Mwl. James Kalekwa |
Somo linaendelea.....
Kusoma Sehemu ya Kwanza Bofya Hapa
Mihula Mitatu ya Maisha ya Mwanadamu
Nimechagua kuiwasilisha mihula mitatu kwa kutumia taswira
hii ifuatayo ambayo tutakuwa tukiirejea kila mara kwa kadiri tunavyoendelea
kujifunza juu ya dhana ya kufanya maamuzi hasa kwa mwanga wa maneno ya Mungu
kwa kinywa cha Nabii Yoeli.
Kwenye Hatua ya Pili: Baada ya Kuzaliwa mpaka Kifo, hapo ndo kwenye BONDE LA KUKATA MANENO.
Maisha kabla ya kuzaliwa
Luka
1:30-33
“Malaika akamwambia, Usiogope,
Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa
mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa mwana
wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.
Atamiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.”
Mathayo
1:21
“Naye
atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa
watu wake na dhambi zao.”
Ni jambo gani linakuijia mawazoni usomapo mistari hiyo?... Hata mimi
kwa muda nilikuwa ninaona mafundisho ya Krsimasi kila nisomapo mpaka
nilipofunuliwa jambo hili kwa namna ya tofauti. Hawa watakatifu wawili,
waandishi wa Injili, wanaleta picha ya namna ya kipeke sana katika habari ya
kuzaliwa kwa Yesu.
Hebu wacha nikuonyeshe kitu hapa… Kama umesoma vizuri na kwa
umakini katika mistari hiyo utagundua ya kwamba imeandikwa kabla Yesu Kristo
hajazaliwa. Mtakatifu Luka ameandika habari kabla hata ya mimba ndani ya
Mariamu; na Mathayo ametueleza habari hiyo wakati wa mimba – lakini yote kwa
yote ni kabla ya kuzaliwa kwa Yesu. Kitu gani unaona? Malaika anazungumza na
Mariamu na kutaja jinsi ya mtoto kuwa atakuwa mwanaume, anataja jina la mtoto
kwamba ataitwa Yesu na anataja baadhi ya majukumu yake baada ya kuzaliwa, yaani
wakati wa kuishi kwake.
Hebu tazama kitu anachotuonyesha Mathayo, malaika
anamtokea Yusufu ndotoni na kumpa habari kwa upana wake na katika habari hizo
malaika anataja jina la mtoto na anataja kusudi la kuja kwake ulimwenguni. Yote
hayo yanatajwa kabla ya mtoto kuzaliwa, yaani kabla hajaanza kuishi na kutembea
ulimwenguni tayari ameshajulikana kwa namna kubwa sana, taarifa zake
zinajulikana, jina lake, jinsi yake na kusudi la kuwepo kwake linajulikana.
Wengi hudhani kwakuwa ni Yesu, mwana wa Mungu, hivyo kwake ilipaswa
kuwa dhahiri- ilikuwa ni ya kipekee (special case). Kabla hujahitimisha hivyo
ni vyema ukumbuke kuwa Yesu alikuwa mwanadamu asilimia mia moja na Mungu
asilimia mia moja, kwahiyo tunapozungumzia sehemu yake ya uanadamu ni vyema
tukatazama kwa jicho hilo tu… Si unajua kuzaliwa ni sehemu ya uanadamu?
Naomba uambatane na mimi katika kutanua wigo wa uelewa kwa kuyasoma
maisha ya watu wengine katika neno la Mungu kisha Tujifunze jambo kwa pamoja.
Yeremia 1:6
“Kabla sijakuumba katika tumbo
nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa
mataifa.”
Waamuzi
13:5
“kwani tazama, Utachukua mimba,
nawe utamzaa mtoto mwanaume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto
huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na
mikono ya Wafilisti.”
Katika andiko la awali utagundua ya kwamba Mungu anazungumza na
Yeremia akiwa tayari anaishi, amekwisha kuzaliwa tayari, na anamweleza kabla ya
kutungwa mimba Yeremia alikuwa anajulikana kwa Mungu tayari. Ndiyo kusema japo
Mungu hakuwaeleza wazazi wa Yeremia au kujifunua kwa mtu yeyote kueleza kuhusu
Yeremia hiyo haiubadalishi mstari wa sita wa sura ya kwanza kwamba Yeremia
alijulikana na Mungu. Kama Mungu alimjua Yeremia uwe na uhakika alimjua jinsi
na kusudi la kuwepo kwake duniani…
Kwahiyo wakati mimba inatungwa, Mungu hakuwa
anaona mimba, bali alikuwa anaona nabii wa mataifa. Kabla wazazi wa Yeremia
hawajakutana, Mungu bado alikuwa anaona nabii wa mataifa. Si kwamba Mungu
alianza kumjua Yeremia baada ya wazazi
wake kukutana, bali Mungu aliwakutanisha wazazi wake Yeremia ili wapate fursa
ya kumfahamu Yeremia.
Kwenye andiko linalofuatia ni ujumbe wa malaika kwa familia ya
wanandoa ambao bado walikuwa hawajawahi kupata mtoto maishani mwao. Malaika
anamtokea mama mtarajiwa, ambaye wakati huo alikuwa ni mwanamke tasa, na
anaanza kumpa habari za mtoto wake wa kiume na anaenda hatua ya mbele zaidi kwa
kumweleza kusudi la kuja kwa mwanaume huyo ulimwenguni na namna gani anapaswa
kulelewa…
Hii inaweza kuonekana ni habari ya kiuendawazimu kidogo, kutoa habari
kamili juu ya mtoto fulani kwa mwanamke tasa!!! Malaika anatoa wapi ujasiri wa
namna hiyo? Amepewa hizo taarifa na Mungu, kwahiyo malaika hakuwa anabahatisha
au anajaribu kutoa utabiri bali alikuwa anazungumza ukweli, yaani ndivyo
ilivyo. Huyu mtoto wa kiume alikuwa anajulikana kwa Mungu kwahiyo ilikuwa ni
habari sahihi kutoka chanzo sahihi cha habari.
Kwa mwanga wa uelewa huo nilioweka msingi ndani yako naomba ujiulize
je, unadhani kuzaliwa kwako duniani kumemshitukiza Mungu? Je, Mungu
ameshangazwa na uwepo wako (Is God caught by surprise by your existence?) yaani
namaanisha unadhani Mungu amesema “Oooh!!! Kumbe huyu aliyezaliwa ni James?” au
“Ahaa!!!
Kumbe leo amezaliwa Sowane?” siku ambapo mimi nilizaliwa au siku
ambapo ndugu Sowane alizaliwa?. Hapana, Yahwe si Mungu mdogo kiasi hicho eti
kwamba kuna matukio yanamshangaza au kumshitukiza! Angekuwa hivyo, basi
asingeweza kuuongoza ulimwengu. Katika lugha ya elimu ya theolojia, Mungu
hutambulishwa kama “omniscient” yaani mwenye ufahamu yote- anayejua mambo yote!
Natambulisha ufahamu huu ya kwamba kabla ya kuwepo ulikuwepo na
ulijulikana kwa Mungu! Ulikuwa ndani ya mawazo na fikra za Mungu kabla
hujatokea duniani. Ulifahamika jinsi na kusudi la kuwepo kwako kabla
hujadhihirika katika ulimwengu wa mwili.
Lakini ni muhimu sana ukarejea mistari
hiyo juu na kuona ya kwamba aliyekuwa ni chanzo cha taarifa za kuzaliwa,
kuishi, kusudi la wanadamu hao alikuwa ni Mungu na hakuna mwingine- hata
malaika!
Hiyo ni udhihirisho ya kwamba aliyefanya maamuzi ya jinsi, nyakati na
kusudi la kuzaliwa ni Mungu pekee. Ni dhahiri ya kwamba ukiambiwa ufikiri
ulikuwaje kabla ya kuzaliwa, picha itakayo kuijia mawazoni mwako ni giza tu!
Hukuwa na ufahamu na uelewa na hukuwa na maamuzi ya kuzaliwa kwako.
Binafsi,
sikuamua kuzaliwa mtanzania, lakini ile kujua kwamba nimezaliwa kuwa mtanzania
ni furaha sana ndani ya moyo wangu kwasababu ni udhihirisho kwamba aliyeniweka
amekusudia kitu kwa nchi ya Tanzania kupitia mimi na ndiyo maana akaniweka. Ile
kwamba mimi ni mwanaume ninatambua si kwa bahati nzuri au mbaya bali ni kwa
kusudi… Nilijulikana kwa Mungu lakini sikuwa na uwezo na nafasi ya kufanya
maamuzi yoyote na hivyo siwajibiki na maamuzi ya kuzaliwa na kuwepo kwangu.
Hakuna mtu anaweza kunihoji kwanini nilizaliwa mtanzania na si mtu wa taifa
jingine, sipaswi kupongezwa au kulaumiwa kwa kuzaliwa mwanaume, wala siwajibiki
kwa kuzaliwa na kuishi kwangu katika zama hizi. Kwani kuna mtoto unaweza kumpa
hongera au kinyume chake kwa kuzaliwa kipindi cha siasa za vyama vingi hapa
Tanzania? Unadhani kuna mzee wetu yeyote anayestahili kuadhibiwa kwa kuzaliwa
kipindi cha mapambano ya uhuru?
Hapana!!! Kwasababu hakuna kati yetu
aliyeshiriki kufanya maamuzi hayo lakini hiyo haiubadili ukweli kwamba sote
tulijulikana kwa Mungu kabla ya kuzaliwa kwetu.
Somo litaendelea jumatatu Ijayo.....
Somo limeandaliwa na:
Mwl. James Kalekwa
0714 762669/0754 917764
Email: jameskalekwa@gmail.com