Rais Jakaya Kikwete |
RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kushiriki maziko ya Askofu Mkuu
wa Kanisa la EAGT, Moses Kulola (86), aliyefariki Agosti 29, jijini Dar
es Salaam. Maziko hayo yatafanyika katika Kanisa la EAGT Bugando, ambapo
ibada ya maziko, inatarajiwa kuanza kati ya saa 3 na 4 asubuhi na
maziko yatakuwa kati saa 4 na 7.30 mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa Mwanza, Evarist
Ndikilo, alisema Rais Kikwete anatarajiwa kuwasili leo, ambapo
atashiriki maziko ya Askofu huyo na baada ya hapo, atakuwa na ziara ya
wiki moja mkoani Mwanza.
“Atafanya ziara katika wilaya zote saba za mkoa wa Mwanza na atakagua
shughuli mbalimbali za maendeleo zinazofanyika katika wilaya hizo,”
alisema Ndikilo.
Alisema baadhi ya shughuli anazotarajiwa kuzifanya ni kuzindua miradi
ya nishati, ukiwemo mradi wa MCC unaofadhiliwa na Wamarekani katika
wilaya za Sengerema, Ilemela, Misungwi, Nyamagana na Magu.
Alisema wilayani Sengerema kuna maeneo 30 ya mradi huo, Misungwi
maeneo mawili, Ilemela mawili, Nyamagana mawili na Magu eneo moja la
mradi, ambapo mradi huo utazinduliwa katika eneo la Bukokwa wilayani
Sengerema. Pia katika ziara hiyo, Rais atazindua mradi wa kufua umeme wa
megawati 60 katika eneo la Nyakato jijini Mwanza.
Kwa upande wa biashara, Rais ataweka jiwe la msingi katika jengo la
kitega uchumi cha biashara lililopo eneo la Ghana na kufungua hoteli ya
Gold Crest. Ndikilo alisema kwa maeneo ya afya, atazindua zahanati ya
Rugeye, maabara ya hospitali ya wilaya ya Ukerewe na mashine ya X- ray
katika hospitali ya Misungwi, ambayo ni ahadi yake ya muda mrefu,
itakayowasaidia wananchi wa wilaya.
Kwa upande wa elimu, atafungua shule ya msingi Itulya iliyojengwa kwa
msaada wa shirika la Marekani yenye madarasa saba na kuweka jiwe la
msingi katika jengo la ghorofa tatu kwa ajili ya ofisi ya Mkuu wa wilaya
ya Magu. Aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi wakati Rais
atakapokuwa kwenye ziara katika maeneo yao.
- Habari Leo -