James Kalekwa |
Somo linaendelea....
Kusoma sehemu ya Kwanza, Bofya Hapa
Mwamba
1: Tawala nafsi
yako kwa kuongoza milango yako ya fahamu.
Mithali 4:23
"Linda sana
moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za
uzima."
Ili uweze kusaidika juu ya habari ya nafsi ni muhimu sana kutambua na
kukumbuka siku zote mwanadamu ni nani, wewe ni nani au ni kiumbe wa namna
gani. Wewe ni roho yenye nafsi
inayoishi ndani ya mwili.
Rejea kitabu cha Mwanzo 2:7, " BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya
ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai." Ambapo utaona mwanadamu ni muunganiko wa mavumbi ya
ardhi, pumzi ya uhai na nafsi hai… Kwa msingi huo basi mavumbi ndiyo mwili,
pumzi ya uhai ni roho na nafsi hai ni nafsi!
Ukienda ndani ya neno la Mungu utakuta lile eneo la nafsi linazungumziwa
kwa lugha au tafsiri tofauti tofauti kwa maana ileile. Kuna nyakati Biblia
inatumia neno “moyo”, “nafsi”, “ufahamu”, “roho” kuelezea eneo moja tu la
mwanadamu nalo ni nafsi. Kwasababu hiyo nakuomba ufungue macho yako kuyatazama
maandiko kwa maana pana zaidi. Hebu tazama mstari huo kwa tafsiri za
kiingereza: “Guard your heart above all else for it determines the course of your
life." (NLT)
"Linda moyo wako zaidi ya vitu vyote kwasababu moyo wako ndiyo
huamua mwenendo/mtiririko wa maisha yako."
"keep your heart with all diligence, for out of it springs out
the issues of life." (KJV)
"Linda moyo wako kwa umakini mkubwa sana ,kwasababu moyo wako
hububujisha mambo yahusianayo na maisha."
Kimsingi tafsiri zote zinatuelekeza kwenye uelewa kwamba maisha ya
mwanadamu huamuliwa na moyo wake, mwenendo/mtiririko wa maisha hujengwa ndani
ya moyo, chemchemi/chanzo cha maisha ya mwanadamu ni moyo! Natamani uone kwa
ukubwa ambao mwandishi wa Mithali anaukusudia uuone… Ya kwamba chochote
kinachotokea kwenye maisha yako, kimetokea moyoni mwako. Yaani kama moyo wako
ni kiwanda na maisha yako ni bidhaa itokayo ndani ya kiwanda hicho na kwa
uelewa huo basi, ni dhahiri ya kwamba kama hupendi bidhaa fulani usikurupuke
kuiangamiza bidhaa hiyo kwasababu utakuwa umetatua tatizo kwa muda (immediate
solution), bali unapaswa kudhibiti uzalishaji unaofanywa kiwandani. Au kama
hupendi mazao yaliyomo gharani mwako, tafadhali usiyachome mazao hayo kwasababu
utakuwa unatatua kwa muda, bali chukua hatua ya kudhibiti shughuli za shamba…
Mungu akusaidie sana uelewe hapa!
Kwakuwa moyo ni sehemu muhimu kiasi hiki, basi tunapaswa kujua bayana na
kwa uhakika tunaposema moyo tunamaanisha nini hasa ili tusijikute tunazungumza
mambo tusiyoyajua “vague”…
Ukishauelewa moyo basi umepata mtaji wa ushindi!
Kila mara ninapozungumza na vijana wenzangu huwa napenda kuwapa tahadhari ya
kwamba moyo wa mwanadamu, huu unaozungumwa hapa si ule wa kwenye masomo ya
sayansi hasa somo la Baiolojia….
Ninachofundisha hapa ni zaidi ya ule moyo wenye
kazi ya kusambaza damu mwilini, kwasababu moyo usambazao damu umeumbwa kwa damu
na nyama, yaani huo ni sehemu ya mwili na kwa uelewa nilioujenga kwako ni
kwamba mwili ni mavumbi ya ardhi. Si kazi ngumu sana kung’amua kwamba moyo
usambazao damu mwilini nao ni nyama (ni mwili) kwasababu baada ya roho kutoka,
mtu kufariki, mavumbi (mwili) hurudi mavumbini… na moyo huo wa kwenye somo la
Baiolojia huwa sehemu ya virudivyo mavumbini.
Kwahiyo kwa kutazama kuwa mwanadamu ni roho yenye nafsi inayoishi ndani
ya mwili….uwe na uhakika Biblia inaposema "moyo" katika andiko hili haimaanishi moyo wa nyama
na haimaanishi roho bali inamaanisha nafsi. Kwahiyo unapojifunza katika eneo
hili naomba ubebe mtazamo wa nafsi ili uelewe vizuri zaidi.
Neno la Mungu
linatanabaisha kuwa moyo/nafsi ndiyo
huamua mwenendo wa maisha yetu na hububujisha mambo yahusianayo na maisha yetu
kwa tafsiri nyepesi ni kwamba jinsi ulivyo ndivyo ulivyoamua kuwa; na uamuzi
huo umefanyika ndani ya nafsi yako Mithali 23:7a,"Maana aonavyo nafsini
mwake ndivyo alivyo." Hakuna mtu anapaswa kulaumiwa bali ndivyo
ulivyoamua.Basi kama nafsi ni sehemu ya muhimu kiasi hicho, tunawajibu mkubwa
sana kulinda sana nafsi zetu.
Hebu tuitazamae nafsi kwa mfano wa hazina…. Naomba uyaelekeze mawazo
yako kwenye maisha ya kawaida kabisa, maisha ya kila siku. Ninaamini kwamba
umeshawahi kusikia ama wewe au mtu anayekuhusu ni mtumiaji wa huduma za kifedha
kwa njia ya simu ya mkononi. Kwa hapa Tanzania kuna huduma ya M-Pesa, Z Pesa,
Airtel Money na Tigo Pesa…
Kwa mfano huo basi, hebu mfikirie mtu ambaye hufunga
safari kwenda kutoa pesa (kwa mtoa huduma) wakati anajua fika ya kwamba hana
akiba/salio kwenye akaunti yake. Huyo ni sawa na mkulima ambaye wakati wa msimu
wa mavuno unapofika yeye hufunga safari kwenda shambani ili akaanze shughuli ya
kuvuna wakati anafahamu wazi ya kwamba hakuna siku ambayo aliwahi kuweka mbengu
ndani ya shamba hilo… Inawezekanaje kuvuna wakati hujapanda? Kwa lugha ya
kiingereza wanasema “you can not give what
you do not have.”.
Ni ukosefu wa akili timamu ndiyo utamwongoza mtu kwenda
kutoa pesa kwenye akaunti ambayo haina pesa (na muhusika hajawahi kuongeza
pesa); ni upumbavu kwenda kuvuna kwenye shamba ambalo hujawahi kupanda mbegu
yoyote.
Nimetumia mifano hiyo kukuleta kwenye dhana moja ya Muhimu sana ya
kwamba kabla ya kutoa pesa kwenye akaunti unapaswa kuweka pesa; kabla ya kuvuna
unapaswa kupanda mbegu. Kama basi inaonekana ni hekima kwa mkulima na mtumiaji
wa huduma za pesa kwenye simu ya mkononi… ni hekima zaidi kwa mtumiaji wa moyo,
mtumiaji wa nafsi ambaye ni wewe. Kabla hujavuna au hujatoa chochote kutoka
kwenye nafsi yako, ni wajibu wako kuweka kitu.
Somo litaendelea Jumatatu Ijayo....
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu, na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu, na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com