POLISI Jumatatu walilipua mabomu
mawili yaliyokuwa yametegwa kwenye lango la Kanisa la Soldiers of Faith,
eneo la Kiamaiko, Kaunti ya Nairobi. Mabomu hayo, moja lenye uzani wa kilo tano na lingine kilo mbili, yalipatikana na wananchi.
Wataalamu wa
mabomu waliyatwaa mabomu hayo kuyalipua wakisema yalikuwa na uzito
mkubwa na kwamba yangesababisha hasara kubwa kama yangelipuka yalipokuwa
yamewekwa.
“Hatungelilipua mabomu hayo mahali yalipokuwa kwa sababu
yangeleta hasara kubwa katika eneo hilo,” akasema afisa mkuu wa polisi
eneo la Starehe, Bw Samuel Anampiu.
Alisema
polisi “hawawezi kukana dhana kwamba kanisa hilo lilikuwa linalengwa na
washambulizi. Mabomu haya ni muundo ule uliotumika wakati wa vita vikuu
vya kwanza na vya pili vya dunia. Yangali na nguvu na ni hatari sana.”
Bw Anampiu alisema mabomu hayo yalikuwa na uwezo wa kubomoa majumba na kufanya eneo hilo tambarare kama yangelipuka.
Aliwapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kuchukua hatua ya haraka na kuwaarifu polisi.
“Tunatambua
juhudi za wakazi wa hapa kwa kuwaarifu polisi badala ya kukaa kimya
kuhusu mabomu haya ambayo ni hatari kubwa kwa kila mtu,” akasema
Anampiu.
Bi Maureen Adhiambo aliyeona bomu la kwanza, alisema alikuwa anasafisha lango la kanisa hilo alipoona kifaa hicho.
“Nilivuta kifaa hicho lakini kilikuwa kizito ndipo nikamwambia jirani na kumuomba ushauri,” akasema.
Alisema
aliona bomu hilo mwendo wa saa tatu asubuhi na kwamba watu wachache
walilichezea kabla polisi kufika. Bw Husein Nura, mkazi wa eneo hilo
aliyemsaidia Bi Adhiambo kuondoa bomu hilo, alisema lilikuwa zito.
“Nilimwambia kwamba kifaa hicho si cha kawaida na huenda ni bomu,” akasema Bw Nura.
Muda mfupi baadaye, polisi walibeba bomu hilo kwa mfuko mweusi uliojaa changarawe. Bomu la pili lilipatikana muda mfupi baadaye.
Polisi
walizingira eneo hilo huku wakitumia mbwa wa kunusa kutafuta mabomu
zaidi. “Tumetafuta mabomu zaidi tukutumia mbwa wa kunusa. Hatujapata
mengine na tuna hakika eneo hili ni salama sasa,” akasema Bw Anampiu.
Aliwatahadharisha
wanaouza na kununua vyuma vikuukuu wajihadhari na vifaa vya chuma
wasivyofahamu. Mkuu huyo wa polisi alisema hakuna mshukiwa aliyekamatwa
kuhusiana na mabomu hayo.
Tukio hilo lililemaza biashara zote katika eneo hilo huku wakazi wakimiminika kanisani humo kuona mabomu hayo.