Maafisa wa polisi wakichunguza kaburi alimozikwa Padre Dominic Jordan katika makaburi ya Mathari Consolata Mission Nyeri Agosti 20, 2013. |
MATAYARISHO ya
kumzika tena Kasisi Dominic Jordan ambaye mwili wake ulifukuliwa kutoka
kwa kaburi lake huko Mathari,Nyeri mnamo siku ya Jumanne yanaendelea.
Makasisi wa kanisa katoliki wamemteua Kasisi Gachanja ili kuandaa matayarisho ya mazishi hayo ambayo yatakuwa ya kipekee kufanyiwa Kasisi wa Kanisa katoliki hapa nchini.
Makasisi wa kanisa katoliki wamemteua Kasisi Gachanja ili kuandaa matayarisho ya mazishi hayo ambayo yatakuwa ya kipekee kufanyiwa Kasisi wa Kanisa katoliki hapa nchini.
Alhamisi
Polisi walithibitisha kwamba mwili wa Kasisi Jordan ulikuwa na viungo
vyote huku wakishuku kwamba wahalifu wanaoshukiwa kuchimba kaburi lake
maarehemu walikuwa na nia ya kuiba mali.
Mwili huo
hata hivyo ulikuwa umeoza kiasi kwamba ilibidi Mwalimu mkuu wa shule
ya upili ya St.Mary’s aitwe ili kuutambua mwili wa kasisi kwa kutumia
mavazi aliyovalishwa wakati wa mazishi yake.
Marehemu
Kasisi Jordan alikuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo kabla ya kifo chake.
Viatu alivyovalia, shungi la nywele kichwani mwake na kola inayovalishwa
makasisi wa Kanisa Katoliki ya Kirumi ndivyo vitu vilivyotumika
kuutambua mwili wa marehemu.
Kasisi Jordan
anasifika kwa kuwasaidia wanafunzi wengi kujiunga na chuo kikuu maarufu
cha Harvard huko marekani wakati wa huduma yake.
Akiongea na Taifa Leo kupitia
kwa simu Afisa Mkuu wa Polisi mjini Nyeri bwana Joseph Mwika alisema
tofauti na ilivyodhaniwa hapo awali, ni mwili wa Kasisi Jordan ambao
ulitolewa kwa Jeneza na kuwekwa kando ya kaburi na wala hapakuwa na
miili miwili ndani ya kaburi.
Bwana Mwika
alisema mwili huo ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha
Hospitali ya Konsolata Mathari huku matayarisho ya mazizi yakiendelea.
Afisa huyo
aliongezea kwamba uchunguzi bado unaendelea lakini itakuwa vigumu
kutoa ushahidi kwa bidhaa alizotumia mshukiwa kuchimba kaburi kwani
mshukiwa huyo alikuwa amevalia glovu kwa mikono yake ili kuficha alama
za vidole.
Glovu alizovalia mshukiwa zilipatikana kando ya kaburi pamoja na jembe na sepetu.
Wakati huo huo Naibu wa Kamishna wa Kaunti ya Nyeri amewataka wakaazi kutohusisha tukio hilo na ushirikina.
Akiongea na
waandishi wa habari Naibu wa Kamishna bwana John Marete alisema tukio
hilo lilikuwa ni uhalifu wa kawaida uliotekelezwa na watu waliodhania
watapata mali kwenye kaburi la marehemu na wala lisihusishwe na mambo
mengine.
“Kama
wakristo hatuamini ushirikina, tusifikirie kuna mambo mengine kuhusu
tukio hili.Hili ni jambo la haibu na lisilostahili kutendeka katika
jamii iliyostaharabika,”akasema bwana Marete.
Kasisi
Bartholomew Mwangi kwa upande wake alisema visa kama hivi vinaonyesha
ukosefu wa maandili katika jamii lakini akasisitiza kwamba kanisa
linatekeleza jukumu lake la kuwafunza wanadamu maadlili mema.
- Swahili Hub -