahsante Yesu kwa wote waliokili ujumbe huu!Baba naomba rehema zako ziwe juu yao tangu sasa, katika jina la Yesu Kristo, uwajaze roho ya msamaha na upendo. Ondoa magonjwa yao yote yaliyowatesa siku zote, futa visasi na laana za kutokusamehe katika Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu uliye hai.

Kwa Mawasiliano zaidi.......

Mwl. Sospeter Simon,
S.L.P. 568
Tukuyu.

Email: sos.sesi@yahoo.com
+255 784/757 464 141
+255 712 909 021

Monday, March 11, 2013

Safari kuelekea uchaguzi wa Papa yaanza kesho Vatican.

MCHAKATO  rasmi wa kumpata kiongozi wa Kanisa Katoliki  duniani atakayemrithi Papa Benedict XVI  aliyejiuzulu Februari 28, unaanza kesho. Katika mchakato huo, makardinali 115 wataingia kwenye Kanisa la Sistine kwa kazi hiyo ngumu ya kupiga kura.

Kura hiyo ya siri inatarajiwa kurudiwa mara kadhaa hadi apatikane  mtu anayekubalika. Tayari kanuni za uchaguzi huo zimeshaandaliwa zikiwamo za namna ya  kupiga kura kwa usiri na wasimamizi wa kura.

Makardinali  hao kutoka mataifa mbalimbali duniani, wamekuwapo Vatican  ambako kila walipowasili walikula kiapo cha kutunza siri wakati wote wa kikao hicho muhimu. Viongozi hao wa kidini, wataongozwa zaidi na sala na maombi kwa roho mtakatifu.

Kama  ilivyokuwa katika miaka ya nyuma,  kampeni haziruhusiwi katika mchakato huu mzima. Kukosekana kwa kampeni, hata hivyo, hakuzuii watu kutoa mawazo yao kuhusu nani angefaa kuchaguliwa.

Wengine wanaipa nafasi kubwa Italia, yaliko makao makuu ya kanisa hilo, Vatican, ingawa pia kuna  wale  wanaofikiri kuwa sasa ni zamu ya Afrika na Amerika Kusini kutoa kiongozi wa juu wa kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.2.

Pia, wengine wanadhani kuwa Ulaya, ambayo ina makardinali wengi zaidi, bado inastahili kutoa kiongozi huyo kama ilivyokuwa kwa Poland na Ujerumani katika miaka ya hivi karibuni.

Kwanini Afrika?
Sababu ya msingi inayotajwa kuipendelea Afrika kwa sasa ni, ongezeko la waumini wapya ambako takwimu zinaonyesha kuwa nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tanzania, Uganda  zimo katika  orodha ya 20  bora duniani kwa  waumini wengi wa Kikatoliki.

Afrika na Amerika Kusini, zikilinganishwa na mabara ya Ulaya na Marekani, zinaelezwa kuwa zina idadi kubwa ya waumini wapya , makanisa yake yanajaa, idadi ya mapadri inaongezeka, tofauti na Ulaya na Marekani inakopungua.

Makardinali wawili, Francis Arinze mwenye umri wa miaka 80, raia wa Nigeria na mwenzake, Peter Turkson (64) kutoka Ghana, wamekuwa wakitajwa kuwa miongoni mwa wale wanaofaa kwa kazi hiyo. Wakati wote wa mchakato huo, makardinali hao 115  hawatakuwa na mawasiliano yoyote na ulimwengu wa nje hadi apatikane papa mpya ndani ya wiki mbili.

Kwa pamoja, wataishi katika hosteli ya kisasa iliyomo ndani ya eneo hilo, umbali mdogo kutoka katika Kanisa la Sistine, ambalo milango na madirisha yake yamezibwa kuzuia watu kuchungulia ndani yake.

Hosteli hiyo ya kisasa inayojitegemea, imeandaliwa mahsusi kwa kazi hiyo, ikiwa na huduma zote za msingi. Ina madaktari, mapadri ambao watawahudumia makardinali hao wakihitajika.

Kila kardinali ataishi katika chumba chake kidogo chenye kitanda, meza ndogo na kabati la nguo, akisali zaidi na wakati huo akifanya tafakuri ya kina kati yake na Mungu ni nani hasa kati yao aliyeteuliwa kuliongoza kanisa hilo.

Inaelezwa kuwa wakati wote wa mchakato, makardinali hao hawazungumzi, bali kusali na kufanya tafakuri na kukutana wakati wa chakula.

Ni nchi gani zinawakilishwa?
Zipo nchi  kadhaa  ambazo zina uwakilishi  katika uchaguzi huo. Hizi ni pamoja na: Italia (28),  Marekani (11), Ujerumani (6), Hispania, India, Brazil (5) kila moja, Ufaransa, Poland (4) kila moja Mexico, Canada (3)  kila moja Ureno, Nigeria, Argentina ( 2) kila moja.

Australia, Austria, Ubelgiji, Bolivia, Bosnia Herzegovina, Chile, China, DR Congo, Colombia, Croatia, Cuba,Czech , Dominica, Ecuador, Misri, Ghana, Guinea,Honduras, Hungary, Ireland, Kenya,Lebanon, Lithuania, Uholanzi, Peru, Ufilipino, Senegal, Slovenia, Afrika Kusini, Sri Lanka, Sudan, Uswisi, Tanzania, Venezuela, Vietnam  (1) kila moja.

- Mwananchi -

Sunday, March 10, 2013

Yaliyojiri kwenye Uzinduzi wa kitabu cha "Wokovu ni Uhakika wa Maisha ya Sasa na ya Baadaye".

Bw. James Kalekwa(Mwandishi wa Kitabu)
LEO pale Isamo Hoteli ndani ya Jiji la Mwanza, kulikuwa na Uzinduzi wa Kitabu cha "Wokovu ni Uhakika wa Maisha ya sasa na ya Baadaye" kilichoandikwa na Mwandishi James Kalekwa ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo cha Mt. Augustino Mwanza, Idara ya Sosholojia.
Cover la Kitabu
Watu mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania walihudhuria Uzinduzi huo, na Kutoka Dar es salaam walikuwepo The Blogger Samuel Sasali pamoja na Mc wa Shughuli Pilipili a.k.a Handsome wa Kigogo.
Mc Pilipili katika Pozi
Wasemaji katika Uzinduzi huo walikuwa Mch. Goodluck Kyara (NVCC), Samuel Sasali na James Kalekwa. Sasa fuatana nasi kutazama picha hizi ya Jinsi tukio lilivyokuwa...
Kutoka kushoto ni Sarah pamoja na Neema
Pipooooo............
Watumishi wa Mungu
Marafiki waliokuja kumuunga Mkono Bw. James Kalekwa
Sehemu ya Praise Team
Praise Team
Ruth Lyanga
Raisi wa Wapiga Vinanda Mwanza, Bw. Sephone Sospeter
Joel Kaema akiongoza Wimbo wa kuabudu
Baadhi ya Watu waliohudhuria
Watumishi wa Mungu kutoka MICC
Bw. Samuel Sasali
James Kalekwa akiwa na Mgeni Rasmi
Kushoto ni Bishop Irene Nzwalla wa Hosanna Christian Centre
Miss Adela Mwampamba, Mtangazaji Hhc Alive Fm
Wazungumzaji
Mc Pilipili akifanya Vitu vyake
Mch. Goodluck Kyara wa New Vine Christian Centre
Sehemu ya Watu waliohudhuria
Kitabu kikizinduliwa Rasmi
Hapo vipiii....
The Team
Bloggers: Kutoka kushoto ni Samuel Sasali, Sowane Emmanuel na Baraka Samson
Blogger Sowane Emmanuel with Mc Pilipili

Saturday, March 9, 2013

Uzinduzi wa Kitabu cha "Wokovu ni Uhakika wa Maisha ya Sasa na ya Baadaye".

 
SIKU ya Jumapili ya Tarehe 10 Mwezi wa 3 Mwaka huu, kutakuwa na Tukio la Uzinduzi wa Kitabu Kinachoitwa "WOKOVU NI UHAKIKA WA MAISHA YA SASA NA YA BAADAYE" kilichoandikwa na Mwandishi James Kalekwa ambaye ni Mkufunzi Msaidizi wa Idara ya Sosholojia katika chuo Kikuu cha Mt. Augustino.
Cover la Kitabu hicho
Shughuli hiyo itafanyika Katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Isamo Hotel, Jijini Mwanza, na Wazungumzaji katika Uzinduzi huo ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la New Vine Christian Centre Mch. Goodluck Kyara - Mwanza, Samuel Sasali - Dar, na Mwandishi wa Kitabu hicho James Kalekwa -  Mwanza.
MD Adolph Robert Nzwalla - Hosanna Praise Team
Uzinduzi huo hauna Kiingilio, na Vikundi vya Kusifu na Kuabudu vitakuwepo chini ya MD Adolph Robert Nzwalla. Mc Pilipili ya Shughuli atakuwepo kupamba Uzinduzi huo.

WOTE MNAKARIBISHWA!

Friday, March 8, 2013

Kutana na Goodluck Gozbert a.k.a Goody.

Goodluck Gozbert a.k.a Goody ni Mwimbaji wa Nyimbo za Injili toka Mkoani Mwanza, Tanzania ambako ndiko alikozaliwa. Goodluck alizaliwa April 12, Mwaka 1991 katika hospitali ya Bugando, Mwanza. Akiwa ni Mtoto pekee wa Bw. Gozbert Rweyemamu pamoja Janeth Gozbert, Goodluck alilelewa na Mama yake pekee baada ya Baba yake mzazi kufariki huku Goodluck akiwa na Umri wa Mwaka 1.
 
Goody anasema alianza kazi za uimbaji Mwaka 2005 akiwa na Tumaini Choir (K.K.K.T- Imani Mwanza). Baada ya Miaka 3 yaani 2008, Goody alianza kuimba nyimbo zake pekeyake huku akiwa bado ni miongoni mwa waimbaji wa Kwaya ya Tumaini (K.K.K.T- Imani Mwanza).
 
Goody alitoa Album yake ya Kwanza Agosti 19, 2008 aliyoifanya katika Studio ya Ujumbe Records chini ya Meneja wake Abraham Nyantori. Katika Utengenezaji wa Album hiyo, Goody alifanya kazi na Maproducer mbalimbali wa Jijini Mwanza kama Selemani Muyomba, na Charles Sokoro.
 
Mwaka 2012 Goody alianza kurekodi Album yake ya 2 aliyoipa Jina la NIMEUONA, ambalo ni Jina la Moja ya Nyimbo zinazopatikana katika Album hiyo. Katika Album hiyo kuna Nyimbo kama vile Nimelipiwa Deni, Nimeuona na Wa Moyo(Wimbo unaopendwa sana na Watu wengi na ni Wimbo Unaofanya vizuri sana katika vituo mbalimbali vya Nyimbo za Injili Kanda ya Ziwa).
 
Mbali ya Uimbaji Goody anauwezo mzuri wa kupiga Kinanda, Drums, Guitar, na Trumpet, Vyombo alivyojifundisha yeye Mwenyewe akiwa kanisa la K.K.K.T- Imani chini ya Tumaini Choir. Goody pia ni Mwandishi wa Nyimbo,  Mtayarishaji wa Nyimbo(Audio Producer), Mwandishi wa Script, Muongozaji wa Filamu na Pia ni Muigizaji. Baadhi ya Nyimbo katika Album yake ya 2 amezitengeneza yeye Mwenyewe kuanzia Utunzi, Utengenezaji wa Beat pamoja na Kufanya Mixing.
Tazama Video hii ya Goodluck Gozbert, Jina la Wimbo ni Nimelipiwa Deni

Mawasiliano ya Goodluck Gozbert
0762486168