Advertise Here

Tuesday, September 17, 2013

Operesheni "Kimbunga" yakamata wachungaji zaidi.

Ofisa Uhamiaji Mwandamizi, Julieth Sagamiko akimworodhesha raia wa Malawi na mtoto wake katika ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam jana ambako mamia ya wahamiaji haramu kutoka nchini humo walijitokeza kujiorodhesha ikiwa ni sehemu ya agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuwarejesha kwao wageni wasio na vibali. (Picha na Mroki Mroki).
Afisa Uhamiaji Mwandamizi, Julieth Sagamiko akimworodhesha Raia wa Malawi na Mtoto wake katika Ofisi ya Uhamiaji Dar es salaam
MSAKO wa wahamiaji haramu kupitia Operesheni Kimbunga inayoendelea nchini, umejikita kanisani kutokana na wahamiaji haramu sita wa Nigeria, kubainika wakijishughulisha na kazi za kichungaji.

Akizungumza jana kwa niaba ya Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Hokororo, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Sylvanus Mwakasekele, alisema wahamiaji hao walikuwa katika Kanisa la Praise la Tabata.

Kwa mujibu wa Mwakasekele, Uhamiaji walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu kuwapo kwa wahamiaji hao kwenye Kanisa hilo.

Baada ya taarifa hiyo, alisema maofisa Uhamiaji walifika kanisani hapo juzi saa tano asubuhi na watu hao walipogundua, waliruka madirishani kukwepa mkono wa sheria na kukimbia wakitumia gari dogo aina ya Toyota Vitz.

“Walipokimbia walikuwa sita, vijana waliokwenda kufanya kazi hiyo waliwafuatilia na walipoona wako hatarini kukamatwa walitelekeza gari na kukimbia kwa miguu na kukamatwa wanne huku wawili wakitoroka,” alisema Mwakasekele na kuongeza kuwa wako katika harakati za kusaka waliokimbia.

Aliwataja waliokamatwa na jinsi walivyoingia nchini, ni Moses Opara mwenye pasipoti namba A04809965, ambaye alikuwa kiongozi wa Kanisa hilo na ameishi nchini kwa miaka mitatu.

James Ateli mwenye pasipoti namba A04665804, aliyeingia nchini kama mfanyabiashara na kuishi kwa mwaka mmoja. Pia Keneth Onyebuchi aliyeingia nchini kama mfanyabiashara tangu Januari na kudai kupoteza pasipoti yake alipoingia nchini na mwingine ni Augustine Ndubilisi aliyeishi nchini mwaka mmoja.

“Huyu Augustine anadai anaishi na familia ya mchumba wake Mtanzania aliyetajwa kwa jina la Caro Mdegela, msichana huyu tunamshikilia kwa kuhifadhi wahamiaji haramu,” alisema.

Alisema baada ya kukamilika kwa mahojiano na watu hao, watafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuishi nchini bila kibali muda wowote kuanzia leo.

- Habari Leo -